< Marko 9 >

1 Na alisema kwao, “Hakika nasema kwenu, baadhi yenu kuna watu waliosimama hapa hawataonja mauti kabla ya kuuona ufalme wa Mungu ukija kwa nguvu.”
Yesu akaendelea kuwaambia, “Amin, nawaambia, kuna watu waliosimama hapa ambao hawataonja mauti kabla ya kuuona Ufalme wa Mungu ukija kwa nguvu.”
2 Na baada ya siku sita, Yesu aliwachukua Petro, Yakobo na Yohana pamoja naye mlimani, pekee yao. Ndipo alianza kubadilika mbele yao.
Baada ya siku sita, Yesu akawachukua Petro, Yakobo na Yohana, akawapeleka juu ya mlima mrefu, mahali walipokuwa faraghani. Huko, Yesu akageuka sura mbele yao.
3 Mavazi yake yakaanza kung'aa sana, meupe zaidi, meupe kuliko mng'arishaji yeyote duniani.
Mavazi yake yakawa na weupe wa kuzima macho, meupe kuliko ambavyo mtu yeyote duniani angaliweza kuyangʼarisha.
4 Ndipo Eliya pamoja na Musa walitokea mbele yao, na walikuwa wakiongea na Yesu.
Mose na Eliya wakawatokea, wakawa wanazungumza na Yesu.
5 Petro alijibu akamwambia Yesu, “Mwalimu, ni vyema sisi kuwa hapa, na tujenge vibanda vitatu, kimoja kwa ajili yako, kimoja kwa ajili Musa na kingine kwa ajili ya Eliya.”
Petro akamwambia Yesu, “Rabi, ni vyema sisi tukae hapa. Turuhusu tujenge vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Mose na kingine cha Eliya.”
6 (Kwa kuwa hakujua nini cha kusema, waliogopa sana.)
Petro hakujua aseme nini kwa maana yeye na wenzake walikuwa wameogopa sana.
7 Wingu lilitokea na kuwafunika. Ndipo sauti ikatoka mawinguni ikisema, “Huyu ni mwanangu mpendwa. Msikieni yeye.”
Ndipo pakatokea wingu, likawafunika, nayo sauti kutoka lile wingu ikasema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Msikieni yeye.”
8 Ghafla, walipokuwa wakitazama, hawakumuona yeyote pamoja nao, isipokuwa Yesu tu.
Mara walipotazama huku na huku, hawakuona tena mtu mwingine yeyote pamoja nao isipokuwa Yesu.
9 Walipokuwa wanateremka kutoka mlimani, aliwaamuru kutokumwambia mtu yeyote yale yote waliyoyaona, mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuka kutoka kwa wafu.
Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawakataza wasimwambie mtu yeyote mambo waliyoona, mpaka Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka kutoka kwa wafu.
10 Ndipo waliyatunza mambo wao wenyewe. Lakini walijadiliana wao kwa wao ni nini maana yake “kufufuliwa kutoka kwa wafu”
Wakalihifadhi jambo hilo wao wenyewe, lakini wakawa wanajiuliza, “Huku kufufuka kwa wafu maana yake nini?”
11 Walimwuliza Yesu,”Kwa nini waandishi husema lazima Eliya aje kwanza?”
Wakamuuliza, “Kwa nini walimu wa sheria husema kwamba ni lazima Eliya aje kwanza?”
12 Akawaambia, “hakika Eliya atakuja kwanza kuokoa vitu vyote. Kwa nini imeandikwa Mwana wa Adamu lazima apate mateso mengi na achukiwe?
Yesu akawajibu, “Ni kweli, Eliya yuaja kwanza ili kutengeneza mambo yote. Mbona basi imeandikwa kwamba Mwana wa Adamu ni lazima ateseke sana na kudharauliwa?
