< Hesabu 8 >

1 BWANA akanena na Musa, akamwambia,
Bwana akamwambia Mose,
2 “Sema na Haruni umwambie, 'zile taa saba lazima zimulike mbele ya kinara utakapoziwasha,”
“Sema na Aroni umwambie, ‘Wakati utakapoziweka zile taa saba, zinatakiwa kuangaza eneo lililo mbele ya kinara cha taa.’”
3 Haruni alifanya haya. Aliziwasha zile taa juu ya kinara ili ziangaze mbele yake kama BWANA alivyomwagiza Musa.
Aroni akafanya hivyo; akaziweka zile taa ili zielekee mbele kwenye kinara cha taa, kama vile Bwana alivyomwamuru Mose.
4 Kinara kilitengenezwa kwa njia hii kama BWANA alivyomwelekeza Musa muundo wake. Kiitakaiwa kutengenezwa kwa dhahabu kuanzia kwenye kitako chake hadi juu, ndivyo kilivyotakiwa kutengenezwa kwa dhahabu kwa maua hadi juu.
Hivi ndivyo kinara cha taa kilivyotengenezwa: Kilitengenezwa kwa dhahabu iliyofuliwa, kuanzia kwenye kitako chake hadi kwenye maua yake. Kinara cha taa kilitengenezwa sawasawa kabisa na kielelezo ambacho Bwana alikuwa amemwonyesha Mose.
5 Tena, BWANA akanena na Musa, akasema,
Bwana akamwambia Mose:
6 '“Uwatwae Walawi kati ya wana wa Israeli na uwatakase.”
“Watwae Walawi kutoka miongoni mwa Waisraeli wengine na uwatakase kwa kawaida ya ibada.
7 Uwafanyie hivi ili kuwatakasa: Uwanyunyizie maji ya utakaso juu yao. Hakikisha wamenyoa miili yao yote, wafue nguo zao, na kwa njia hii wajitakase wenyewe.
Ili kuwatakasa fanya hivi: Nyunyizia maji ya utakaso juu yao; kisha uwaambie wanyoe nywele kwenye mwili mzima, wafue nguo zao na hivyo wajitakase wenyewe.
8 Kisha wachukue fahari mchanga na sadaka ya unga mwembamba uliochanganywa na mafuta. Halafu wachukue fahari mchanga kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
Waambie wamchukue fahali mchanga pamoja na sadaka yake ya nafaka ya unga laini uliochanganywa na mafuta; kisha utamchukua fahali mchanga wa pili kwa ajili ya sadaka ya dhambi.
9 Uwalete Walawi mbele ya hema ya kukutania, na uwakusanye jamii yote ya wana wa Israeli.
Walete Walawi mbele ya Hema la Kukutania na ukusanye jumuiya yote ya Waisraeli.
10 Uwalete Walawi mbele yangu, BWANA. Wana wa Israeli wataweka mikono yao juu ya Walawi.
Utawaleta Walawi mbele za Bwana, na Waisraeli wataweka mikono yao juu ya Walawi.
11 Haruni atawatoa Walawi mbele yangu, kuwa sadaka ya kutikiswa. Atafanya hivi ili kwamba Walawi wanitumikie.
Aroni atawaweka Walawi mbele za Bwana kama sadaka ya kuinua kutoka kwa Waisraeli, ili kwamba wawe tayari kuifanya kazi ya Bwana.
12 Walawi wataweka mikono yao juu ya hao fahari. Mtatoa fahari mmoja kuwa sadaka ya dhambi na fahari mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa kwangu, ili kuwa upatanisho kwa Walawi.
“Baada ya Walawi kuweka mikono yao juu ya vichwa vya hao mafahali wawili, tumia mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi kwa Bwana, na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Walawi.
13 Walete Walawi mbele ya Haruni na mbele ya wana wake, uwainue kuwa sadaka ya kutikiswa kwa ajili yangu.
Waambie hao Walawi wasimame mbele ya Aroni na wanawe, kisha wawatoe kama sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana.
14 Kwa njia hii utawatenganisha Walawi toka wana wa Israeli. Walawi watakuwa wangu.
Kwa njia hii utakuwa umewatenga Walawi kutoka kwa Waisraeli wengine, nao Walawi watakuwa wangu.
15 Baadaye Walawi wataingia ndani ya hema ya kukutania. Utawatakasa. utawatoa kuwa sadaka ya kutikiswa
“Utakapokuwa umekwisha kuwatakasa Walawi na kuwatoa kama sadaka ya kuinuliwa, watakuja kufanya kazi yao katika Hema la Kukutania.
