< Luka 24 >
1 Mapema sana siku ya kwanza ya juma, walikuja kaburini, wakileta manukato ambayo walikuwa wameyaandaa.
2 Wakakuta jiwe limevingirishwa mbali na kaburi.
3 Wakaingia ndani, lakini hawakuukuta mwili wa Bwana Yesu.
4 Ilitokea kwamba, wakati wamechanganyikiwa kuhusu hili, ghafla, watu wawili walisimama katikati yao wamevaa mavazi ya kung'aa.
5 Wanawake wakiwa wamejaa hofu na wakiinamisha nyuso zao chini, wakawaambia wanawake, “Kwanini mnamtafuta aliye hai miongoni mwa wafu?
6 Hayupo hapa, ila amefufuka! Kumbukeni alivyosema nanyi alipokuwa angali Galilaya,
7 akisema kwamba Mwana wa Adamu lazima atolewe kwenye mikono ya watu wenye dhambi na asulubishwe, na siku ya tatu, afufuke tena.”
8 Wale wanawake wakakumbuka maneno yake,
9 na wakarudi kutoka kaburini na wakawaambia mambo haya yote wale kumi na moja na wengine wote.
10 Basi Maria Magdalena, Joana, Maria mama wa Yakobo, na wanawake wengine pamoja nao wakatoa taarifa hizi kwa mitume.
11 Lakini ujumbe huu ukaonekana kama mzaha tu kwa mitume, na hawakuwaamini wale wanawake.
12 Hata hivyo Petro aliamka, na akakimbia kuelekea kaburini, na akichungulia na kuangalia ndani, aliona sanda peke yake. Petro kisha akaondoka akaenda nyumbani kwake, akistaajabu nini ambacho kimetokea.
13 Na tazama, wawili miongoni mwao walikuwa wakienda siku hiyo hiyo katika kijiji kimoja kiitwacho Emmau, ambacho kilikuwa maili sitini kutoka Yerusalemu.
14 Wakajadiliana wao kwa wao kuhusu mambo yote yaliyotokea.
15 Ikatokea kwamba, wakati walipokuwa wakijadiliana na kuulizana maswali, Yesu akasogea karibu akaambatana nao.
16 Lakini macho yao yalizuiliwa katika kumtambua yeye.
17 Yesu akawaambia, “Nini ambacho ninyi wawili mnakiongelea wakati mnatembea?” Wakasimama pale wakionekana na huzuni.
18 Mmoja wao, jina lake Cleopa, akamjibu, “Je wewe ni mtu pekee hapa Yerusalemu ambaye hajui mambo yaliyotokea huko siku hizi?”
19 Yesu akawaambia, “Mambo gani?” Wakamjibu, “Mambo kuhusu Yesu Mnazareti, ambaye alikuwa nabii, muweza katika matendo na maneno mbele za Mungu na watu wote.
20 Na kwa jinsi ambayo wakuu wa makuhani na viongozi wetu walivyomtoa kuhukumiwa kifo na kumsulubisha.
21 Lakini tulitumaini kwamba yeye ndiye atakaye waweka huru Israeli. Ndiyo, mbali na haya yote, sasa ni siku ya tatu tangu mambo haya yatokee.
22 Lakini pia, baadhi ya wanawake kutoka katika kundi letu walitushangaza, baada ya kuwapo kaburini asubuhi na mapema.
23 Walipoukosa mwili wake, wakaja, wakisema kwamba waliona pia maono ya malaika waliosema kwamba yu hai.
24 Baadhi ya wanaume ambao walikuwa pamoja nasi walienda kaburini, na kukuta ni kama vile wanawake walivyosema. Lakini hawakumuona yeye.”
25 Yesu akawaambia, “Ninyi watu wajinga na wenye mioyo mizito ya kuamini yote ambayo manabii wamesema!
26 Je haikuwa lazima Yesu kuteseka kwa mambo haya, na kuingia katika utukufu wake?”
27 Kisha kuanzia kutoka kwa Musa na manabii wote, Yesu akawatafsiria mambo yanayomuhusu yeye katika maandiko yote.
28 Walipokaribia kile kijiji, huko walikokuwa wakienda, Yesu akafanya kana kwamba anaendelea mbele.
29 Lakini walimlazimisha, wakisema, “Kaa pamoja nasi, maana inaelekea jioni na siku ni kama imeisha.” Hivyo Yesu akaingia kwenda kukaa nao.
30 Ilitokea kwamba, wakati amekaa nao kula, alichukua mkate, akaubariki, na kuuvunja, akawapa.
31 Kisha macho yao yakafunguliwa, wakamjua, na akatoweka ghafla mbele ya macho yao.
32 Wakasemezana wao kwa wao, “Hivi mioyo yetu haikuwaka ndani yetu, wakati alipoongea nasi njiani, wakati alipotufungulia maandiko?”
33 Wakanyanyuka saa hiyo hiyo, na kurudi Yerusalemu. Wakawakuta wale kumi na mmoja wamekusanyika pamoja, na wale waliokuwa pamoja nao,
34 wakisema, “Bwana amefufuka kwelikweli, na amemtokea Simoni.”
35 Hivyo wakawaambia mambo yaliyotokea njiani, na namna Yesu alivyodhihirishwa kwao katika kuumega mkate.
36 Wakati wakiongea mambo hayo, Yesu mwenyewe alisimama katikati yao, na akawaambia, “Amani iwe kwenu.”
37 Lakini waliogopa na kujawa na hofu, na wakafikiri kwamba waliona roho.
38 Yesu akawaambia, Kwanini mnafadhaika? Kwanini maswali yanainuka mioyoni mwenu?
39 Angalieni mikono yangu na miguu yangu, kwamba ni mimi mwenyewe. Niguseni na muone. Kwa maana roho haina nyama na mifupa, kama mnionavyo mimi kuwa navyo.”
40 Alipokwisha kusema hivi, akawaonyesha mikono yake na miguu yake.
41 Walipokuwa bado na furaha iliyochanganyikana na kutokuamini, na kustaajabu, Yesu akawaambia, “Je mna kitu chochote cha kula?”
42 Wakampa kipande cha samaki aliyechomwa.
43 Yesu akakichukua, na kukila mbele yao.
44 Akawaambia, “Nilipokuwa nanyi, niliwaambia kwamba yote yalioandikwa kwenye sheria ya Musa na manabii na Zaburi lazima yatimilike.”
45 Kisha akafungua akili zao, kwamba waweze kuyaelewa maandiko.
46 Akawaambia, “Kwamba imeandikwa, Kristo lazima ateseke, na kufufuka tena kutoka katika wafu siku ya tatu.
47 Na toba na msamaha wa dhambi lazima ihubiriwe kwa jina lake kwa mataifa yote, kuanzia kutokea Yerusalemu.
48 Ninyi ni mashahidi wa mambo haya.
49 Angalia, nawapelekea ahadi ya Baba yangu juu yenu. Lakini subirini hapa jijini, mpaka mtakapovishwa nguvu kutoka juu.
50 Kisha Yesu akawaongoza nje mpaka walipokaribia Bethania. Akainua mikono yake juu, na akawabariki.
51 Ikatokea kwamba, wakati alipokuwa akiwabariki, aliwaacha na akabebwa juu kuelekea mbinguni.
52 Basi wakamwabudu, na kurudi Yerusalemu na furaha kuu.
53 Waliendelea kuwepo hekaluni, wakimbariki Mungu.