13 Lakini nasema kwenu Eliya alikwisha kuja, na walimfanya kama walivyopenda, kama vile maandiko yasemavyo kuhusu yeye.”
Lakini ninawaambia, Eliya amekwisha kuja, nao wakamtendea walivyopenda, kama ilivyoandikwa kumhusu yeye.”
14 Na waliporudi kwa wanafunzi, waliona kundi kubwa limewazunguka na Masadukayo walikuwa wanabishana nao.
Walipowafikia wale wanafunzi wengine, wakawakuta wamezungukwa na umati mkubwa wa watu na baadhi ya walimu wa sheria wakibishana nao.
15 Na mara walipomwona, kundi lote lilishangaa na kumkimbilia kumsalimia.
Mara wale watu walipomwona Yesu, wakastaajabu sana, wakamkimbilia ili kumsalimu.
16 Aliwauliza wanafunzi wake, “Mnabishana nao juu ya nini?”
Akawauliza wanafunzi wake, “Mnabishana nao kuhusu nini?”
17 Mmoja wao katika kundi alimjibu, “Mwalimu, nilimleta mwanangu kwako; ana roho chafu ambayo humfanya asiweze kuongea,
Mtu mmoja miongoni mwa ule umati wa watu akajibu, “Mwalimu, nilimleta kwako mwanangu ambaye ana pepo mchafu anayemfanya asiweze kuongea.
18 na humsababishia kutetemeka na kumwangusha chini, na kutoka povu mdomoni na kusaga meno na kukakamaa. Niliwaomba wanafunzi wako kumtoa pepo, lakini hawakuweza.
Kila mara huyo pepo mchafu ampagaapo mwanangu, humwangusha chini na kumfanya atokwe povu mdomoni na kusaga meno, kisha mwili wake hukauka. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.”
19 Aliwajibu, “Kizazi kisichoamini, nitakaa nanyi kwa muda gani? Nitachukuliana nanyi hadi lini? Mleteni kwangu.”
Yesu akawaambia, “Enyi kizazi kisicho na imani! Nitakuwa pamoja nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni mvulana kwangu.”
20 Walimleta mtoto wake. Roho mchafu alipomwona Yesu, ghafla ilimtia katika kutetemeka. Mvulana alianguka chini na kutoa povu mdomoni.
Nao wakamleta yule mvulana. Yule pepo mchafu alipomwona Yesu, mara akamtia yule mvulana kifafa, akaanguka, akagaagaa chini huku akitokwa na povu kinywani.
21 Yesu alimwuliza baba yake, “Amekuwa katika hali hii kwa muda gani?” Baba alisema, “Tangu utoto.
Yesu akamuuliza baba yake, “Mwanao amekuwa katika hali hii tangu lini?” Akamjibu, “Tangu utoto wake.
22 Mara nyingine huanguka katika moto au kwenye maji, na kujaribu kumwangamiza. Kama unaweza kufanya chochote tuhurumie na utusaidie.”
Mara kwa mara huyo pepo mchafu amekuwa akimwangusha kwenye moto au kwenye maji ili kumwangamiza. Lakini kama unaweza kufanya jambo lolote, tafadhali tuhurumie utusaidie.”
23 Yesu alimwambia, “Kama uko tayari? Kila kitu kinawezekana kwa yeyote aaminiye.”
Yesu akamwambia, “Kama ukiweza kuamini, yote yawezekana kwake yeye aaminiye.”
24 Ghafla baba wa mtoto alilia na kusema, “Naamini! Nisaidie kutokuamini kwangu.”
Mara baba yake yule mvulana akapiga kelele akisema, “Ninaamini. Nisaidie kutokuamini kwangu!”
25 Wakati Yesu alipoona kundi linakimbilia kwao, alimkemea roho mchafu na kusema, “wewe roho bubu na kiziwi, nakuamuru mwache, usiingie kwake tena.”