16 Fanya hivi kwa sababu wao ni wangu wote kutoka kwa wana wa Israeli. Watachukua nafasi ya kila mzaliwa wa kwanza afunguaye tumbo, mzaliwa wa kwanza wa uzao wa Israeli. Nimewachukua Walawi kwa ajili yangu.
Wao ndio Waisraeli ambao watatolewa kabisa kwangu. Nimewatwaa kama mali yangu mwenyewe badala ya mzaliwa wa kwanza, mzaliwa wa kwanza wa kiume kutoka kwa kila mwanamke wa Kiisraeli.
17 Wazaliwa wa kwanza wote kutoka kwa wana wa Israeli ni wangu, watu wote pamoja na wanyama pia. Siku ile nilipowachukua wazaliwa wa kwanza katika nchi ya Misri, Niliwatenga kwa ajili yangu
Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume katika Israeli, awe wa mwanadamu au mnyama, ni wangu. Wakati nilipowaua wazaliwa wote wa kwanza huko Misri, niliwatenga kwa ajili yangu mwenyewe.
18 Nimewachukua Walawi kutoka kwa wana wa Israeli badala ya wazaliwa wa kwanza.
Nami nimewatwaa Walawi badala ya wazaliwa wote wa kwanza wa kiume katika Israeli.
19 Nimewatoa Walawi kuwa zawadi kwa Haruni na wana wake. Nimewachukua toka wana wa Isreali ili kuwatumikia wana wa Israeli katika hema ya kukutania. Nimewatoa ili kuwa upatanisho kwa watu ili kwamba wasipatwe na mapigo wakati wanapokaribia kwenye eneo takatifu.
Kati ya Waisraeli wote, nimempa Aroni na wanawe Walawi kama zawadi ili wafanye kazi katika Hema la Kukutania kwa niaba ya Waisraeli, na kufanya upatanisho kwa ajili yao ili pasiwepo na pigo lolote litakalowapata Waisraeli wakati watakapokaribia mahali patakatifu.”
20 Musa, Haruni na jamii ya Waisraeli wote waliwafanyia Walawi hivi. Walifanya kila kitu ambacho BWANA alikuwa amemwamuru Musa kuhusu Walawi. Wana wa Israeli wakafanya haya pamoja nao.
Mose, Aroni na jumuiya yote ya Waisraeli wakawafanyia Walawi kama Bwana alivyomwamuru Mose.
21 Walawi wakajitakasa wenyewe na kufua mavazi yao, Na Haruni akawatoa kama sadaka ya kutikiswa kwa BWANA na akafanya upatanisho kwao ili kuwatakasa.
Walawi wakajitakasa wenyewe na wakafua nguo zao. Kisha Aroni akawasogeza mbele za Bwana kuwa sadaka ya kuinuliwa, na kufanya upatanisho kwa ajili yao ili kuwatakasa.
22 Baada ya hayo, Walawi waliingia ndani kufanya utumishi wao katika hema ya kukutania mbele ya Haruni na mbele ya wanawe. Kama BWANA alivyokuwa amemwagiza Musa juu ya Walawi. Waliwahudumia Walawi wote kwa jinsi hii.
Baada ya hayo, Walawi walikuja kufanya kazi yao katika Hema la Kukutania chini ya usimamizi wa Aroni na wanawe. Waliwafanyia Walawi kama vile Bwana alivyomwamuru Mose.
23 BWANA akanena na Musa tena, Akasema,
Bwana akamwambia Mose,
24 “Haya yote ni kwa ajili ya Walawi ambao wana umri wa miaka ishirini na mitano na zaidi. Wataungana na wale wanaohudumia hekaluni.
“Hili linawahusu Walawi: Wanaume wenye umri wa miaka ishirini na mitano au zaidi watakuja kushiriki katika kazi kwenye Hema la Kukutania,
25 Wataacha kutoa huduma hii watakapokuwa na umri wa miaka hamsini. Katika umri huu hawatakiwi kuendelea na huduma tena.
lakini watakapofika umri wa miaka hamsini, ni lazima waache kazi zao za kawaida wala wasiendelee.
26 Wanaweza kuwasaidia ndugu zao wanaoendelea kufanya kazi ndani ya hema ya kukutania, lakini hawatakiwai kufanya kazi tena. Utawaelekeza Walawi kuyafahamu haya yote.”
Wanaweza kuwasaidia ndugu zao kufanya wajibu wao katika Hema la Kukutania, lakini wao wenyewe kamwe hawatafanya hiyo kazi. Basi, hivi ndivyo utakavyogawa wajibu kwa Walawi.”

< Hesabu 8 >