< Marko 1 >
1 Huu ni mwanzo wa injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.
2 Kama ilivyoandikwa na nabii Isaya, “Tazama, ninamtuma mjumbe wangu mbele yako, mmoja atakayetayarisha njia yako.
3 Sauti ya mtu aitaye nyikani, “Ikamilisheni njia ya Bwana; zinyosheni njia zake”.
4 Yohana alikuja, akibatiza nyikani na kuhubiri ubatizo wa toba kwa msamaha wa dhambi.
5 Nchi yote ya Yudea na watu wote wa Yerusalemu walikwenda kwake. Walikuwa wakibatizwa naye katika mto Yordani, wakiungama dhambi zao.
6 Yohana alikuwa anavaa vazi la manyoya ya ngamia na mkanda wa ngozi kiunoni mwake, na alikuwa anakula nzige na asali ya porini.
7 Alihubiri na kusema, “Yupo mmoja anakuja baada yangu mwenye nguvu zaidi kuliko mimi, na sina hadhi hata ya kuinama chini na kufungua kamba za viatu vyake.
8 Mimi niliwabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza ninyi kwa Roho Mtakatifu.”
9 Ilitokea katika siku hizo kwamba Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, na alibatizwa na Yohana katika mto Yordani.
10 Wakati Yesu alipoinuka kutoka majini, aliona mbingu zimegawanyika wazi na Roho akishuka chini juu yake kama njiwa.
11 Na sauti ilitoka mbinguni, “Wewe ni Mwanangu mpendwa. Ninapendezwa sana na wewe.”
12 Kisha mara moja Roho akamlazimisha kwenda nyikani.
13 Alikuwako nyikani siku arobaini, akijaribiwa na Shetani. Alikuwa pamoja na wanyama wa mwituni, na malaika walimhudumia.
14 Sasa baada ya Yohana kukamatwa, Yesu alikuja Galilaya akitangaza injili ya Mungu,
15 akisema, “Muda umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuamini katika injili”.
16 Na akipita kando ya bahari ya Galilaya, alimwona Simoni na Andrea ndugu wa Simoni wakitupa nyavu zao katika bahari, kwa kuwa walikuwa wavuvi.
17 Yesu aliwaambia, “Njoni, nifuateni, na nitawafanya wavuvi wa watu.”
18 Na mara moja waliacha nyavu na wakamfuata.
19 Wakati Yesu alipotembea umbali kidogo, alimwona Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana ndugu yake; walikuwa kwenye mtumbwi wakitengeneza nyavu.
20 Mara aliwaita na wao walimwacha baba yao Zebedayo ndani ya mtumbwi na watumishi waliokodiwa, wakamfuata.
21 Na walipofika Kaperinaumu, siku ya Sabato, Yesu aliingia kwenye sinagogi na kufundisha.
22 Walilishangaa fundisho lake, kwa vile alikuwa akiwafundisha kama mtu ambaye ana mamlaka na siyo kama waandishi.
23 Wakati huo huo kulikuwa na mtu katika sinagogi lao aliyekuwa na roho mchafu, na alipiga kelele,
24 akisema, “Tuna nini cha kufanya na wewe, Yesu wa Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Nakujua u nani. Wewe ni Mtakatifu pekee wa Mungu!”
25 Yesu alimkemea pepo na kusema, “Nyamaza na utoke ndani yake!”
26 Na roho mchafu alimwangusha chini na akatoka kwake wakati akilia kwa sauti ya juu.
27 Na watu wote walishangaa, hivyo wakaulizana kila mmoja, “Hii ni nini? Fundisho jipya lenye mamlaka? Hata huamuru pepo wachafu nao wanamtii!”
28 Na habari kuhusu yeye mara moja zikasambaa kila mahali ndani ya mkoa wote wa Galilaya.
29 Na mara moja baada ya kutoka nje ya sinagogi, waliingia nyumbani mwa Simoni na Andrea wakiwa na Yakobo na Yohana.
30 Sasa mama mkwe wa Simoni alikuwa amelala mgonjwa wa homa, na mara moja walimwambia Yesu habari zake.
31 Hivyo alikuja, alimshika kwa mkono, na kumwinua juu; homa ikaondoka kwake, na akaanza kuwahudumia.
32 Jioni hiyo wakati jua limekwisha zama, walimletea kwake wote waliokuwa wagonjwa, au waliopagawa na pepo.
33 Mji wote walikusanyika pamoja katika mlango.
34 Aliwaponya wengi waliokuwa wagonjwa wa magonjwa mbalimbali na kutoa pepo wengi, bali hakuruhusu pepo kuongea kwa sababu walimjua.
35 Aliamka asubuhi na mapema, wakati ilikuwa bado giza; aliondoka na kwenda mahali pa faragha na aliomba huko.
36 Simoni na wote waliokuwa pamoja naye walimtafuta.
37 Walimpata na wakamwambia, “Kila mmoja anakutafuta”
38 Aliwaambia, “Twendeni mahali pengine, nje katika miji inayozunguka, ili niweze kuhubiri huko pia. Ndiyo sababu nilikuja hapa.”
39 Alikwenda akipita Galilaya yote, akihubiri katika masinagogi yao na kukemea pepo.
40 Mwenye ukoma mmoja alikuja kwake. Alikuwa akimsihi; alipiga magoti na alimwambia, “Kama unataka, waweza kunifanya niwe safi.”
41 Akisukumwa na huruma, Yesu alinyosha mkono wake na kumgusa, akimwambia, “Ninataka. Uwe msafi.”
42 Mara moja ukoma ukamtoka, na alifanywa kuwa safi.
43 Yesu akamwonya vikali na akamwambia aende mara moja,
44 Alimwambia, “Hakikisha hausemi neno kwa yeyote, lakini nenda, ujionyeshe kwa kuhani, na utoe dhabihu kwa ajili ya utakaso ambayo Musa aliagiza, kama ushuhuda kwao.”
45 Lakini alikwenda na kuanza kumwambia kila mmoja na kueneza neno zaidi hata Yesu hakuweza tena kuingia mjini kwa uhuru. Hivyo alikaa mahali pa faragha na watu walikuja kwake kutoka kila mahali.