< Nehemia 4 >
1 Sanbalati alipoposikia tulikuwa tukijenga ukuta, akaghadhabika ndani yake, naye akakasirika sana, akawacheka Wayahudi.
2 Mbele ya ndugu zake na jeshi la Samaria, akasema, “Wayahudi dhaifu hawa wanafanya nini? Je, watajifanyia mji wenyewe? Je, watatoa dhabihu? Je, wataimaliza kazi siku moja? Je! Watawaletea mawe kutoka kwenye kifusi baada ya kuchomwa moto?
3 Tobia Mwamoni alikuwa pamoja naye, naye akasema, 'Ikiwa tu mbweha angepanda juu ya hichi wanachokijenga, angeubomoa ukuta huo wa mawe.”
4 Tusikilize, Mungu wetu, kwa maana sisi tunatukanwa. Rudisha malalamiko yao juu ya vichwa vyao wenyewe na kuwapa wapate kutekwa katika nchi ambapo wao ni wafungwa.
5 Usiufunike uovu wao, wala usiondoe dhambi zao mbele yako; kwa sababu wamewachukiza wanaojenga.
6 Kwa hiyo tulijenga ukuta na ukuta wote uliunganishwa kwa nusu ya urefu wake, kwa kuwa watu walikuwa na hamu ya kufanya kazi
7 Lakini Sanbalati, Tobia, Waarabu, Waamoni, na Waashdodi waliposikia kwamba kazi ya ukarabati wa kuta za Yerusalemu ilikuwa ikiendelea, na kwamba sehemu zilizovunjika katika ukuta zilikuwa zimefungwa, ghadhabu kubwa ikawaka ndani yao.
8 Wote walifanya shauri pamoja, na walikuja kupigana dhidi ya Yerusalemu na kusababisha machafuko ndani yake.
9 Lakini tuliomba kwa Mungu wetu na kuweka walinzi kama ulinzi dhidi yao mchana na usiku kwa sababu ya tishio lao.
10 Kisha watu wa Yuda wakasema, “Nguvu ya wale wanaobeba mizigo inashindwa. Kuna kifusi kikubwa, na hatuwezi kujenga ukuta.”
11 Na adui zetu wakasema,” Wala hawatajua au kuona mpaka tutakapokuja kati yao na kuwaua, na kuisimamisha kazi.”
12 Wakati huo Wayahudi waliokuwa wakiishi karibu nao walitoka pande zote na kuzungumza nasi mara kumi, wakituonya juu ya mipango waliyofanya dhidi yetu.
13 Kwa hiyo nikaweka watu katika sehemu za chini za ukuta katika sehemu zilizo wazi. Niliweka kila familia wenye upanga, mikuki, na upinde.
14 Nikatazama, nikasimama, nikawaambia wakuu, na watawala, na watu wengine, “Msiogope. mkumbukeni Bwana, ambaye ni mkuu na wa kushangaza. Wapiganie ndugu zenu, wana zenu, binti zenu, wake zenu na nyumba zenu.
15 Ilipokuwa wakati adui zetu waliposikia kwamba mipango yao ilikuwa inayojulikana kwetu, na Mungu alikuwa amebatilisha mipango yao, sote tulirudi ukutani, kila mmoja kwa kazi yake.
16 Kwa hiyo tangu wakati huo nusu ya watumishi wangu walifanya kazi tu juu ya kujenga ukuta, na nusu yao wakaishika mikuki, ngao, pinde, na kuvaa silaha, wakati viongozi walisimama nyuma ya watu wote wa Yuda.
17 Na hivyo wafanyakazi haohao ambao walikuwa wakijenga ukuta na kubeba mizigo walikuwa pia wakilinda nafasi zao. Kila mtu alifanya kazi kwa mkono mmoja, na kwa mkono mwingine alikuwa na silaha yake.
18 Kila mjenzi alivaa upanga wake ubavuni mwake na ndivyo alivyojenga. Yule aliyepiga tarumbeta akakaa karibu nami.
19 Niliwaambia wakuu na viongozi na watu wengine, “Kazi ni nzuri na ya kina, na tumejitenga kwenye ukuta, mbali na mtu mwingine.
20 Lazima mkimbilie mahali ambapo mtasikia sauti ya tarumbeta na kusanyika huko. Mungu wetu atatupigania.”
21 Kwa hiyo tulifanya kazi hiyo. Nusu yao walikuwa wakichukua mikuki kutoka kupambazuka asubuhi hadi kutokea kwa nyota.
22 Nikawaambia watu wakati huo, “Kila mtu na mtumishi wake waende usiku katikati ya Yerusalemu, ili wawe walinzi wakati wa usiku na mfanyakazi wakati huo.”
23 Basi si mimi, wala ndugu zangu, wala watumishi wangu, wala watu wa walinzi waliokuwa wananifuata, hakuna hata mmoja wetu aliyebadili nguo zake, na kila mmoja wetu alichukua silaha yake, hata kama angeenda kwa ajili ya kuteka maji.