< Mathayo 18 >
1 Muda huo huo wanafunzi wakaja kwa Yesu na kumwambia, “Ni nani aliye mkubwa katika ufalme wa mbinguni?”
2 Yesu akamwita mtoto mdogo, akamweka katikati yao,
3 na kusema, “Kweli nawaambieni, msipotubu na kuwa kama watoto wadogo hamtaweza kuingia katika ufalme wa Mungu.
4 Hivyo yeyote ajishushaye kama mtoto mdogo, mtu kama huyo ni mkuu katika ufalme wa mbinguni.
5 Na yeyote ampokeaye mtoto mdogo kwa jina langu anipokea mimi.
6 Lakini yeyote asababishaye mmoja kati ya wadogo hawa wanaoniamini kuasi, itakuwa vizuri kwa mtu huyo jiwe kuu la kusagia likafungwa shingoni mwake, na kuzamishwa kilindini mwa bahari.
7 Ole kwa dunia kwa sababu ya wakati wa kukwazwa! kwa kuwa haina budi kwa nyakati hizo kuja, lakini ole kwake kwa mtu yule nyakati hizo zitakuja kwa ajili yake!
8 kama mkono wako au mguu wako ukikusababishia kukwazika, ukate na uutupe mbali na wewe. Ni vizuri zaidi kwako wewe kuingia kwenye uzima ukiwa bila mkono au kilema, kuliko kutupwa kwenye moto wa milele ukiwa na mikono yote au miguu yote. (aiōnios )
9 Kama jicho lako likikukwaza, uling`oe na ulitupe mbali na wewe. Ni vizuri zaidi kwako wewe uingie kwenye uzima na jicho moja, kuliko kutupwa kwenye moto wa milele ukiwa na macho yote. (Geenna )
10 Tazameni kwamba msije mkamdharau mmoja wa wadogo hawa. Kwa maana nawambieni kuwa mbinguni kuna malaika wao siku zote wakiutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni.
11 (Zingatia: Maneno yanayoonekana kama ya msitari wa 11, “Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kuokoa kile kilichokuwa kimepotea” hayakuonekana katika nakala bora za kale).
12 Mnafikiri nini? Ikiwa mtu ana kondoo mia moja, na mmoja wao akapotea, je hatawaacha tisini na tisa ya mlimani na kwenda kumtafuta mmoja aliyepotea?
13 Na akiisha kumpata, kweli nawaambieni, anamfurahia kuliko wale tisini na tisa wasiopotea.
14 Vivyo hivyo, siyo mapenzi ya Baba yenu wa mbinguni kuwa mmoja wa wadogo hawa aangamie.
15 Kama ndugu yako akikukosea, nenda, kamwonyeshe dosari iliyopo kati yako na yeye akiwa pekee yake. Kama akikusikiliza, utakuwa umemrejesha ndugu yako.
16 Lakini kama hatakusikiliza, mchukue ndugu mmoja au wawili zaidi pamoja nawe, kwa kuwa kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno linaweza kuthibitishwa.
17 Na kama akipuuza kuwasikiliza, liambie kanisa jambo hilo, kama akipuuza vilevile kulisikiliza kanisa, basi na awe kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru.
18 Kweli nawaambieni, chochote kile mtakachokifunga duniani na mbinguni kitafungwa. na chochote mtakachokifungua duniani na mbinguni kitafunguliwa.
19 Tena nawaambieni kwamba kama watu wawili kati yenu wakikubaliana juu ya jambo lolote duniani waliombalo, hilo Baba yangu wa mbinguni atalifanya.
20 Kwa kuwa wawili au watatu wakikusanyika pamoja kwa jina langu, Mimi niko katikati yao.
21 Tena Petro akaja na kumwambia Yesu, “Bwana, ni mara ngapi ndugu yangu akinikosea nami nimsamehe? Hata mara saba?”
22 Yesu akamwambia, “Sikuambii mara saba, lakini hata sabini mara saba.
23 Kwa sababu hiyo ufalme wa mbinguni ni sawa na mfalme fulani aliyetaka kusahihisha hesabu kutoka kwa watumwa wake.
24 Alipoanza kusahihisha hesabu, mtumwa moja akaletwa kwake ambaye alikuwa anamdai talanta elfu kumi.
25 Kwa kuwa hakuwa na njia ya kulipa, bwana wake aliagiza auzwe, mke wake pamoja na watoto wake na kila kitu alichokuwa nacho, na malipo yafanyike.
26 Hivyo mtumwa alianguka, akapiga magoti mbele yake, akisema, 'Bwana, uwe na uvumilivu pamoja nami, na nitakulipa kila kitu.'
27 Hivyo bwana wa yule mtumwa, kwa kuwa alisukumwa sana na huruma, alimwachilia na kumsamehe deni hilo
28 Lakini mtumwa yule alitoka na kumpata mmoja kati ya watumwa wenzake, aliyekuwa anamdai denari mia. Alimvuta, akamkaba kooni, na kumwambia, 'Nilipe kile ninachokudai.'
29 Lakini yule mtumwa mwenzake alianguka na kumsihi sana, akisema, 'Uwe na uvumilivu nami, na nitakulipa.'
30 Lakini mtumwa yule wa kwanza alikataa. Badala yake, alienda na kumtupa gerezani, mpaka atakapo mlipa kile anachomdai.
31 Na walipoona watumwa wenzake kile kilichotokea. Walisikitishwa sana. Walikuja na kumwambia bwana wao kila kitu kilichotokea.
32 Ndipo yule bwana wa mtumwa yule alimwita, na kumwambia, 'Ewe mtumwa mwovu, nilikusamehe wewe deni langu lote kwa sababu ulinisihi sana.
33 Je! Haukutakiwa kuwa na huruma kwa mtumwa mwenzio, kama mimi nilivyokuhurumia wewe?
34 Bwana wake alikasirika na kumkabidhi kwa wale watesaji mpaka atakapolipa kiasi chote alichokuwa anadaiwa.
35 Hivyo ndivyo Baba yangu wa Mbinguni atakavyowafanyia, kama kila mmoja wenu hatamsamehe ndugu yake kutoka moyoni mwenu.”