Yesu alipoona kwamba umati wa watu unakusanyika pamoja mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akimwambia, “Wewe pepo bubu na kiziwi, nakuamuru umtoke, wala usimwingie tena!”
26 Alilia kwa nguvu na kumhangaisha mtoto na roho alimtoka. Mtoto alionekana kama amekufa, Ndipo wengi walisema, “Amekufa,”
Yule pepo mchafu akiisha kupiga kelele, akamtia kifafa kwa nguvu, na akamtoka. Yule mvulana alikuwa kama maiti, hivyo watu wengi wakasema, “Amekufa.”
27 Lakini Yesu alimchukua kwa mkono akamwinua, na mtoto alisimama.
Lakini Yesu akamshika mkono, akamwinua, naye akasimama.
28 Wakati Yesu alipoingia ndani, wanafunzi wake walimwuliza faragha, “Kwa nini hatukuweza kumtoa?”
Baada ya Yesu kuingia ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamuuliza wakiwa peke yao, “Mbona sisi hatukuweza kumtoa huyo pepo mchafu?”
29 Aliwaambia, “kwa namna hii hatoki isipokuwa kwa maombi.”
Yesu akawajibu, “Hali hii haiwezi kutoka isipokuwa kwa kuomba na kufunga.”
30 Walitoka pale na kupitia Galilaya. Hakutaka mtu yeyote ajue walipo,
Wakaondoka huko, wakapitia Galilaya. Yesu hakutaka mtu yeyote afahamu mahali walipo,
31 kwa kuwa alikuwa anafundisha wanafunzi wake. Aliwaambia, “Mwana wa Adamu atafikishwa mikononi mwa watu, na watamuua. Atakapokuwa amekufa, baada ya siku tatu atafufuka tena.”
kwa maana alikuwa anawafundisha wanafunzi wake. Akawaambia, “Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutiwa mikononi mwa watu. Nao watamuua, lakini siku tatu baada ya kuuawa atafufuka.”
32 Lakini hawakuelewa maelezo haya, na waliogopa kumwuliza.
Lakini wao hawakuelewa kile alimaanisha, nao waliogopa kumuuliza maana yake.
33 Ndipo walifika Karperinaumu. Wakati akiwa ndani ya nyumba aliwauliza, ''Mlikuwa mnajadili nini njiani”?
Basi wakafika Kapernaumu na baada ya kuingia nyumbani akawauliza, “Mlikuwa mnabishana nini kule njiani?”
34 Lakini walikuwa kimya. Kwani walikuwa wanabishana njiani kwamba nani alikuwa mkubwa zaidi.
Lakini hawakumjibu, kwa sababu njiani walikuwa wakibishana kuhusu nani miongoni mwao alikuwa mkuu zaidi ya wote.
35 Alikaa chini akawaita kumi na wawili pamoja, na alisema nao, “Kama yeyote anataka kuwa wa kwanza, ni lazima awe wa mwisho na mtumishi wa wote.”
Akaketi chini, akawaita wote kumi na wawili, akawaambia: “Kama mtu yeyote akitaka kuwa wa kwanza, hana budi kuwa wa mwisho na mtumishi wa wote.”
36 Alimchukua mtoto mdogo akamweka katikati yao. Akamchukua katika mikono yake, akasema,
Kisha akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha katikati yao. Akamkumbatia, akawaambia,
37 “Yeyote ampokeaye mtoto kama huyu kwa jina langu, pia amenipokea mimi, na ikiwa mtu amenipokea, hanipokei mimi tu, lakini pia aliyenituma.”
“Mtu yeyote amkaribishaye mmoja wa hawa watoto wadogo kwa Jina langu, anikaribisha mimi. Naye anikaribishaye mimi, amkaribisha Baba yangu aliyenituma.”
38 Yohana alimwambia, “Mwalimu tulimwona mtu anatoa pepo kwa jina lako na tukamzuia, kwa sababu hatufuati.”
Yohana akamwambia, “Mwalimu, tumemwona mtu akitoa pepo wachafu kwa jina lako, nasi tukamkataza, kwa sababu yeye si mmoja wetu.”
