< Mathayo 5 >
1 Yesu alipo uona umati, akaondoka na kuelekea Mlimani. Alipokuwa ameketi chini, wanafunzi wake wakaja kwake.
2 Akafunua kinywa chake na akawafundisha, akisema,
3 “Heri walio maskini wa roho maana ufalme wa mbinguni ni wao.
4 Heri walio na huzuni, maana watafarijiwa.
5 Heri wenye upole, maana watairithi nchi.
6 Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watashibishwa.
7 Heri wenye rehema maana hao watapata Rehema.
8 Heri wenye moyo safi maana watamwona Mungu.
9 Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu.
10 Heri wale wanaoteswa kwa ajili ya haki, maana ufalme wa mbinguni ni wao.
11 Heri ninyi ambao watu watawatukana na kuwatesa, au kusema kila aina ya ubaya dhidi yenu kwa uongo kwa ajili yangu.
12 Furahini na kushangilia, maana thawabu yenu ni kubwa juu mbinguni. Kwa kuwa hivi ndivyo watu walivyo watesa manabii walioishi kabla yenu.
13 Ninyi ni chumvi ya dunia. Lakini kama chumvi imepoteza ladha yake, itawezaje kufanyika chumvi halisi tena? Kamwe haiwezi kuwa nzuri kwa kitu kingine chochote tena, isipokuwa ni kutupwa nje na kukanyagwa na miguu ya watu.
14 Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojegwa juu ya mlima haufichiki.
15 Wala watu hawawashi taa na kuweka chini ya kikapu, bali kwenye kinara, nayo yawaangaza wote walio ndani ya nyumba.
16 Acha nuru yenu iangaze mbele za watu kwa namna ambayo kwamba, wayaone matendo yenu mema na kumtukuza Baba yenu aliye mbinguni.
17 Msifikiri nimekuja kuiharibu sheria wala manabii. Sijaja kuharibu lakini kutimiza.
18 Kwa kweli nawaambia kwamba mpaka mbingu na dunia zote zipite hapana yodi moja wala nukta moja ya sheria itaondoshwa katika sheria hadi hapo kila kitu kitakapokuwa kimekwisha timizwa.
19 Hivyo yeyote avunjaye amri ndogo mojawapo ya amri hizi na kuwafundisha wengine kufanya hivyo ataitwa mdogo katika ufalme wa mbinguni. Lakini yeyote azishikaye na kuzifundisha ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.
20 Kwa maana nawaambia haki yenu isipozidi haki ya waandishi na Mafarisayo, kwa vyovyote vile hamtaingia katika ufalme wa mbinguni.
21 Mmesikia ilinenwa zamani kuwa, “usiue” na 'yeyote auaye yuko katika hatari ya hukumu.'
22 Lakini nawaambia yeyote amchukiaye ndugu yake atakuwa katika hatari ya hukumu. Na yeyote amwambiaye ndugu yake kuwa, 'Wewe ni mtu usiyefaa!' atakuwa katika hatari ya baraza. Na yeyote asemaye, 'Wewe mjinga!' atakuwa katika hatari ya moto wa jehanamu. (Geenna )
23 Hivyo kama unatoa sadaka yako katika madhabahu na unakumbuka kuwa ndugu yako ana jambo lolote dhidi yako,
24 iache sadaka mbele ya madhabahu, kisha shika njia yako. Kapatane kwanza na ndugu yako, na kisha uje kuitoa sadaka yako.
25 Patana na mshitaki wako upesi, ukiwa pamoja naye njiani kuelekea mahakamani, vinginevyo mshtaki wako anaweza kukuacha mikononi mwa hakimu, na hakimu akuache mikononi mwa askari, nawe utatupwa gerezani.
26 Amini nawaambieni, kamwe hutawekwa huru hadi umelipa senti ya mwisho ya pesa unayodaiwa.
27 Mmesikia imenenwa kuwa, 'Usizini.'
28 Lakini nawaambieni yeyote amtazamaye mwanamke kwa kumtamani amekwisha kuzini naye moyoni mwake.
29 Na kama jicho lako la kulia linakusababisha kujikwaa, ling'oe na ulitupe mbali nawe. Kwa kuwa ni afadhali kiungo kimoja katika mwili wako kiharibike kuliko mwili mzima kutupwa jehanamu. (Geenna )
30 Na kama mkono wako wa kuume unakusababisha kujikwaa, ukate kisha uutupilie mbali nawe. Maana ni afadhali kiungo kimoja katika mwili wako kiharibike kuliko mwili mzima kutupwa jehanamu. (Geenna )
31 Imenenwa pia, yeyote amfukuzaye mkewe, na ampe hati ya talaka.'
32 Lakini mimi nawaambia, yeyote anaye mwacha mke wake, isipokuwa kwa kwa sababu ya zinaa, amfanya kuwa mzinzi. Na yeyote amuoaye baada ya kupewa talaka afanya uzinzi.
33 Tena, mmesikia ilinenwa kwa wale wa zamani, 'Msiape kwa uongo, bali pelekeni viapo vyenu kwa Bwana.'
34 Lakini nawaambia, msiape hata kidogo, ama kwa mbingu, kwa sababu ni enzi ya Mungu;
35 wala kwa dunia, maana ni mahali pa kuweka kiti cha kukanyagia nyayo zake, ama kwa Jerusalemu, maana ni mji wa mfalme mkuu.
36 Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi.
37 Bali maneno yenu yawe, 'Ndiyo, ndiyo, Hapana, hapana.' Kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.
38 Mmesikia imenenwa kuwa, 'Jicho kwa jicho, na jino kwa jino.'
39 Lakini mimi namwambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akikupiga shavu la kulia mgeuzie na jingine pia.
40 Na kama yeyote anatamani kwenda na wewe mahakamani na akakunyang'anya kanzu yako, mwachie na joho lako pia.
41 Na yeyote akulazimishaye kwenda naye maili moja, nenda naye maili mbili.
42 Kwa yeyote akuombaye mpatie, na usimwepuke yeyote anayehitaji kukukopa.
43 Mmesikia imenenwa, 'Umpende jirani yako, na umchukie adui yako.'
44 Lakini nawaambia, wapendeni adui zenu, waombeeni wanao waudhi,
45 Ili kwamba muwe watoto wa baba yenu aliye mbinguni. Kwa kuwa anafanya jua liwaangazie wabaya na wema, na anawanyeshea mvua waovu na wema.
46 Kama mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu gani? Kwani watoza ushuru hawafanyi hivyo?
47 Na kama mkiwasalimia ndugu zenu tu mwapata nini zaidi ya wengine? Je!, Watu wa mataifa hawafanyi vivyo hivyo?
48 Kwa hiyo yawapasa kuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.