< Nehemia 8 >

1 Watu wote walikusanyika kama mtu mmoja katika eneo la wazi mbele ya lango la maji. Wakamwomba Ezra mwandishi akilete Kitabu cha Sheria ya Musa, ambacho Bwana aliwaamuru Israeli.
watu wote wakakusanyika kama mtu mmoja kwenye uwanja mbele ya Lango la Maji. Wakamwambia Ezra mwandishi alete Kitabu cha Sheria ya Mose, ambacho Bwana aliamuru kwa ajili ya Israeli.
2 Siku ya kwanza ya mwezi wa saba, Ezra, kuhani, akaleta sheria mbele ya mkutano, wanaume na wanawake, na wote waliokuwa na uwezo wa kusikia na kuelewa.
Basi katika siku ya kwanza ya mwezi wa saba, kuhani Ezra akaleta Sheria mbele ya kusanyiko, ambamo walikuwamo wanaume, wanawake na watu wote walioweza kufahamu.
3 Akatizama eneo lililo wazi mbele ya lango la Maji, na akasoma toka asubuhi hadi adhuhuri, mbele ya wanaume na wanawake, na yeyote ambaye angeweza kuelewa. Na wote wakasikiliza kwa makini kitabu cha Sheria.
Akaisoma kwa sauti kubwa tangu mapambazuko mpaka adhuhuri, akiwa ameuelekea uwanja uliokuwa mbele ya Lango la Maji mbele ya wanaume, wanawake na wengine ambao waliweza kufahamu. Watu wote wakasikiliza kwa makini kile Kitabu cha Sheria.
4 Na Ezra, mwandishi, alisimama juu ya jukwaa la mbao ambalo watu walikuwa wametengeneza kwa kusudi hilo. Pembeni yake walisimama Matithia, Shema, Anaya, Uria, Hilkia na Maaseya, upande wake wa kuume; na Pedaya, Misbaeli, Malkiya, Hashumu, Hashbadani, Zekaria na Meshulamu walikuwa wamesimama upande wake wa kushoto.
Mwandishi Ezra alikuwa amesimama juu ya jukwaa la miti lililojengwa kwa kusudi hilo. Karibu naye upande wa kuume alisimama Matithia, Shema, Anaya, Uria, Hilkia na Maaseya. Upande wake wa kushoto walikuwepo Pedaya, Mishaeli, Malkiya, Hashumu, Hashbadani, Zekaria na Meshulamu.
5 Ezra alifungua kitabu mbele ya watu wote, kwa kuwa alikuwa amesimama juu ya watu, na alipoufungua watu wote wakasimama.
Ezra akakifungua kile kitabu. Watu wote waliweza kumwona kwa sababu alikuwa amesimama juu zaidi, naye alipokifungua watu wote wakasimama.
6 Ezra akamshukuru Bwana, Mungu mkuu; na watu wote wakainua mikono yao, wakajibu, “Amina! Amina!” Wakainamisha vichwa vyao, wakamwabudu Bwana kwa nyuso zao zikiwa chini.
Ezra akamsifu Bwana, Mungu mkuu, nao watu wote wakainua mikono yao na kuitikia, “Amen! Amen!” Kisha wakasujudu na kumwabudu Bwana hali nyuso zao zikigusa ardhi.
7 Yeshua, Bani, Sherebia, Yamini, Akubu, Shabethai, Hodai, Maaseya, Kelita, Azaria, Yozabidi, Hanania, Pelaya nao ni Walawi, waliwasaidia watu kuelewa sheria, watu wakakaa mahali pao.
Watu wakiwa wamesimama pale, Walawi wafuatao waliwafunza ile Sheria: Yeshua, Bani, Sherebia, Yamini, Akubu, Shabethai, Hodia, Maaseya, Kelita, Azaria, Yozabadi, Hanani na Pelaya.
8 Wao walisoma katika kitabu, Sheria ya Mungu, wakaeleza wazi kwa tafsiri na kutoa maana ili watu waelewe yaliyosomwa.
Walisoma kutoka kile Kitabu cha Sheria ya Mungu, wakiifafanua na kuwapa maelezo ili watu waweze kufahamu kile kilichokuwa kikisomwa.
9 Nehemia, gavana, na Ezra kuhani, na mwandishi, na Walawi waliokuwa wakitafsiri kwa watu, wakawaambia watu wote, Siku hii ni takatifu kwa Bwana, Mungu wenu. Msiomboleze au kulia. Kwa kuwa watu wote walilia wakati waliposikia maneno ya sheria.
Ndipo Nehemia aliyekuwa mtawala, Ezra kuhani na mwandishi, pamoja na Walawi waliokuwa wakiwafundisha watu wakawaambia wote, “Siku hii ni takatifu kwa Bwana Mungu wenu. Msiomboleze wala msilie.” Kwa kuwa watu wote walikuwa wakilia walipokuwa wakisikiliza maneno ya ile Sheria.