39 Lakini Yesu alisema, “Msimzuie, kwa kuwa hakuna atakayefanya kazi kubwa kwa jina langu na ndipo baadaye aseme neno baya lolote juu yangu.
Yesu akasema, “Msimkataze, kwa kuwa hakuna yeyote atendaye miujiza kwa Jina langu ambaye baada ya kitambo kidogo aweza kunena lolote baya dhidi yangu.
40 Yeyote asiyekuwa kinyume nasi yuko upande wetu.
Kwa maana yeyote asiye kinyume chetu, yuko upande wetu.
41 Yeyote atakayekupa kikombe cha maji ya kunywa kwa sababu uko na Kristo, kweli nawaambia, hatapoteza thawabu yake.
Amin, nawaambia, yeyote awapaye ninyi kikombe cha maji kwa Jina langu kwa sababu ninyi ni mali ya Kristo, hakika hataikosa thawabu yake.”
42 Yeyote anayewakosesha hawa wadogo waniaminio mimi, ingekuwa vyema kwake kufungiwa jiwe la kusagia shingoni na kutupwa baharini.
“Kama mtu yeyote akimsababisha mmojawapo wa wadogo hawa wanaoniamini kutenda dhambi, ingekuwa bora kwake afungiwe jiwe kubwa la kusagia shingoni mwake, na kutoswa baharini.
43 Kama mkono wako ukikukosesha ukate. Ni heri kuingia katika uzima bila mkono kuliko kuingia kwenye hukumu ukiwa na mikono yote. Katika moto “usiozimika”. (Geenna g1067)
Kama mkono wako ukikusababisha kutenda dhambi, ukate. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa na mkono mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili lakini ukaingia jehanamu, mahali ambako moto hauzimiki. [ (Geenna g1067)
44 (Zingatia: Mstari hii, “Mahali ambapo funza hawafi na moto usiozimika.” haumo katika nakala za kale).
Mahali ambako funza wake hawafi wala moto wake hauzimiki.]
45 Kama mguu wako ukikukosesha, ukate. Ni vyema kwako kuingia uzimani ukiwa kilema, kuliko kutupwa hukumuni na miguu miwili. (Geenna g1067)
Kama mguu wako ukikusababisha kutenda dhambi, ukate. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili lakini ukaingia jehanamu. [ (Geenna g1067)
46 (Zingatia: Mstari huu, “Mahali ambapo funza hawafi na moto usioweza kuzimika” haumo kwenye nakala za kale).
Mahali ambako funza wake hawafi wala moto hauzimiki.]
47 Kama jicho lako likikukosesha ling'oe. Ni vyema kwako kuingia katika Ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja, kuliko kuwa na macho mawili na kutupwa kuzimu. (Geenna g1067)
Nalo jicho lako likikusababisha kutenda dhambi, lingʼoe. Ni afadhali kwako kuingia katika Ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja, kuliko kuwa na macho mawili lakini ukatupwa jehanamu, (Geenna g1067)
48 Mahali palipo na funza wasiokufa, na moto usiozimika.
mahali ambako “‘funza wake hawafi, wala moto wake hauzimiki.’
49 Kwa kuwa kila mmoja atakolezwa na moto.
Kila mmoja atatiwa chumvi kwa moto.
50 Chumvi ni nzuri, kama chumvi ikipoteza ladha yake, utaifanyaje iwe na ladha yake tena? Muwe na chumvi miongoni mwenu wenyewe, na muwe na amani kwa kila mmoja.”
“Chumvi ni nzuri, lakini ikipoteza ladha yake utaifanyaje ili iweze kukolea tena? Mwe na chumvi ndani yenu, mkaishi kwa amani, kila mmoja na mwenzake.”

< Marko 9 >