< Marko 14 >
1 Ilikuwa siku mbili tu baada ya sikukuu ya Pasaka na ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Makuhani wakuu na waandishi walikuwa wakitafuta namna ya kumkamata Yesu kwa hila na kumuua.
2 Kwa kuwa walisema, “Sio wakati huu wa sikukuu, watu wasije wakafanya ghasia.”
3 Wakati Yesu alipokuwa Bethania nyumbani kwa Simoni mkoma, na alipokuwa akielekea mezani, mwanamke mmoja alikuja kwake akiwa na chupa ya marashi ya nardo safi yenye gharama kubwa sana, aliivunja chupa na kuimimina juu ya kichwa chake.
4 Lakini kulikuwa na baadhi yao waliokasirika. Waliambiana wao kwa wao wakisema, “Ni nini sababu ya upotevu huu?
5 Manukato haya yangeweza kuuzwa kwa zaidi ya dinari mia tatu, na wakapewa maskini.” Nao walimkemea.
6 Lakini Yesu alisema, “Mwacheni peke yake. Kwa nini mnamsumbua? Amefanya jambo zuri kwangu.
7 Siku zote maskini mnao, na wakati wowote mnapotamani mnaweza kufanya mazuri kwao, lakini hamtakuwa nami wakati wote.
8 Amefanya kile anachoweza: ameupaka mwili wangu mafuta kwa ajili ya maziko.
9 Kweli nawaambia, kila mahali injili inapohubiriwa katika ulimwengu wote, kile alichofanya mwanamke huyu kitazungumzwa kwa ukumbusho wake.
10 Kisha Yuda Iskariote, mmoja wa wale kumi na wawili, alikwenda kwa wakuu wa makuhani ili kwamba apate kumkabidhi kwao.
11 Wakati wakuu wa Makuhani waliposikia hivyo, walifurahi na wakaahidi kumpa fedha. Alianza kutafuta nafasi ya kumkabidhi kwao.
12 Katika siku ya kwanza ya mkate usiotiwa chachu, wakati walipotoa mwanakondoo wa pasaka, wanafunzi wake walimwambia, “Unataka twende wapi tukaandae ili upate kula mlo wa Pasaka?”
13 Aliwatuma wanafuzi wake wawili na kuwaambia, “Nendeni mjini, na mwanamume ambaye amebeba mtungi ataonana nanyi. Mfuateni.
14 Nyumba atakayoingia, mfuateni na mmwambie mwenye nyumba hiyo, 'Mwalimu asema, “Kiko wapi chumba cha wageni mahali nitakapokula Pasaka na wanafunzi wangu?”
15 Atawaonesha chumba cha juu kikubwa chenye samani ambacho kiko tayari. Fanyeni maandalizi kwa ajili yetu pale.”
16 Wanafunzi waliondoka wakaenda mjini; walikuta kila kitu kama alivyokuwa amewaambia, na wakaandaa mlo wa Pasaka.
17 Wakati ilipokuwa jioni, alikuja na wale Kumi na wawili.
18 Na walipokuwa wakiikaribia meza na kula, Yesu alisema, “Kweli nawaambia, mmoja kati yenu anayekula pamoja nami atanisaliti.”
19 Wote walisikitika, na mmoja baada ya mwingine walimwambia, “Hakika siyo mimi?”
20 Yesu alijibu na kuwaambia, “Ni mmoja wa Kumi na wawili kati yenu, mmoja ambaye sasa anachovya tonge katika bakuli pamoja nami.
21 Kwa kuwa Mwana wa Adamu atakwenda kama vile maandiko yasemavyo juu yake. Lakini ole wake mtu yule ambaye kupitia yeye Mwana wa Adamu atasalitiwa! Ingekuwa vizuri zaidi kwake kama mtu yule asingezaliwa.”
22 Na walipokuwa wakila, Yesu alichukua mkate, akaubariki, na kuumega. Aliwapa akisema, “Chukueni. Huu ni mwili wangu.”
23 Alichukua kikombe, akashukuru, na akawapatia, na wote wakakinywea.
24 Aliwaambia, “Hii ni damu yangu ya agano, damu imwagikayo kwa ajili ya wengi.
25 Kweli nawaambia, sitakunywa tena katika zao hili la mzabibu mpaka siku ile nitakapokunywa mpya katika ufalme wa Mungu.”
26 Walipokwisha kuimba wimbo, walikwenda nje katika Mlima wa Mizeituni.
27 Yesu aliwaaambia, “Ninyi nyote mtajitenga mbali kwa sababu yangu, kwa kuwa imeandikwa, 'Nitampiga mchungaji na kondoo watatawanyika.'
28 Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia mbele yenu Galilaya.”
29 Petro alimwambia, “Hata kama wote watakuacha, mimi sitakuacha.”
30 Yesu alimwambia, “Kweli nakuambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, utakuwa umenikana mara tatu.”
31 Lakini Petro alisema, “Hata itanilazimu kufa pamoja nawe, sitakukana.” Wote walitoa ahadi ile ile.
32 Walikuja kwenye eneo lililoitwa Gethsemane, na Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa wakati nasali.”
33 Aliwachukua Petro, Yakobo, na Yohana pamoja naye, akaanza kuhuzunika na kutaabika sana.
34 Aliwaambia, “Nafsi yangu ina huzuni sana, hata kufa. Bakini hapa na mkeshe.”
35 Yesu alienda mbele kidogo, akaanguka chini, akaomba, kama ingewezekana, kwamba saa hii ingemwepuka.
36 Alisema, “Aba, Baba, Mambo yote kwako yanawezekana. Niondolee kikombe hiki. Lakini siyo kwa mapenzi yangu, bali mapenzi yako.”
