< Marko 7 >
1 Mafarisayo na baadhi ya waandishi ambao walikuwa wametokea Yerusalemu walikusanyika kumzunguka yeye.
Baadhi ya Mafarisayo na walimu wa Sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu walikusanyika mbele ya Yesu.
2 Na waliona kuwa baadhi ya wanafunzi wake walikula mkate kwa mikono najisi; ambayo haikuoshwa.
Waliona kwamba baadhi ya wanafunzi wake walikula mikate kwa mikono najisi, yaani bila kunawa.
3 (kwa Mafarisayo na Wayahudi wote hawali mpaka wameosha mikono yao vizuri; wanashikilia utamaduni wa wazee. Wakati
Maana Mafarisayo na Wayahudi wengine wote huzingatia mapokeo ya wazee wao: hawali kitu kabla ya kunawa mikono ipasavyo.
4 Mafarisayo wanaporudi kutoka mahali pa soko, hawali mpaka wameoga kwanza. Na kuna sheria zingine ambazo wanazifuata kabisa, ikiwa ni pamoja na kuosha vikombe, masufuria, vyombo vya shaba, na hata viti vinavyotumika wakati wa chakula.)
Tena hawali kitu chochote kutoka sokoni mpaka wamekiosha kwanza. Kuna pia desturi nyingine walizopokea kama vile namna ya kuosha vikombe, sufuria na vyombo vya shaba.
5 Mafarisayo na waandishi walimuuliza Yesu, “Kwa nini wanafunzi wako hawaishi kulingana na tamaduni za wazee, kwani wanakula mkate pasipo kunawa mikono?”
Basi, Mafarisayo na walimu wa Sheria wakamwuliza Yesu, “Mbona wanafunzi wako hawayajali mapokeo tuliyopokea kwa wazee wetu, bali hula chakula kwa mikono najisi?”
6 Lakini yeye aliwaambia, “Isaya alitabiri vizuri kuhusu ninyi wanafiki, aliandika, 'Watu hawa wananiheshimu kwa midomo yao, lakini mioyo yao iko mbali na mimi.
Yesu akawajibu, “Wanafiki ninyi! Nabii Isaya alitabiri ukweli juu yenu alipoandika: Watu hawa, asema Mungu, huniheshimu kwa maneno matupu, lakini mioyoni mwao wako mbali nami.
7 Wananifanyia ibaada zisizo na maana, wakifundisha sheria za wanadamu kama mapokeo yao.'
Kuniabudu kwao hakufai, maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu.
8 Mmeiacha sheria ya Mungu na kushikilia kwa wepesi tamaduni za wanadamu.”
Ninyi mnaiacha amri ya Mungu na kushikilia maagizo ya watu.”
9 Na akasema kwao, “Mmeikataa amri ya Mungu kwa urahisi ili kwamba mtunze tamaduni zenu!
Yesu akaendelea kusema, “Ninyi mnajua kuepa kwa ujanja sheria ya Mungu kwa ajili ya kufuata mapokeo yenu.
10 Kwa kuwa Musa alisema, 'mheshimu baba yako na mama yako,' na 'Yeye asemaye mabaya juu ya baba yake au mama yake hakika atakufa.'
Maana Mose aliamuru: Waheshimu baba yako na mama yako, na, Anayemlaani baba au mama, lazima afe.
11 Lakini mnasema, 'kama mtu akisema kwa baba yake au mama, “Msaada wowote ambao mngepokea kutoka kwangu ni hazina ya Hekalu,”' (hiyo ni kusema kwamba, 'imetolewa kwa Mungu')
Lakini ninyi mwafundisha, Kama mtu anacho kitu ambacho angeweza kuwasaidia nacho baba au mama yake, lakini akasema kwamba kitu hicho ni Korbani (yaani ni zawadi kwa Mungu),
12 hivyo haumruhusu kufanya jambo lolote kwa ajili ya baba au mama yake.
basi, halazimiki tena kuwasaidia wazazi wake.
13 Mnaifanya amri ya Mungu kuwa bure kwa kuleta tamaduni zenu. Na mambo mengi ya jinsi hiyo mnayoyafanya.”
Hivyo ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa ajili ya mafundisho mnayopokezana. Tena mnafanya mambo mengi ya namna hiyo.”
14 Aliwaita makutano tena na kuwaambia, “Mnisikilize mimi, ninyi nyote, na mnielewe.
Yesu aliuita tena ule umati wa watu, akawaambia, “Nisikilizeni nyote, mkaelewe.
15 Hakuna chochote kutoka nje ya mtu ambacho chaweza kumchafua mtu kiingiapo kwake. Bali ni kile kimtokacho mtu ndicho kimchafuacho.
Hakuna kitu kinachoingia ndani ya mtu toka nje ambacho chaweza kumtia mtu najisi. Lakini kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia mtu najisi.”
16 (Zingatia: mstari huu, “kama mtu yeyote ana masikio ya kusikia, na asikie” haumo kwenye nakala za kale).
Mwenye masikio na asikie!
17 Yesu alipowaacha makutano na kuingia nyumbani, wanafunzi wake wakamwuliza kuhusu mfano huo.
Alipouacha umati wa watu na kuingia nyumbani, wanafunzi wake walimwuliza maana ya huo mfano.
