< Mathayo 24 >

1 Yesu alitoka hekaluni na kwenda zake. Wanafunzi wake walimwendea na kumuonesha majengo ya hekalu.
Yesu akatoka Hekaluni na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya Hekalu.
2 Laikni aliwajibu na kuwaambia, “Je, hamuyaoni mambo haya yote? Kweli nawaambia, hakuna jiwe litalobaki juu ya lingine bila kubomolewa.”
Ndipo Yesu akawauliza, “Je, mnayaona haya yote? Amin, nawaambia, hakuna hata jiwe moja hapa litakalobaki juu ya jingine, bali kila moja litabomolewa.”
3 Na alipokaa katika Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake walimwendea kwa faragha na kusema, “Tuambie, mambo haya yatatokea lini? Kitu gani kitakuwa dalili ya kuja kwako na mwisho wa ulimwengu?” (aiōn g165)
Yesu alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamjia faraghani, wakamuuliza, “Tuambie, mambo haya yatatukia lini, nayo dalili ya kuja kwako na ya mwisho wa dunia ni gani?” (aiōn g165)
4 Yesu aliwajibu na kuwaambia, “Iweni makini kwamba asije mtu akawapotosha.
Yesu akawajibu, “Jihadharini, mtu yeyote asiwadanganye.
5 Kwa kuwa wengi watakuja kwa jina langu. Watasema, 'Mimi ndiye Kristo', na watawapotosha wengi.
Kwa maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye Kristo,’nao watawadanganya wengi.
6 Mtasikia vita na taarifa za vita. Angalieni msije mkawa na wasiwasi, kwa kuwa mambo haya hayabudi kutokea; lakini ule mwisho utakuwa bado.
Mtasikia habari za vita na matetesi ya vita. Angalieni msitishike, kwa maana haya hayana budi kutukia. Lakini ule mwisho bado.
7 Kwa kuwa taifa litainuka dhidi ya taifa jingine, na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na njaa na matetemeko ya ardhi katika sehemu mbalimbali.
Taifa litainuka dhidi ya taifa, na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali.
8 Lakini mambo haya yote ni mwanzo tu wa uchungu wa kujifungua.
Haya yote yatakuwa ndio mwanzo wa utungu.
9 Ndipo watawatoa kwa ajili ya mateso na kuwaua. Mtachukiwa na mataifa yote kwa sababu ya jina langu.
“Ndipo mtasalitiwa, ili mteswe na kuuawa, nanyi mtachukiwa na mataifa yote kwa ajili yangu.
10 Ndipo wengi watajikwaa na kusalitiana na watachukiana wenyewe kwa wenyewe.
Wakati huo, wengi wataacha imani yao, nao watasalitiana kila mmoja na mwenzake na kuchukiana.
11 Manabii wengi wa uongo watatokea na kuwadanganya wengi.
Watatokea manabii wengi wa uongo, nao watawadanganya watu wengi.
12 Kwa sababu uovu utaongezeka, upendo wa wengi utapoa.
Kwa sababu ya kuongezeka kwa uovu upendo wa watu wengi utapoa,
13 Lakini atakaye vumilia mpaka mwisho, ataokolewa.
lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa.
14 Hii Injili ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu mzima kama ushuhuda kwa mataifa yote. Na ndipo ule mwisho utafika.
Injili ya Ufalme itahubiriwa ulimwenguni kote kuwa ushuhuda kwa mataifa yote. Ndipo mwisho utakapokuja.
15 Kwa hiyo, mtakapoona chukizo la uharibifu, lililosemwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu [asomaye na afahamu],
“Hivyo mtakapoona lile ‘chukizo la uharibifu’ lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu (asomaye na afahamu),
16 ndipo walioko Yuda wakimbilie milimani.
basi wale walioko Uyahudi wakimbilie milimani.
17 Na yule aliyeko juu ya paa la nyumba asiweze kuteremka chini kuchukua kitu chochote kutoka ndani ya nyumba yake,
Yeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke ili kuchukua chochote kutoka ndani ya nyumba.
