< Mathayo 4 >
1 Kisha Yesu aliongozwa na Roho mpaka jangwani ili ajaribiwe na ibilisi.
2 Alipokuwa amefunga kwa siku arobaini mchana na usiku alipata njaa.
3 Mjarabu akaja na akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mkate.”
4 Lakini Yesu alimjibu na kumwambia, “Imeandikwa, 'Mtu hataishi kwa mkate peke yake, bali kwa kila neno litokalo kinywani mwa Mungu.'''
5 Kisha ibilisi akampeleka katika mji mtakatifu na kumweka mahali pa juu sana pa jengo la hekalu,
6 na kumwambia,'' kama wewe ni Mwana wa Mungu, jirushe chini, kwa maana imeandikwa, 'Ataamuru malaika wake waje wakudake,' na, 'watakuinua kwa mikono yao, ili usijikwae mguu wako katika jiwe.”
7 Yesu akamwambia, ''Tena imeandikwa, 'Usimjaribu Bwana Mungu wako.'''
8 Kisha, ibilisi akamchukua na kumpeleka sehemu ya juu zaidi akamwonyesha falme zote za ulimwengu na fahari ya hizo zote.
9 Akamwambia, “Nitakupa vitu vyote hivi ukunisujudia na kuniabudu.”
10 Kisha Yesu akamwambia, “Nenda zako utoke hapa, Shetani! Kwa maana imeandikwa, 'Yakupasa kumwabudu Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.'”
11 Kisha ibilisi akamwacha, na tazama, malaika wakaja wakamtumikia.
12 Basi Yesu aliposikia kuwa Yohana amekamatwa, aliondoka mpaka Galilaya.
13 Aliondoka Nazareti alienda na kuishi Kaperanaumu, iliyoko kandokando na Bahari ya Galilaya, mipakani mwa majimbo ya Zabuloni na Naftali.
14 Hii ilitokea kutimiza kile kilichonenwa na nabii Isaya,
15 “Katika mji wa Zabuloni na mji wa Naftali, kuelekea Baharini, ng'ambo ya Yorodani, Galilaya ya wamataifa!
16 Watu walio kaa gizani wameuona mwanga mkuu, na wale waliokuwa wameketi katika maeneo na kivuli cha mauti, juu yao nuru imewaangazia.''
17 Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri na kusema, “Tubuni, kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.''
18 Alipokuwa akitembea kandokando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona ndugu wawili, Simoni aliyekuwa akiitwa Petro, na Andrea kaka yake, wakitega nyavu baharini, kwa kuwa walikuwa wavuvi wa samaki.
19 Yesu akawaambia, “Njooni mnifuate, nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.”
20 Mara moja waliziacha nyavu na walimfuata.
21 Na Yesu alipokuwa akiendelea kutoka hapo aliwaona ndugu wawili wengine, Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana kaka yake. Walikuwa katika mtumbwi pamoja na Zebedayo baba yao wakishona nyavu zao. Akawaita,
22 na mara moja wakaacha mtumbwi na baba yao nao wakamfuata.
23 Yesu alienda karibia Galilaya yote, akifundisha katika Masinagogi yao, akihubiri injili ya ufalme, na akiponya kila aina ya maradhi na magonjwa miongoni mwa watu.
24 Habari zake zilienea Siria yote, na watu wakawaleta kwake wale wote waliokuwa wakiugua, wakiwa na maradhi mbalimbali na maumivu, waliokuwa na mapepo, na wenye kifafa na waliopooza. Yesu aliwaponya.
25 Umati mkubwa wa watu ulimfuata kutoka Galilaya, na Dekapoli, na Yerusalemu na Uyahuda na kutoka ng'ambo ya Yorodani.