< Nehemia 5 >
1 Kisha wale wanaume na wake zao wakalia kwa nguvu dhidi ya Wayahudi wenzao.
Wakati huu wanaume na wake zao wakalia kilio kikuu dhidi ya ndugu zao Wayahudi.
2 Kwa maana kulikuwa na baadhi ya watu ambao walisema, “Sisi na wana wetu na binti zetu tupo wengi. Basi hebu tupate nafaka tuweze kula na tukae tuishi.”
Baadhi yao walikuwa wakisema, “Sisi na wana wetu na binti zetu tuko wengi. Ili tuweze kula na kuishi, ni lazima tupate nafaka.”
3 Pia kulikuwa na baadhi ya watu ambao walisema, “Tunaweka rehani mashamba yetu, mizabibu yetu, na nyumba zetu ili tupate nafaka wakati wa njaa.”
Wengine walikuwa wakisema, “Tunaweka rehani mashamba yetu, mashamba ya mizabibu, na nyumba zetu ili tupate nafaka wakati wa njaa.”
4 Wengine pia walisema, “Tumekopesha pesa kulipa kodi ya mfalme kwenye mashamba yetu na mashamba yetu ya mizabibu.
Bado kukawa na wengine waliokuwa wakisema, “Ilitubidi tukope fedha ili kulipa kodi ya mfalme kwa ajili ya mashamba yetu na mashamba yetu ya mizabibu.
5 Hata hivyo sasa miili yetu na damu ni sawa na ndugu zetu, na watoto wetu ni sawa na watoto wao. Tunalazimishwa kuuza wana wetu na binti zetu kuwa watumwa. Baadhi ya binti zetu tayari wamekuwa watumwa. Lakini hatuna nguvu za kusaidia kwa sababu watu wengine sasa wana mashamba yetu na mizabibu yetu.”
Ingawa sisi ni mwili na damu moja sawa na watu wa nchi yetu, na ijapo wana wetu ni wazuri kama wana wao, bado inatupasa kuwatoa wana wetu na binti zetu kwenye utumwa. Baadhi ya binti zetu wameshakuwa watumwa tayari, lakini hatuna uwezo wa kuwakomboa, kwa sababu mashamba yetu na mashamba ya mizabibu yetu ni mali ya wengine.”
6 Nilikasirika sana niliposikia kilio chao na maneno haya.
Niliposikia kilio chao na malalamiko haya, nilikasirika sana.
7 Kisha nikafikiri juu ya hili, na kuleta mashtaka dhidi ya wakuu na viongozi. Nikawaambia, “Ninyi mnatafuta riba, kila mmoja kutoka kwa ndugu yake mwenyewe.” Nikakutanisha kusanyiko kubwa juu yao
Nikayatafakari katika akili yangu, nikiwalaumu wakuu na maafisa. Nikawaambia, “Mnawaonea ndugu zenu kwa kuwatoza riba!” Basi nikaitisha mkutano mkubwa ili kuwashughulikia
8 na kuwaambia, “Sisi, kwa kadiri tulivyoweza, tumewakomboa toka utumwani ndugu zetu wa Kiyahudi ambao walikuwa wameuzwa kwa mataifa, lakini hata mnawauza ndugu na dada zenu ili wauzwe tena kwetu!” Walikuwa kimya na hawakupata neno la kusema.
na kusema: “Kulingana na uwezo wetu, tumewakomboa ndugu zetu Wayahudi waliokuwa wameuzwa kwa watu wasioamini. Sasa mnawauza ndugu zenu, ili wauzwe tena kwetu!” Walinyamaza kimya, kwa sababu hawakupata chochote cha kusema.
9 Pia nikasema, 'Mnachokifanya sio kizuri. Je, hampaswi kutembea katika hofu ya Mungu wetu ili kuzuia malalamiko ya mataifa ambayo ni adui zetu?
Basi nikaendelea kusema, “Mnachokifanya si sawa. Je, haikuwapasa kutembea katika hofu ya Mungu wetu ili tuepukane na shutuma za adui zetu wasioamini?
10 Mimi na ndugu zangu na watumishi wangu tunawapa fedha na nafaka. Lakini lazima tuache kutoza riba juu ya mikopo hii.
Mimi na ndugu zangu na watu wangu tunawakopesha watu fedha na nafaka. Lakini jambo hili la kutoza riba likome!
11 Warudishieni leo leo mashamba yao, mizabibu yao, mashamba yao ya mizeituni, na nyumba zao na asilimia ya fedha, nafaka, divai mpya, na mafuta mliyowatoza.”
