< Nehemia 1 >
1 Maneno ya Nehemia mwana wa Hakalia Ikawa, katika mwezi wa Kisleu, katika mwaka wa ishirini, nilikuwa katika mji mkuu wa Sushani,
Maneno ya Nehemia mwana wa Hakalia: Katika mwezi wa Kisleu katika mwaka wa ishirini, wakati nilikuwa ngomeni katika jumba la kifalme la Shushani,
2 mmoja wa ndugu zangu, Hanani, alikuja pamoja na watu wengine kutoka Yuda, nami nikawauliza kuhusu Wayahudi waliopona, Wayahudi waliosalia waliokuwa huko, na kuhusu Yerusalemu.
Hanani, mmoja wa ndugu zangu, alikuja kutoka Yuda akiwa na watu wengine, nami nikawauliza kuhusu mabaki ya Wayahudi wale walionusurika kwenda uhamishoni na pia kuhusu Yerusalemu.
3 Wakaniambia, “Wale waliokuwa katika mkoa ule waliookoka katika kifungo wapo katika shida kubwa na aibu kwa sababu ukuta wa Yerusalemu umebomolewa na milango yake imeteketezwa kwa moto.”
Wakaniambia, “Wale walionusurika kwenda uhamishoni, wale ambao wamerudi kwenye lile jimbo, wako katika taabu kubwa na aibu. Ukuta wa Yerusalemu umebomoka, na malango yake yamechomwa moto.”
4 Na mara tu niliposikia maneno haya, nikakaa na kulia, na kwa siku niliendelea kuomboleza na kufunga na kuomba mbele ya Mungu wa mbinguni.
Niliposikia mambo haya, niliketi, nikalia. Kwa siku kadhaa niliomboleza na kufunga na kuomba mbele za Mungu wa mbinguni.
5 Ndipo nikasema, “Wewe ndiwe Bwana, Mungu wa mbinguni, Mungu uliye mkuu na kushangaza, unayetimiza agano na upendo wa kudumu pamoja na wale wanaokupenda na kushika amri zake.
Kisha nikasema: “Ee Bwana, Mungu wa mbinguni, mkuu na mwenye kuogofya, ambaye hulishika agano lake la upendo na wale wampendao na kutii amri zake,
6 Sikiliza maombi yangu na fungua macho yako, ili uisikie sala ya mtumishi wako kwamba sasa nasali mbele yako mchana na usiku kwa ajili ya watu wa Israeli watumishi wako. Mimi ninakiri dhambi za watu wa Israeli, ambazo tumefanya dhidi yako. Wote mimi na nyumba ya baba yangu tumefanya dhambi.
tega masikio yako, na ufungue macho yako, ili usikie maombi ya mtumishi wako anayoomba mbele yako usiku na mchana kwa ajili ya watumishi wako, watu wa Israeli. Ninaungama dhambi zetu sisi Waisraeli, pamoja na zangu na za nyumba ya baba yangu, tulizotenda dhidi yako.
7 Tumefanya uovu sana juu yako, na hatukuzingatia amri, sheria, na hukumu ambazo ulimwamuru mtumishi wako Musa.
Tumetenda uovu sana mbele zako. Hatukutii amri, maagizo na sheria ulizompa Mose mtumishi wako.
8 Tafadhali kumbuka neno ulilomuamuru mtumishi wako Musa, 'mkitenda pasipo uaminifu, nitawatawanya kati ya mataifa,
“Kumbuka agizo ulilompa Mose mtumishi wako, ukisema, ‘Kama mkikosa uaminifu, nitawatawanya miongoni mwa mataifa,
9 lakini mkirudi kwangu na kufuata amri zangu na kuzifanya, ingawa watu wako walienea chini ya mbingu za mbali, Nami nitawakusanya kutoka huko na kuwaleta mahali pale nilipopachagua ili kulifanya jina langu.'
lakini mkinirudia na kutii amri zangu, ndipo hata kama watu wenu walio uhamishoni wako mbali sana katika miisho ya dunia, nitawakusanya kutoka huko na kuwaleta mahali ambapo nimepachagua kuwa makao kwa ajili ya Jina langu.’
10 Sasa wao ni watumishi wako na watu wako, ambao uliwaokoa kwa nguvu yako kubwa na kwa mkono wako wenye nguvu.
“Hawa ni watumishi wako na watu wako, uliowakomboa kwa nguvu zako kuu na mkono wako wenye nguvu.
11 Bwana, naomba, sikiliza sasa maombi ya watumishi wako na sala ya watumishi wako ambao hufurahia kuheshimu jina lako. Sasa unifanikishe mimi mtumishi wako leo, na unijalie rehema mbele ya mtu huyu.” Nilikuwa mnyweshaji wa mfalme.
Ee Bwana, tega sikio lako na usikie maombi ya huyu mtumishi wako, na maombi ya watumishi wako wanaofurahia kuliheshimu Jina lako. Nipe leo, mimi mtumishi wako, mafanikio kwa kunipa kibali mbele ya mtu huyu.” Kwa maana nilikuwa mnyweshaji wa mfalme.