< Luka 23 >
1 Mkutano wote wakasimama, wakampeleka Yesu mbele ya Pilato.
2 Wakaanza kumshutumu, wakisema, “Tumemkuta mtu huyu akipotosha taifa letu, kwa kukataza tusitoe kodi kwa Kaisari, na akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, Mfalme.”
3 Pilato akamuuliza, akisema, “Je wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Na Yesu akamjibu akisema, “Wewe wasema hivyo”.
4 Pilato akamuambia kuhani mkuu na makutano, “Sioni kosa kwa mtu huyu”.
5 Lakini wao wakasisitiza, wakisema, “Amekuwa akiwachochea watu, akifundisha katika Uyahudi yote, kuanzia Galilaya na sasa yuko hapa.”
6 Pilato aliposikia haya, akaulizia kama mtu huyo ni wa Galilaya?
7 Alipotambua kuwa alikuwa chini ya utawala wa Herode, akampeleka Yesu kwa Herode, ambaye naye alikuwa Yerusalemu kwa siku hizo.
8 Herode alipomuona Yesu, alifurahi sana kwasababu alitaka kumuona kwa siku nyingi. Alisikia habari zake na alitamani kuona moja ya miujiza ikifanywa na yeye.
9 Herode alimhoji Yesu kwa maneno mengi, lakini Yesu hakumjibu chochote.
10 Makuhani wakuu pamoja na waandishi walisimama kwa ukali wakimshitaki.
11 Herode pamoja na maaskari wake, walimtukana na kumdhihaki, na kumvika mavazi mazuri, kisha akamrudisha Yesu kwa Pilato.
12 Herode na Pilato wakawa marafiki kuanzia siku hiyo, (kabla ya hapo walikuwa maadui).
13 Pilato akawaita pomoja makuhani wakuu na watawala na umati wa watu,
14 Akawaambia, “Mmeniletea mtu huyu kama mtu anaye waongoza watu wafanye mabaya, na tazama, baada ya kuwa nimemhoji mbele yenu, sikuona kosa kwa mtu huyu kuhusu mambo yote ambayo ninyi mnamshitaki yeye.
15 Hapana, wala Herode, kwa maana amemrudisha kwetu, na tazama hakuna chochote alichokifanya kinachostahili adhabu ya kifo.
16 Kwahiyo basi nitamuadhibu na kumuachilia.
17 (Sasa, Pilato anawajibika kumuachilia mfungwa mmoja kwa wayahudi wakati wa sikukuu).
18 Lakini wote wakapiga kelele pamoja, wakisema, “Mwondoe huyo, na tufungulie Baraba!”
19 Baraba alikuwa ni mtu ambaye amewekwa gerezani kwa sababu ya uasi fulani katika jiji na kwa kuua.
20 Pilato akawaambia tena, akitamani kumwachilia Yesu.
21 Lakini wao wakapiga kelele, wakisema, “Msulibishe, msulibishe.”
22 Akawauliza kwa mara ya tatu, “kwa nini, huyu mtu amefanya maovu gani? Sikupata kosa linalostahili adhabu ya kifo kwake. Kwahiyo nitakapo maliza kumuadhibu nitamuachilia.”
23 Lakini wakasisitiza kwa sauti ya juu, wakitaka asulubiwe. Na sauti zao zikamshawishi Pilato.
24 Hivyo Pilato akaamua kuwapatia matakwa yao.
25 Akamuachilia yule waliyemtaka ambaye alifungwa kwa kusababisha ghasia na kuua. Lakini akamtoa Yesu kwa matakwa yao.
26 Walipokuwa wakimpeleka, walimkamata mtu mmoja aitwaye Simoni wa Ukirene, akitokea katika nchi, wakamtwika msalaba ili abebe, akimfuata Yesu.
27 umati mkubwa wa watu, na wanawake ambao walihuzunika na kuomboleza kwa ajili yake, walikuwa wakimfuata.
