< Luka 23 >
1 Mkutano wote wakasimama, wakampeleka Yesu mbele ya Pilato.
Kisha, wote kwa jumla, wakasimama, wakampeleka Yesu mbele ya Pilato.
2 Wakaanza kumshutumu, wakisema, “Tumemkuta mtu huyu akipotosha taifa letu, kwa kukataza tusitoe kodi kwa Kaisari, na akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, Mfalme.”
Wakaanza kumshtaki wakisema: “Tulimkuta mtu huyu akiwapotosha watu wetu, akipinga kulipa kodi kwa Kaisari na kujiita ati yeye ni Kristo, Mfalme.”
3 Pilato akamuuliza, akisema, “Je wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Na Yesu akamjibu akisema, “Wewe wasema hivyo”.
Pilato akamwuliza Yesu, “Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Yesu akamjibu, “Wewe umesema.”
4 Pilato akamuambia kuhani mkuu na makutano, “Sioni kosa kwa mtu huyu”.
Pilato akawaambia makuhani wakuu na umati wa watu, “Sioni kosa lolote katika mtu huyu.”
5 Lakini wao wakasisitiza, wakisema, “Amekuwa akiwachochea watu, akifundisha katika Uyahudi yote, kuanzia Galilaya na sasa yuko hapa.”
Lakini wao wakasisitiza wakisema: “Anawachochea watu kwa mafundisho yake katika nchi yote ya Yudea; alianza Galilaya, na sasa yuko hapa.”
6 Pilato aliposikia haya, akaulizia kama mtu huyo ni wa Galilaya?
Pilato aliposikia hayo, akauliza, “Je, mtu huyu ni mwenyeji wa Galilaya?”
7 Alipotambua kuwa alikuwa chini ya utawala wa Herode, akampeleka Yesu kwa Herode, ambaye naye alikuwa Yerusalemu kwa siku hizo.
Alipojua kwamba Yesu alikuwa chini ya utawala wa Herode, akampeleka kwa Herode, ambaye wakati huo alikuwa Yerusalemu.
8 Herode alipomuona Yesu, alifurahi sana kwasababu alitaka kumuona kwa siku nyingi. Alisikia habari zake na alitamani kuona moja ya miujiza ikifanywa na yeye.
Herode alifurahi sana alipomwona Yesu. Alikuwa amekwisha sikia habari zake, na hivyo alikuwa anatazamia kwa muda mrefu kumwona kwa macho yake mwenyewe. Zaidi ya hayo, alikuwa anatumaini kumwona Yesu akitenda mwujiza.
9 Herode alimhoji Yesu kwa maneno mengi, lakini Yesu hakumjibu chochote.
Basi, akamwuliza maswali mengi kwa muda mrefu, lakini Yesu hakumjibu neno.
10 Makuhani wakuu pamoja na waandishi walisimama kwa ukali wakimshitaki.
Makuhani wakuu na walimu wa Sheria wakajitokeza mbele, wakatoa mashtaka yao kwa nguvu sana.
11 Herode pamoja na maaskari wake, walimtukana na kumdhihaki, na kumvika mavazi mazuri, kisha akamrudisha Yesu kwa Pilato.
Basi, herode pamoja na maaskari wake, wakamwaibisha Yesu na kumfanyia mzaha; kisha wakamvika vazi la kifalme, wakamrudisha kwa Pilato.
12 Herode na Pilato wakawa marafiki kuanzia siku hiyo, (kabla ya hapo walikuwa maadui).
Herode na Pilato, ambao hapo awali walikuwa maadui, tangu siku hiyo wakawa marafiki.