10 Nehemia akawaambia, 'Nendeni, mle kilichonona, mkate na maji ya kunywa, na mpelekeni mtu asiye na kitu, kwa maana siku hii ni takatifu kwa Bwana wetu. Msiwe na huzuni, kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu.
Nehemia akasema, “Nendeni mkafurahie chakula kizuri na vinywaji vitamu, na mpeleke sehemu kwa wale ambao hawana chochote cha kula. Siku hii ni takatifu kwa Bwana. Msihuzunike, kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu.”
11 Basi Walawi wakawafanya watu kuwa na utulivu, wakisema, “Nyamazeni! kwa maana siku hii ni takatifu. Msiwe na huzuni.”
Walawi wakawatuliza watu wote wakisema, “Kuweni watulivu, kwa kuwa hii ni siku takatifu. Msihuzunike.”
12 Watu wote wakaenda kula na kunywa na kugawana chakula na kusherehekea kwa furaha kubwa kwa sababu walielewa maneno waliyohubiriwa.
Kisha watu wote wakaondoka kwenda kula na kunywa, na kupeana sehemu ya chakula, na wakaadhimisha kwa furaha kubwa, kwa sababu sasa walifahamu maneno yale waliyokuwa wameelezwa.
13 Siku ya pili viongozi wa nyumba za mababu kutoka kwa watu wote, makuhani na Walawi, wakakusanyika kwa Ezra, mwandishi ili kupata ufahamu kutoka kwenye maneno ya sheria.
Katika siku ya pili ya mwezi, wakuu wa mbari zote, pamoja na makuhani na Walawi, walikusanyika wakimzunguka Ezra mwandishi ili wapate kusikiliza kwa makini maneno ya Sheria.
14 Wakaona imeandikwa katika sheria namna Bwana alivyomuamuru Musa kwamba wana wa Israeli waishi katika hema wakati wa sikukuu ya mwezi wa saba.
Wakakuta imeandikwa katika ile Sheria, ambayo Bwana aliiamuru kupitia kwa Mose, kwamba Waisraeli walipaswa kukaa katika vibanda wakati wa sikukuu ya mwezi wa saba,
15 Wanapaswa kutoa tamko katika miji yao yote, na huko Yerusalemu, wakisema, 'Nendeni nje kwenye nchi ya vilima, na mkalete matawi kutoka kwenye mzeituni mwitu, na matawi ya mihadsi, na matawi ya mitende na matawi ya miti minene ili kufanya vibanda vya muda kama ilivyoandikwa.”
na kwamba walipaswa kutangaza neno hili na kulieneza katika miji yao na katika Yerusalemu wakisema: “Enendeni katika nchi ya mlima na kuleta matawi kutoka miti ya mizeituni, mizeituni mwitu, mihadasi, mitende na miti ya kivuli, ili kutengeneza vibanda,” kama ilivyoandikwa.
16 Basi watu wakatoka na kuleta matawi, wakajifanyia mahema, kila mmoja juu ya paa zao, katika ua zao, katika mahakama za nyumba ya Mungu, mahali pa wazi pa lango la Maji, na katika mraba wa lango la Efraimu.
Basi watu wakaenda na kuleta matawi, nao wakajijengea vibanda juu ya paa za nyumba zao, katika nyua zao, katika nyua za nyumba ya Mungu, na katika uwanja karibu na Lango la Maji na uwanja wa Lango la Efraimu.
17 Kisha kusanyiko lote la wale waliorudi kutoka kifungoni wakafanya mahema na kukaa ndani yake. Kwa kuwa tangu siku za Yoshua, mwana wa Nuni hata siku hiyo, watu wa Israeli hawakuadhimisha sikukuu hii. Na furaha ilikuwa kubwa sana.
Jamii yote ya watu waliorudi kutoka utumwani wakajenga vibanda na kuishi ndani yake. Tangu wakati wa Yoshua mwana wa Nuni mpaka siku ile, Waisraeli hawakuwahi kuiadhimisha namna hii. Furaha yao ilikuwa kubwa sana.
18 Pia siku kwa siku, tangu siku ya kwanza hadi mwisho, Ezra alisoma kutoka Kitabu cha Sheria ya Mungu. Walifanya sikukuu kwa siku saba na siku ya nane kilikuwa na kusanyiko zuri, kwa utiifu wa amri.
Siku baada ya siku, kuanzia siku ya kwanza hadi ya mwisho, Ezra alisoma kutoka kwenye kile Kitabu cha Sheria ya Mungu. Wakaiadhimisha sikukuu ile kwa siku saba, nayo siku ya nane, kufuatana na maagizo, kulikuwa na kusanyiko maalum.

< Nehemia 8 >