28 Lakini akawageukia, Yesu akawaambia, 'Mabinti wa Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni ninyi wenyewe na kwa ya ajili watoto wenu.
29 Tazama, siku zinakuja ambazo watasema, “Wamebarikiwa walio tasa na matumbo yasiyozaa, na matiti ambayo hayakunyonyesha.
30 Ndipo watakapo anza kuiambia milima, 'Tuangukieni,' na vilima, 'Mtufunike.'
31 Maana kama wakifanya mambo haya ikiwa mti mbichi, itakuwaje ukiwa mkavu?”
32 wanaume wengine, wahalifu wawili, walipelekwa pamoja naye ili wauwawe.
33 Walipofika mahali paitwapo Fuvu la kichwa, ndipo wakamsulubisha pamoja na wale wahalifu, mmoja upande wa kulia na mwingine upande wa kushoto.
34 Yesu alisema, “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. “Nao wakapiga kura, kugawa mavazi yake.
35 Watu walikuwa wamesimama wakiangalia huku watawala wakimdhihaki, wakisema, “Aliwaokoa wengine. Sasa ajiokoe mwenyewe, kama yeye ni Kristo wa Mungu, mteule”.
36 Askari pia walimdharau, walimkaribia yeye na wakumpa siki,
37 wakisema, “Kama wewe ni Mfalme wa Wayahudi jiokoe mwenyewe”
38 Kulikuwa pia na alama juu yake iliyoandikwa “HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI.”
39 Mmoja wa wahalifu aliyesulubishwa alimtukana akisema, “Wewe si Kristo? jiokoe mwenyewe na sisi”
40 Lakini yule mwingine akajibu, akimkemea na akisema, “Je wewe humuogopi Mungu, nawe uko katika hukumu hiyo hiyo?
41 Sisi tupo hapa kwa haki, kwa maana sisi tunapokea kile tunachostahili kwa matendo yetu. Lakini mtu huyu hakufanya chochote kibaya.”
42 Na aliongeza, “Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.”
43 Yesu akamwambia, “Amini nakuambia, leo hii utakuwa pamoja nami Paradiso.”
44 Hapo ilikuwa karibu saa ya sita, giza likaja juu ya nchi yote hadi saa ya tisa,
45 Mwanga wa jua ulizimika. Kisha pazia la hekalu likagawanyika katikati kuanzia juu.
46 Akilia kwa sauti kuu, Yesu alisema, “Baba mikononi mwako naiweka roho yangu,” baada ya kusema haya, akafa.
47 Wakati Akida alipoona yaliyotendeka alimtukuza Mungu akisema, “Hakika huyu alikuwa mtu mwenye haki.”
48 Wakati umati wa watu waliokuja pamoja kushuhudia walipoona mambo yaliyofanyika, walirudi huku wakipiga vifua vyao.
49 Lakini marafiki zake, na wanawake waliomfuata toka Galilaya, walisimama kwa mbali wakiangalia hayo mambo.
50 Tazama, palikuwepo na mtu aitwaye Yusufu, ambaye ni mmoja wa baraza, mtu mzuri na mwenye haki,
51 (alikuwa hajakubaliana na maamuzi au matendo yao), kutoka Armathaya, mji wa Kiyahudi, ambao ulikua ukisubiria ufalme wa Mungu.
52 Mtu huyu, alimkaribia Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu.
53 Alimshusha, na akauzungushia sanda, na akaumweka katika kaburi lililokuwa limechongwa katika jiwe, ambalo hakuna aliyewahi kuzikwa.
54 Ilikuwa ni siku ya maandalizi, na Sabato inakaribia.
55 Wanawake, waliokuja nao kutoka Galilaya, walimfuata, na wakaona kaburi na jinsi mwili wake ulivyolazwa.
56 Walirudi na kuanza kuandaa manukato na marashi. Kisha siku ya sabato walipumzika kwa mujibu wa sheria.