13 Pilato akawaita pomoja makuhani wakuu na watawala na umati wa watu,
Basi, Pilato akaitisha mkutano wa makuhani wakuu, viongozi na watu,
14 Akawaambia, “Mmeniletea mtu huyu kama mtu anaye waongoza watu wafanye mabaya, na tazama, baada ya kuwa nimemhoji mbele yenu, sikuona kosa kwa mtu huyu kuhusu mambo yote ambayo ninyi mnamshitaki yeye.
akawaambia, “Mmemleta mtu huyu kwangu mkisema kwamba alikuwa anawapotosha watu. Sasa sikilizeni! Baada ya kuchunguza jambo hilo mbele yenu, sikumpata na kosa lolote kuhusu mashtaka yenu juu yake.
15 Hapana, wala Herode, kwa maana amemrudisha kwetu, na tazama hakuna chochote alichokifanya kinachostahili adhabu ya kifo.
Wala si mimi tu, bali hata Herode hakuona kosa lolote, kwa maana amemrudisha kwangu. Ni dhahiri kwamba mtu huyu hakufanya chochote kinachostahili adhabu ya kifo.
16 Kwahiyo basi nitamuadhibu na kumuachilia.
Hivyo, nitaamuru apigwe viboko, halafu nitamwachilia.”
17 (Sasa, Pilato anawajibika kumuachilia mfungwa mmoja kwa wayahudi wakati wa sikukuu).
Kila sikukuu ya Pasaka, ilimlazimu Pilato kuwafungulia mfungwa mmoja.
18 Lakini wote wakapiga kelele pamoja, wakisema, “Mwondoe huyo, na tufungulie Baraba!”
Lakini wote wakapiga kelele pamoja: “Mwondoe huyo, utufungulie Baraba!”
19 Baraba alikuwa ni mtu ambaye amewekwa gerezani kwa sababu ya uasi fulani katika jiji na kwa kuua.
(Baraba alikuwa ametiwa ndani kwa kusababisha uasi katika mji na pia kwa sababu ya kuua.)
20 Pilato akawaambia tena, akitamani kumwachilia Yesu.
Pilato alitaka kumwachilia Yesu, hivyo akasema nao tena;
21 Lakini wao wakapiga kelele, wakisema, “Msulibishe, msulibishe.”
lakini wao wakapiga kelele: “Msulubishe, msulubishe!”
22 Akawauliza kwa mara ya tatu, “kwa nini, huyu mtu amefanya maovu gani? Sikupata kosa linalostahili adhabu ya kifo kwake. Kwahiyo nitakapo maliza kumuadhibu nitamuachilia.”
Pilato akawaambia mara ya tatu, “Amefanya kosa gani? Sioni kosa lolote kwake linalomstahili auawe; kwa hiyo nitampiga viboko, halafu nimwachilie.”
23 Lakini wakasisitiza kwa sauti ya juu, wakitaka asulubiwe. Na sauti zao zikamshawishi Pilato.
Lakini wao wakazidi kupiga kelele kwa nguvu sana, kwamba Yesu ni lazima asulubiwe. Mwishowe, sauti zao zikashinda.
24 Hivyo Pilato akaamua kuwapatia matakwa yao.
Basi, Pilato akaamua kwamba matakwa yao yatimizwe.
25 Akamuachilia yule waliyemtaka ambaye alifungwa kwa kusababisha ghasia na kuua. Lakini akamtoa Yesu kwa matakwa yao.
Akamfungua kutoka gerezani yule waliyemtaka, ambaye alikuwa ametiwa gerezani kwa sababu ya uasi na kuua; akamtoa Yesu kwao, wamfanyie walivyotaka.
26 Walipokuwa wakimpeleka, walimkamata mtu mmoja aitwaye Simoni wa Ukirene, akitokea katika nchi, wakamtwika msalaba ili abebe, akimfuata Yesu.
Walipokuwa wakimpeleka, walikutana na mtu mmoja, aitwaye Simoni wa Kurene, aliyekuwa anatoka shambani. Basi, walimkamata, wakamtwika ule msalaba auchukue nyuma ya Yesu.
27 umati mkubwa wa watu, na wanawake ambao walihuzunika na kuomboleza kwa ajili yake, walikuwa wakimfuata.
Watu, umati kwa umati, walimfuata; miongoni mwao wakiwemo wanawake waliokuwa wanaomboleza na kumlilia.