18 naye aliyeko shambani asirudi kuchukua vazi lake.
Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake.
19 Lakini ole wao ambao wana mtoto na wale ambao wananyonyesha katika siku hizo!
Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo!
20 Ombeni kwamba kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato.
Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi au siku ya Sabato.
21 Kwa kuwa kutakuwa na dhiki kuu, ambayo haijawahi kuwapo tangu kuumbwa kwa ulimwengu hadi sasa, na wala haitakuwapo tena.
Kwa maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa dunia mpaka sasa: wala haitakuwako tena kamwe.
22 Kama siku hizo zisingefupishwa, hakuna ambaye angeokoka. Lakini kwa sababu ya wateule, siku hizo zitafupishwa.
Kama siku hizo zisingefupishwa, hakuna hata mtu mmoja ambaye angeokoka. Lakini kwa ajili ya wateule, siku hizo zitafupizwa.
23 Kisha ikiwa mtu yeyote atawaambia 'Tazama, Kristo yuko hapa! au, 'Kristo yuko kule' msiamini maneno hayo.
Wakati huo kama mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Kristo huyu hapa!’ Au, ‘Kristo yuko kule,’ msisadiki.
24 Kwa kuwa Makristo wa uongo na manabii wa uongo watakuja na kuonesha ishara kubwa na maajabu, kwa kusudi la kupotosha, kama ingewezekana hata na wateule.
Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara kubwa na maajabu mengi ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule hasa.
25 Tazameni, nimewatahadharisha kabla ya mambo hayo kutokea.
Angalieni, nimekwisha kuwaambia mapema.
26 Kwa hiyo, ikiwa watawaambia, ''Kristo yuko jangwani,' msiende huko jangwani. Au, 'Tazameni, yuko ndani ya nyumba,' msiamini maneno hayo.
“Kwa hiyo mtu yeyote akiwaambia, ‘Yule kule nyikani,’ msiende huko. Au akisema, ‘Yuko kwenye chumba,’ msisadiki.
27 Kama vile radi inavyomulika kutokea mashariki na kuangaza hadi magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwa Mwana wa Adamu.
Kwa maana kama vile umeme utokeavyo mashariki na kuonekana hata magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
28 Popote ulipo mzoga, huko ndiko tai wakusanyikapo.
Kwa maana popote ulipo mzoga, huko ndiko wakusanyikapo tai.
29 Lakini mara baada ya dhiki kuu ya siku zile, Jua litatiwa giza, mwezi hautatoa mwanga wake, nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbinguni zitatikisika.
“Mara baada ya dhiki ya siku zile, “‘jua litatiwa giza, nao mwezi hautatoa nuru yake; nazo nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za anga zitatikisika.’
30 Ndipo ishara ya Mwana wa Adamu itaonekana angani, na makabila yote ya dunia wataomboleza. Watamwona Mwana wa Adamu akija katika mawingu ya angani kwa nguvu na utukufu mkuu.
“Ndipo itakapotokea ishara ya Mwana wa Adamu angani, na makabila yote ya dunia yataomboleza. Nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya angani, katika uwezo na utukufu mkuu.
31 Atawatuma malaika wake kwa sauti kuu ya tarumbeta, nao watawakusanya pamoja wateule wake kutoka pande nne za dunia, kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwingine.
Naye atawatuma malaika zake kwa sauti kuu ya tarumbeta, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwisho mwingine.
32 Jifunzeni somo kutokana na mti mtini. Mara tu tawi linapochipuka na kutoa majani, mnajua kwamba kiangazi kinakaribia.
“Basi jifunzeni somo hili kutokana na mtini: Matawi yake yanapoanza kuchipua na kutoa majani, mnatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.
33 Hivyo pia, mtakapoona mambo haya yote, mnapaswa kujua kwamba amekaribia, karibu na malango.
Vivyo hivyo, myaonapo mambo haya yote, mnatambua kwamba wakati u karibu, hata malangoni.