18 Yesu akasema, “Na ninyi pia bado hamjaelewa? Hamuoni kwamba chochote kimuingiacho mtu hakiwezi kumchafua,
Naye akawaambia, “Je, hata ninyi hamwelewi? Je, hamwelewi kwamba kitu kinachomwingia mtu toka nje hakiwezi kumtia unajisi,
19 kwa sababu hakiwezi kwenda kwenye moyo wake, lakini kinaingia katika tumbo lake na kisha kinapita kwenda chooni.” Kwa maelezo haya Yesu alivifanya vyakula vyote kuwa safi.
kwa maana hakimwingii moyoni, ila tumboni, na baadaye hutolewa nje chooni?” (Kwa kusema hivyo, Yesu alivihalalisha vyakula vyote.)
20 Alisema, “Ni kile ambacho kinamtoka mtu ndicho kimchafuacho.
Akaendelea kusema, “Kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomtia najisi.
21 Kwa kuwa hutoka ndani ya mtu, nje ya moyo, hutoka mawazo maovu, zinaa, wizi, mauaji,
Kwa maana kutoka ndani, katika moyo wa mtu, hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji,
22 uasherati, tamaa mbaya, uovu, udanganyifu, kujamiiana, wivu, kashfa, majivuno, ujinga.
uzinzi, uchoyo, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, kashfa, kiburi na upumbavu.
23 Maovu haya yote yanatoka ndani, ndiyo yale yamchafuayo mtu.”
Maovu hayo yote yatoka ndani ya mtu, nayo humtia mtu najisi.”
24 Aliamka kutoka pale na kuondoka kwenda katika mkoa wa Tiro na Sidoni. Aliingia ndani na hakutaka mtu yeyote ajue kuwa alikuwa hapo, lakini haikuwezekana kumficha.
Yesu aliondoka hapo, akaenda hadi wilaya ya Tiro. Huko aliingia katika nyumba moja na hakutaka mtu ajue; lakini hakuweza kujificha.
25 Lakini ghafla mwanamke, ambaye mtoto wake mdogo alikuwa na roho mchafu, alisikia habari zake, akaja, na akaanguka miguuni pake.
Mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo, alisikia habari za Yesu. Basi, akaja akajitupa chini mbele ya miguu yake.
26 Mwanamke huyo alikuwa Myunani, wa kabila la Kifoeniki. Alimsihi yeye amfukuze pepo kutoka kwa binti yake.
Mama huyo alikuwa Mgiriki, mwenyeji wa Sirofoinike. Basi, akamwomba Yesu amtoe binti yake pepo mchafu.
27 Yesu akamwambia mwanamke, “Waache watoto walishwe kwanza, kwa kuwa sio sawa kuuchukua mkate wa watoto na kuwatupia mbwa.”
Yesu akamwambia, “Kwanza watoto washibe; kwa maana si vizuri kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”
28 Lakini mwanamke akamjibu na kusema, “Ndiyo Bwana, hata mbwa chini ya meza hula mabaki ya chakula cha watoto.”
Lakini huyo mama akasema, “Sawa, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto.”
29 Akamwambia, “Kwa kuwa umesema hivi, uko huru kwenda. Pepo ameshamtoka binti yako.”
Yesu akamwambia, “Kwa sababu ya neno hilo, nenda. Pepo amemtoka binti yako!”
30 Mwanamke alirudi nyumbani kwake na akamkuta binti yake amelala kitandani, na pepo alikuwa amemtoka.
Basi, akaenda nyumbani kwake, akamkuta mtoto amelala kitandani, na pepo amekwisha mtoka.
31 Yesu alitoka tena nje ya mkoa wa Tiro na kupitia Sidoni kuelekea Bahari ya Galilaya mpaka kanda ya Dikapolisi.
Kisha Yesu aliondoka wilayani Tiro, akapitia Sidoni, akafika ziwa Galilaya kwa kupitia nchi ya Dekapoli.
32 Na wakamletea mtu aliyekuwa kiziwi na alikuwa hawezi kuzungumza vizuri, walimsihi Yesu aweke mikono juu yake.
Basi, wakamletea bubu-kiziwi, wakamwomba amwekee mikono.
33 Alimtoa nje ya kusanyiko kwa siri, na akaweka vidole vyake kwenye masikio yake, na baada ya kutema mate, aligusa ulimi wake.
Yesu akamtenga na umati wa watu, akamtia vidole masikioni, akatema mate na kumgusa ulimi.
34 Alitazama juu mbinguni, akahema na kumwambia, “Efata,” hiyo ni kusema “funguka!”
Kisha akatazama juu mbinguni, akapiga kite, akamwambia, “Efatha,” maana yake, “Funguka.”
35 Na muda ule ule masikio yakafunguka, na kilichokuwa kimezuia ulimi kiliharibiwa na akaweza kuongea vizuri.
Mara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukafunguliwa, akaanza kusema sawasawa.
36 Na aliwaamuru wasimwambie mtu yeyote. Lakini kadri alivyowaamuru, ndivyo walivyotangaza habari hizo kwa wingi.
Yesu akawaamuru wasimwambie mtu juu ya jambo hilo. Lakini kadiri alivyowakataza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari hiyo.
37 Hakika walishangazwa, na kusema, “Amefanya kila kitu vizuri. Hata amewafanya viziwi kusikia na mabubu kuongea.”
Watu walishangaa sana, wakasema, “Amefanya yote vyema: amewajalia viziwi kusikia, na bubu kusema!”