28 Lakini akawageukia, Yesu akawaambia, 'Mabinti wa Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni ninyi wenyewe na kwa ya ajili watoto wenu.
Yesu akawageukia, akasema, “Enyi kina mama wa Yerusalemu! Msinililie mimi, ila lieni kwa ajili yenu wenyewe na kwa ajili ya watoto wenu.
29 Tazama, siku zinakuja ambazo watasema, “Wamebarikiwa walio tasa na matumbo yasiyozaa, na matiti ambayo hayakunyonyesha.
Maana, hakika siku zitakuja ambapo watasema: Heri yao wale walio tasa, ambao hawakupata kuzaa wala kunyonyesha watoto!
30 Ndipo watakapo anza kuiambia milima, 'Tuangukieni,' na vilima, 'Mtufunike.'
Wakati huo, ndipo watu wataanza kuiambia milima: Tuangukieni! na vilima, Tufunikeni!
31 Maana kama wakifanya mambo haya ikiwa mti mbichi, itakuwaje ukiwa mkavu?”
Kwa maana, kama watu wanautendea mti mbichi namna hiyo, itakuwaje kwa mti mkavu?”
32 wanaume wengine, wahalifu wawili, walipelekwa pamoja naye ili wauwawe.
Waliwachukua pia watu wengine wawili, wahalifu, wauawe pamoja naye.
33 Walipofika mahali paitwapo Fuvu la kichwa, ndipo wakamsulubisha pamoja na wale wahalifu, mmoja upande wa kulia na mwingine upande wa kushoto.
Walipofika mahali paitwapo, “Fuvu la Kichwa,” ndipo wakamsulubisha Yesu pamoja na wale wahalifu wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto.
34 Yesu alisema, “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. “Nao wakapiga kura, kugawa mavazi yake.
Yesu akasema, “Baba, uwasamehe kwa maana hawajui wanalofanya.” Kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura.
35 Watu walikuwa wamesimama wakiangalia huku watawala wakimdhihaki, wakisema, “Aliwaokoa wengine. Sasa ajiokoe mwenyewe, kama yeye ni Kristo wa Mungu, mteule”.
Watu wakawa wamesimama pale wakitazama. Nao viongozi wakamdhihaki wakisema: “Amewaokoa wengine; sasa na ajiokoe mwenyewe, kama yeye ndiye Kristo, mteule wa Mungu!”
36 Askari pia walimdharau, walimkaribia yeye na wakumpa siki,
Askari nao walimdhihaki pia; walimwendea wakampa siki
37 wakisema, “Kama wewe ni Mfalme wa Wayahudi jiokoe mwenyewe”
wakisema: “Kama kweli wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.”
38 Kulikuwa pia na alama juu yake iliyoandikwa “HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI.”
Vilevile maandishi haya yalikuwa yameandikwa na kuwekwa juu yake: “Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi.”
39 Mmoja wa wahalifu aliyesulubishwa alimtukana akisema, “Wewe si Kristo? jiokoe mwenyewe na sisi”
Mmoja wa wale wahalifu waliotundikwa msalabani, alimtukana akisema: “Je, si kweli kwamba wewe ndiwe Kristo? Basi, jiokoe mwenyewe, utuokoe na sisi pia.”
40 Lakini yule mwingine akajibu, akimkemea na akisema, “Je wewe humuogopi Mungu, nawe uko katika hukumu hiyo hiyo?
Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake akisema: “Wewe humwogopi Mungu hata kidogo? Wewe umepata adhabu hiyohiyo.
41 Sisi tupo hapa kwa haki, kwa maana sisi tunapokea kile tunachostahili kwa matendo yetu. Lakini mtu huyu hakufanya chochote kibaya.”
Wewe na mimi tunastahili, maana haya ni malipo ya yale tuliyotenda. Lakini mtu huyu hakufanya chochote kibaya.”