Warudishieni mara moja mashamba yao, mashamba yao ya mizabibu, mashamba yao ya mizeituni, na nyumba zao, pia riba yao mnayowatoza na sehemu ya fungu la mia la fedha, nafaka, divai mpya na mafuta.”
12 Wakasema, “Tutarudisha kile tulichochukua kutoka kwao, wala hatutahitaji kitu kutoka kwao. Tutafanya kama unavyosema.” Ndipo nikawaita makuhani, na kuwaapisha kuwafanya kama walivyoahidi.
Wakasema, “Tutawarudishia na hatutataka kitu chochote zaidi kutoka kwao. Tutafanya kama ulivyosema.” Kisha nikawaita makuhani na kuwafanya wakuu na maafisa kuapa kufanya kile walichoahidi.
13 Nikakung'uta vazi langu, nikasema, “Basi Mungu aondoe nyumba na mali ya kila mtu asiyetimiza ahadi yake. Kwa hiyo akung'utwe na kuwa hana kitu. Kusanyiko lote likasema “Amina,” na wakamsifu Bwana. Na watu wakafanya kama walivyoahidi.
Pia nikakungʼuta makunjo ya vazi langu na kusema, “Kila mtu ambaye hatatimiza ahadi hii, Mungu na amkungʼute hivi kutoka nyumba yake na katika mali zake. Basi mtu wa namna hiyo akungʼutiwe nje na aachwe bila kitu!” Waliposikia hili, mkutano wote ukasema, “Amen,” na wakamtukuza Bwana. Nao watu wakafanya kama walivyokuwa wameahidi.
14 Kwa hiyo tangu wakati niliowekwa kuwa mkuu wao katika nchi ya Yuda, tangu mwaka wa ishirini mpaka mwaka wa thelathini na pili wa mfalme Artashasta, miaka kumi na miwili, mimi na ndugu zangu hatukula chakula kilichotolewa kwa gavana.
Zaidi ya hayo, kutoka mwaka wa ishirini wa Mfalme Artashasta, wakati nilipoteuliwa kuwa mtawala wao katika nchi ya Yuda, mpaka mwaka wake wa thelathini na mbili, yaani miaka kumi na miwili, mimi wala ndugu zangu hatukula chakula ambacho kwa kawaida hupewa watawala.
15 Lakini wakuu wa zamani waliokuwa kabla yangu waliwaweka watu mizigo mizito, na wakachukua kwao shekeli arobaini za fedha kwa ajili ya chakula na divai yao ya kila siku. Hata watumishi wao waliwadhulumu watu. Lakini sikufanya hivyo kwa sababu ya hofu ya Mungu.
Lakini watawala wa mwanzoni, wale walionitangulia, waliwalemea watu na kuchukua kutoka kwao shekeli arobaini za fedha, pamoja na chakula na mvinyo. Wasaidizi wao pia walijifanya wakuu juu ya watu. Lakini kwa kumheshimu Mungu sikufanya hivyo.
16 Niliendelea kufanya kazi kwenye ukuta, na hatukununua ardhi. Na watumishi wangu wote walikusanyika huko kwa ajili ya kazi hiyo.
Badala yake, nilijitoa kwa bidii katika kazi ya ukuta huu. Watu wangu wote walikutanika pale kwa ajili ya kazi. Hatukujipatia shamba lolote.
17 Katika meza yangu walikuwa Wayahudi na maafisa, watu 150, isipokuwa wale waliokuja kwetu kutoka kwa mataifa waliokuwa wakituzunguka.
Zaidi ya hayo, Wayahudi na maafisa 150 walikula mezani pangu, pamoja na wale waliotujia kutoka mataifa jirani.
18 Kila kitu kilichoandaliwa kila siku kilikuwa ng'ombe moja, kondoo sita waliochaguliwa, na ndege, na kila siku kumi aina zote za divai nyingi. Na hata kwa haya yote sikuhitaji mahitaji ya chakula cha gavana, kwa sababu madai yalikuwa mazito sana juu ya watu.
Kila siku niliandaliwa maksai mmoja, kondoo sita wazuri, na kuku, na mvinyo wa kila aina kwa wingi kila baada ya siku kumi. Licha ya mambo haya yote, sikudai chakula kilichokuwa fungu la mtawala, kwa sababu madai yalikuwa mazito sana kwa watu hawa.
19 Nikumbuke, Ee Mungu wangu, kwa wema, kwa sababu ya yote niliyoyafanya kwa watu hawa.
Unikumbuke kwa fadhili, Ee Mungu wangu, kwa yote niliyofanya kwa ajili ya watu hawa.