37 Alirudi na kuwakuta wamelala, na akamwambia Petro, “Simoni, je umelala? Hukuweza kukesha hata saa moja?
38 Kesheni na muombe kwamba msije mkaingia katika majaribu. Hakika roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.”
39 Alienda tena na kuomba, na alitumia maneno yaleyale.
40 Alikuja tena akawakuta wamelala, kwa kuwa macho yao yalikuwa mazito na hawakujua nini cha kumwambia.
41 Alikuja mara ya tatu na kuwaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Yatosha! Saa imefika. Tazama! Mwana wa Adamu atasalitiwa mikononi mwa wenye dhambi.
42 Amkeni, twendeni. Tazama, yule anayenisaliti yuko karibu.”
43 Mara tu alipokuwa bado anaongea, Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili, alifika, na kundi kubwa kutoka kwa wakuu wa makuhani, waandishi na wazee wenye mapanga na marungu.
44 Wakati huo msaliti wake alikuwa amewapa ishara, akisema, Yule nitakayembusu, ndiye. Mkamateni na kumpeleka chini ya ulinzi.”
45 Wakati Yuda alipofika, moja kwa moja alienda kwa Yesu na kusema, “Mwalimu!” Na akambusu.
46 Kisha wakumtia chini ya ulinzi na kumkamata.
47 Lakini mmoja kati yao aliyesimama karibu naye alichomoa upanga wake akampiga mtumishi wa kuhani mkuu na kumkata sikio.
48 Yesu aliwaambia, “Mmekuja kunikamata kwa mapanga na marungu kama mnyang'anyi?
49 Wakati kila siku nilikuwa nanyi na nikifundisha hekaluni, hamkunikamata. Lakini hili limefanyika ili maandiko yatimie.
50 Na wale wote waliokuwa na Yesu walimwacha na kukimbia.
51 Kijana mmoja alimfuata, aliyekuwa amevaa shuka tu aliyokuwa amejifunika kumzunguka; walimkamata lakini
52 aliwaponyoka akaiacha shuka pale akakimbia uchi.
53 Walimwongoza Yesu kwa kuhani mkuu. Pale walikusanyika pamoja naye makuhani wakuu wote, wazee, na waandishi.
54 Petro naye alimfuata Yesu kwa mbali, kuelekea kwenye ua wa kuhani mkuu. Aliketi pamoja na walinzi, waliokuwa karibu na moto wakiota ili kupata joto.
55 Wakati huo makuhani wakuu wote na Baraza lote walikuwa wakitafuta ushahidi dhidi ya Yesu ili wapate kumwua. Lakini hawakuupata.
56 Kwa kuwa watu wengi walileta ushuhuda wa uongo dhidi yake, lakini hata ushahidi wao haukufanana.
57 Baadhi walisimama na kuleta ushahidi wa uongo dhidi yake; wakisema,
58 “Tulimsikia akisema, 'Nitaliharibu hekalu hili lililotengenezwa kwa mikono, na ndani siku tatu nitajenga lingine lisilotengenezwa kwa mikono.'”
59 Lakini hata ushahidi wao haukufanana.
60 Kuhani mkuu alisimama katikati yao na akamwuliza Yesu, “Je, huna jibu? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?”
61 Lakini alikaa kimya na hakujibu chochote. Mara Kuhani mkuu alimwuliza tena, “Je wewe ni Kristo, mwana wa Mbarikiwa?”
62 Yesu alisema, “Mimi ndiye. Na utamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kulia wa nguvu akija na mawingu ya mbinguni.”
63 Kuhani mkuu alirarua mavazi yake na kusema, “Je, bado tunahitaji mashahidi?
64 Mmesikia kufuru. Uamuzi wenu ni upi?” Na wote walimhukumu kama mmoja aliyestahili kifo.
65 Baadhi wakaanza kumtemea mate na kumfunika uso na kumpiga na kumwambia, “Tabiri!” Maafisa walimchukua na kumpiga.
66 Na Petro alipokuwa bado yuko chini uani, mtumishi mmoja wa wasichana wa kuhani mkuu alikuja kwake.
67 Alimwona Petro alipokuwa amesimama akiota moto, na alimtazama kwa kumkaribia. Kisha alisema, “Nawe pia ulikuwa na Mnazareti, Yesu”.
68 Lakini alikataa, akisema, “Sijui wala sielewi kuhusu kile unachosema!” Kisha alitoka akaenda nje uani. (Zingatia; Mstari huu, “Na jogoo akawika” haumo kwenye nakala za kale).
69 Lakini mtumishi wa kike pale, alimwona na alianza kuwaambia tena wale ambao walikuwa wamesimama pale, “Mtu huyu ni mmoja wao!”
70 Lakini alikana tena. Baadaye kidogo wale waliokuwa wamesimama pale walikuwa wakimwambia Petro, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana wewe pia ni Mgalilaya.”
71 Lakini alianza kujiweka mwenyewe chini ya laana na kuapa, “Simjui mtu huyu mnayemsema.”
72 Kisha jogoo aliwika mara ya pili. Kisha Petro alikumbuka maneno ambayo Yesu aliyokuwa amemwambia: “Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” Na alianguka chini na kulia.