< Luka 4 >
1 Kisha, Yesu akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Mto Jordani, na aliongozwa na Roho jangwani
2 kwa siku arobaini, na huko alijaribiwa na Ibilisi. Wakati huo hakula chochote, na mwisho wa wakati huo alihisi njaa.
3 Ibilisi akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, liamru jiwe hili kuwa mkate.”
4 Yesu akamjibu, “Imeandikwa; 'mtu hataishi kwa mkate pekee.”
5 Kisha Ibilisi alimwongoza juu kwenye kilele cha mlima, na akamwonyesha falme zote za dunia kwa muda mfupi.
6 Ibilisi akamwambia, “Nitakupa mamlaka ya kutawala falme hizi zote pamoja na fahari zake. Naweza kufanya hivyo kwa sababu vyote vimekabidhiwa kwangu nivitawale, na ninaweza kumpa yeyote nitakaye kumpa.
7 Kwahiyo, kama utaniinamia na kuniabudu, vitu hivi vyote vitakuwa vyako.”
8 Lakini Yesu alijibu na kumwambia, “Imeandikwa, “lazima umwabudu Bwana Mungu wako, na lazima umtumikie Yeye peke yake.”
9 Baadaye Ibilisi alimwongoza Yesu hadi Yerusalemu na kumweka sehemu ya juu kabisa ya jengo la hekalu na kumwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, jitupe chini kutoka hapa.
10 Kwa sababu imeandikwa, “Atawaagiza malaika zake wakutunze na kukulinda,
11 na watakuinua juu mikononi mwao ili kwamba usiumize miguu yako juu ya jiwe.”
12 Yesu akijibu alimwambia, “Imenenwa, “usimjaribu Bwana Mungu wako.”
13 Ibilisi alipomaliza kumjaribu Yesu, alienda zake na kumwacha hadi wakati mwingine.
14 Kisha Yesu alirudi Galilaya kwa nguvu za Roho, na habari kumhusu yeye zikaenea na kusambaa katika mikoa jirani yote.
15 Alifundisha katika masinagogi yao, na kila mmoja alimsifu.
16 Siku moja alikwenda Nazareti, mji ambao alilelewa na kukulia. Kama ilivyokuwa desturi yake aliingia kwenye sinagogi siku ya sabato, na alisimama kusoma maandiko.
17 Alikabidhiwa gombo la nabii Isaya, hivyo, alilifungua gombo na akatafuta sehemu iliyoandikwa,
18 “Roho wa Bwana yuu juu yangu, kwa sababu alinitia mafuta kuhubiri habari njema kwa maskini. Amenituma kutangaza uhuru kwa wafungwa, na kuwafanya wasioona waweze kuona tena. Kuwaweka huru wale wanaogandamizwa,
19 kuutangaza mwaka ambao Bwana ataonesha wema wake.”
20 Kisha akalifunga gombo, akamrudishia kiongozi wa sinagogi, na akaketi chini. Macho ya watu wote waliokuwa katika sinagogi yalimwangalia yeye.
21 Alianza kuzungumza nao akisema, “Leo andiko hili limetimizwa masikioni mwenu.”
22 Kila mmoja pale alishuhudia kile alichokisema Yesu, na wengi miongoni mwao walishangazwa na maneno ya hekima yaliyokuwa yakitoka katika kinywa chake. Walikuwa wakisema, “huyu ni kijana tu wa Yusufu, siyo hivyo?”
23 Yesu akawaambia, “hakika mtasema methali hii kwangu, “Tabibu, jiponye mwenyewe. Chochote tulichosikia ukifanya Kapernaumu, kifanye hapa pia kijijini kwako.”
24 Pia alisema, “hakika nawaambia ninyi, hakuna nabii anayekubalika katika nchi yake.”
25 Lakini nawaambia ninyi kweli kwamba kulikuwa na wajane wengi Israel katika kipindi cha Eliya, wakati mbingu ilipofungwa kusiwe na nvua kwa miaka mitatu na nusu, wakati kulipokuwa na njaa kubwa katika nchi yote.
26 Lakini Eliya hakutumwa kwa yeyote mmoja wao, lakini kwa mjane mmoja tu aliyeishi Sarepta karibu na mji wa Sidoni.
27 Pia, kulikuwa na wakoma wengi Israel katika kipindi cha Elisha nabii, lakini hakuna hatammoja wao aliyeponywa isipokuwa Naamani mtu wa Siria.
28 Watu wote ndani ya sinagogi walijawa na gadhabu walipoyasikia haya yote.
29 Walisimama na kumsukumizia nje ya mji, na kumwongoza mpaka kwenye ukingo wa mlima wa mji ambapo mji wao ulijengwa juu yake, ili waweze kumtupa chini.
30 Lakini alipita salama katikati yao na akaenda zake.
31 Kisha alitelemkia Kapernaumu, katika mji wa Galilaya. Sabato moja alikuwa akifundisha watu ndani ya sinagogi.
32 Walishangazwa na mafundisho yake, kwasababu alifundisha kwa mamlaka.
33 Sasa siku hiyo ndani ya sinagogi, kulikuwa na mtu aliyekuwa na roho ya pepo mchafu, na alilia kwa sauti ya juu,
34 “Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Ninajua wewe ni nani! Wewe ni mtakatifu wa Mungu!”
35 Yesu alimkemea pepo akisema, “Nyamaza kimya, na umtoke mtu huyu!” Pepo yule alipomtupa mtu yule chini katikati yao, alimtoka yule mtu bila ya kumsababishia maumivu yoyote.
36 Watu wote walishangaa, na waliendelea kuzungumzia jambo hilo kila mmoja na mwenzake. Wakasema, “Ni maneno ya aina gani haya?” Anawaamuru roho wachafu kwa mamlaka na nguvu na watondoka.”
37 Hivyo, habari juu ya Yesu zilienea kila sehemu katika maeneo yanayozunguka mkoa huo.
38 Kisha Yesu aliondoka katika mji huo na akaingia katika nyumba ya Simoni. Sasa, mama mkwe wake na Simoni alikuwa anaumwa homa kali, na wakamsihi kwa niaba yake.
39 Hivyo, Yesu alimsogelea, akaikemea ile homa na ikamwachia. Ghafla alisimama na akaanza kuwatumikia.
40 Jua lilipokuwa likizama, watu walimletea Yesu kila mmoja aliyekuwa mgonjwa wa maradhi ya aina mbalimbali. Aliweka mikono yake juu ya kila mgonjwa na akawaponya wote.
41 Mapepo pia yaliwatoka wengi wao yakilia kwa sauti na kusema, “Wewe ni mwana wa Mungu!” Yesu aliwakemea mapepo na hakuwaruhusu waongee, kwa sababu walijua kwamba yeye alikuwa ni Kristo.
42 Wakati kulipopambazuka, alienda eneo lisilokuwa na watu. Makutano ya watu walikuwa wakimtafuta na wakaja katika eneo alilokuwapo. Walijaribu kumzuia asiende mbali na wao.
43 Lakini akawaambia, “Lazima pia nihubiri habari njema za ufalme wa Mungu katika miji mingine mingi, kwa kuwa hii ndiyo sababu nilitumwa hapa.”
44 Kisha aliendelea kuhubiri ndani ya masinagogi katika uyahudi wote.