42 Na aliongeza, “Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.”
Kisha akasema, “Ee Yesu! Unikumbuke wakati utakapoingia katika ufalme wako.”
43 Yesu akamwambia, “Amini nakuambia, leo hii utakuwa pamoja nami Paradiso.”
Yesu akamwambia, “Nakwambia kwa hakika, leo utakuwa pamoja nami peponi.”
44 Hapo ilikuwa karibu saa ya sita, giza likaja juu ya nchi yote hadi saa ya tisa,
Ilikuwa yapata saa sita mchana; jua likaacha kuangaza, giza likafunika nchi yote mpaka saa tisa,
45 Mwanga wa jua ulizimika. Kisha pazia la hekalu likagawanyika katikati kuanzia juu.
na pazia lililokuwa limetundikwa Hekaluni likapasuka vipande viwili.
46 Akilia kwa sauti kuu, Yesu alisema, “Baba mikononi mwako naiweka roho yangu,” baada ya kusema haya, akafa.
Yesu akalia kwa sauti kubwa: “Baba, naiweka roho yangu mikononi mwako.” Alipokwisha sema hayo, akakata roho.
47 Wakati Akida alipoona yaliyotendeka alimtukuza Mungu akisema, “Hakika huyu alikuwa mtu mwenye haki.”
Hapo, yule jemadari alipoona yaliyotukia akamsifu Mungu akisema: “Hakika huyu alikuwa mtu mwema.”
48 Wakati umati wa watu waliokuja pamoja kushuhudia walipoona mambo yaliyofanyika, walirudi huku wakipiga vifua vyao.
Watu wale wote waliokuwa wamekusanyika hapo kwa ajili ya tukio hilo, walipoona hayo yaliyotukia, walirudi makwao wakijipiga vifua kwa huzuni.
49 Lakini marafiki zake, na wanawake waliomfuata toka Galilaya, walisimama kwa mbali wakiangalia hayo mambo.
Marafiki zake wote pamoja na wale wanawake walioandamana naye kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali kutazama tukio hilo.
50 Tazama, palikuwepo na mtu aitwaye Yusufu, ambaye ni mmoja wa baraza, mtu mzuri na mwenye haki,
Kulikuwa na mtu mmoja jina lake Yosefu, mwenyeji wa kijiji kimoja cha Wayahudi kiitwacho Armathaya. Alikuwa mtu mwema anayeheshimika;
51 (alikuwa hajakubaliana na maamuzi au matendo yao), kutoka Armathaya, mji wa Kiyahudi, ambao ulikua ukisubiria ufalme wa Mungu.
Alikuwa akitazamia kuja kwa Ufalme wa Mungu. Ingawa alikuwa mmoja wa Baraza kuu la Wayahudi, hakuwa amekubaliana nao katika kitendo chao.
52 Mtu huyu, alimkaribia Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu.
Basi, yeye alikwenda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu.
53 Alimshusha, na akauzungushia sanda, na akaumweka katika kaburi lililokuwa limechongwa katika jiwe, ambalo hakuna aliyewahi kuzikwa.
Kisha, akaushusha mwili huo kutoka msalabani, akauzungushia sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililokuwa limechongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limetumika.
54 Ilikuwa ni siku ya maandalizi, na Sabato inakaribia.
Siku hiyo ilikuwa Ijumaa, na maandalio ya siku ya Sabato yalikuwa yanaanza.
55 Wanawake, waliokuja nao kutoka Galilaya, walimfuata, na wakaona kaburi na jinsi mwili wake ulivyolazwa.
Wale wanawake walioandamana na Yesu kutoka Galilaya walimfuata Yosefu, wakaliona lile kaburi na jinsi mwili wake Yesu ulivyowekwa
56 Walirudi na kuanza kuandaa manukato na marashi. Kisha siku ya sabato walipumzika kwa mujibu wa sheria.
Halafu, walirudi nyumbani, wakatayarisha manukato na marashi kuyapaka mwili wa Yesu. Siku ya Sabato walipumzika kama ilivyoamriwa na sheria.