34 Kweli nawaambia, kizazi hiki hakitapita, hadi mambo yote haya yatakuwa yametokea.
Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia.
35 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
36 Lakini kuhusu siku ile na saa hakuna mtu ajuaye, hata malaika wa mbinguni, wala Mwana, bali Baba peke yake.
“Kwa habari ya siku ile na saa, hakuna ajuaye, hata malaika walio mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake.
37 Kama vile ilivyokuwa katika siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa kuja kwa Mwana wa Adamu.
Kama ilivyokuwa wakati wa Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
38 Kwa kuwa katika siku hizo kabla ya gharika watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa hadi siku ile ambayo Nuhu aliingia katika safina,
Kwa maana siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka siku ile Noa alipoingia katika safina.
39 na hawakujua kitu chochote hadi gharika ilipokuja na kuwasomba wote - ndivyo itakavyokuwa kuja kwa Mwana wa Adamu.
Nao hawakujua lolote mpaka gharika ilipokuja ikawakumba wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa atakapokuja Mwana wa Adamu.
40 Ndipo watu wawili watakuwa shambani- mmoja atachukuliwa, na mmoja ataachwa nyuma.
Watu wawili watakuwa shambani, naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa.
41 Wanawake wawili watakuwa wanasaga pamoja - mmoja atachukuliwa, na mmoja atabaki.
Wanawake wawili watakuwa wanasaga pamoja, naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa.
42 Kwa hiyo, kuweni macho kwa sababu hamjui ni siku gani ambayo atakuja Bwana wenu.
“Basi kesheni, kwa sababu hamjui ni siku gani atakapokuja Bwana wenu.
43 Lakini mjue kwamba, ikiwa bwana mwenye nyumba angejua ni saa ipi ambayo mwizi angekuja, angekesha na asingeruhusu nyumba yake kuvamiwa.
Lakini fahamuni jambo hili: Kama mwenye nyumba angejua ni wakati gani wa usiku ambao mwizi atakuja, angekesha na hangekubali nyumba yake kuvunjwa.
44 Kwa hiyo, pia mnapaswa kuwa tayari, kwa kuwa Mwana wa Adamu atakuja katika saa msiyoitarajia.
Kwa hiyo ninyi pia hamna budi kuwa tayari, kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja saa msiyotazamia.
45 Hivyo ni nani aliye mwaminifu, mtumwa mwenye akili, ambaye bwana wake amempa madaraka juu ya walio katika nyumba yake, ili awape chakula kwa wakati unaofaa?
“Ni nani basi aliye mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake amemweka kusimamia watumishi wengine katika nyumba yake, ili awape chakula chao kwa wakati unaofaa?
46 Amebarikiwa mtumishi huyo, ambaye bwana wake atamkuta akifanya hivyo wakati ajapo.
Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo.
47 Kweli nawaambia kwamba bwana atamweka juu ya kila kitu kilicho chake.
Amin, nawaambia, atamweka mtumishi huyo kuwa msimamizi wa mali yake yote.
48 Lakini kama mtumwa mwovu akisema moyoni mwake, 'Bwana wangu amekawia,'
Lakini kama huyo mtumishi ni mwovu, naye akasema moyoni mwake, ‘Bwana wangu atakawia muda mrefu,’
49 na akaanza kuwapiga watumishi wake, na akala na kulewa vileo,
kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, na kula na kunywa pamoja na walevi.
50 Bwana wa mtumwa huyo atakuja katika siku ambayo haitarajii, na katika saa ambayo haijui.
Basi bwana wa mtumishi huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua.
51 Bwana wake atamkata vipande viwili na kumweka katika nafasi moja sawa na wanafiki, ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.
Atamkata vipande vipande na kumweka katika sehemu moja pamoja na wanafiki, mahali ambako kutakuwa ni kulia na kusaga meno.

< Mathayo 24 >