< Mathayo 19 >
1 Ilitokea wakati Yesu alipomaliza maneno hayo, akaondoka Galilaya, na akaenda mpakani mwa Yudea mbele ya mto Jordani.
2 Umati mkubwa ukamfuata, na akawaponya huko.
3 Mafarisayo wakamjia, wakamjaribu, wakamwambia, “Je ni halali kwa mtu kumwacha mke wake kwa sababu yoyote?”
4 Yesu akajibu na kusema, “Hamkusoma, kwamba yeye aliyewaumba mwanzo aliwaumba mume na mke?
5 Na tena akasema, 'Kwa sababu hiyo mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuungana na mke wake, nao wawili watakuwa mwili mmoja?'
6 Hivyo siyo wawili tena, bali mwili mmoja. Basi, kile alichokiunganisha Mungu, mtu yeyote asikitenganishe.”
7 Wakamwambia, “Sasa kwa nini Musa alituamuru kutoa hati ya talaka na kumwacha?”
8 Akawaambia, “Kwa ugumu wenu wa mioyo Musa aliwaruhusu kuwaacha wake zenu, lakini tangu mwanzo haikuwa hivyo.
9 Nawaambieni, kwamba yeyote atayemwacha mke wake, isipokuwa kwa sababu ya uzinzi, na akamwoa mwingine, amezini. Na mwanaume atakayemwoa mke aliyeachwa amezini.”
10 Wanafunzi wakamwambia Yesu, “Kama ndivyo ilivyo kwa mume na mkewe, siyo vizuri kuoa.”
11 Lakini Yesu akawaambia, “Si kila mtu anaweza kupokea mafundisho haya, bali ni kwa wale tu walioruhusiwa kupokea.
12 Kwa vile wapo matowashi waliozaliwa tokea tumboni mwa mama zao. Na vilevile kuna matowashi waliofanywa na watu. Na kuna matowashi waliojifanya matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kupokea mafundisho haya na ayapokee.”
13 Kisha akaletewa baadhi ya watoto wadogo ili awawekee mikono juu yao na kuomba, lakini wanafunzi wake wakawakemea.
14 Bali Yesu akasema, “Waruhusuni watoto wadogo, wala msiwakataze kuja kwangu, kwa maana ufalme wa mbinguni ni wa watu kama wao.
15 Naye akaweka mikono yake juu yao, na kisha akaondoka pale.
16 Tazama mtu mmoja akaja kwa Yesu na kusema, “Mwalimu, ni kitu gani kizuri ninachotakiwa kufanya ili nipate kuwa na uzima wa milele?” (aiōnios )
17 Yesu akamwambia, “Kwa nini unaniuliza ni kitu gani kizuri? Kuna mmoja tu aliye mwema, lakini kama ukitaka kupata uzima, shika sheria za Mungu.”
18 Yule mtu akamwuliza, “Ni sheria zipi?” Yesu akasema, “Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo,
19 waheshimu baba yako na mama yako, na mpende jirani yako kama nafsi yako.”
20 Mtu yule akamwambia, “Mambo yote hayo nimeyatii. Bado ninahitaji nini?
21 “Yesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze ulivyo navyo, na uwape maskini, na utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo unifuate.”
22 Lakini kijana yule aliposikia yale Yesu aliyomwambia, akaondoka kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na amemiliki mali nyingi.
23 Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kweli nawaambieni, ni vigumu kwa mtu tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni.
24 Tena nawaambieni, ni rahisi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko kwa mtu tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”
25 Wanafunzi waliposikia hivyo, wakashangaa sana na kusema, “Ni yupi basi atakayeokoka?”
26 Yesu akawatazama na kusema, “Kwa wanadamu hilo haliwezekani, lakini kwa Mungu yote yanawezekana.”
27 Kisha Petro akamjibu na kumwambia, “Tazama, tumeacha vyote na kukufuata wewe. Ni kitu gani tutakachopata?”
28 Yesu akawaambia, “Kweli nawaambieni, yeye aliyenifuata mimi, katika uzao mpya wakati Mwana wa Adam atakapoketi katika kiti cha enzi cha utukufu wake, ninyi pia mtaketi juu ya viti kumi na viwili vya enzi, kuwahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.
29 Kila mmoja wenu aliyeacha nyumba, kaka, dada, baba, mama, watoto, au shamba kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia na kuurithi uzima wa milele. (aiōnios )
30 Lakini wengi walio wa kwanza sasa, watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.