< Luka 21 >
1 Yesu alitazama akawaona wanaume matajiri waliokuwa wanaweka zawadi zao kwenye hazina.
2 Akamuona mjane mmoja masikini akiweka senti zake mbili.
3 Hivyo akasema, “Kweli nawaambieni, huyu Mjane maskini ameweka nyingi kuliko wengine wote.
4 Hawa wote wametoa hizi zawadi kutoka katika vingi walivyonavyo. Lakini huyu mjane, katika umaskini wake, ametoa fedha zote alizokuwa nazo kwa ajili ya kuishi kwake.”
5 Wakati wengine walipokuwa wakisema juu ya hekalu, namna lilivyokuwa limepambwa na mawe mazuri na matoleo, alisema,
6 “Kwa habari ya mambo haya mnayoyaona, siku zitakuja ambazo hakuna jiwe moja ambalo litaachwa juu ya jiwe jingine ambalo halitabomolewa.”
7 Hivyo wakamuuliza, wakasema, “Mwalimu, mambo haya yatatokea lini? Na nini ni itakuwa ishara kwamba haya mambo yako karibu kutokea?”
8 Yesu akajibu, “Muwe waangalifu kwamba msidanganywe. Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, 'Mimi ndiye, 'na 'Muda umekaribia'. Msiwafuate.
9 Mkisikia vita na vuruguvurugu msiogope, kwa sababu haya mambo lazima yatokee kwanza, lakini mwisho hautatokea upesi.”
10 Kisha akawaambia, “Taifa litainuka kupigana na taifa jingine, na ufalme juu ya ufalme mwingine.
11 Kutakuwa na matetemeko makubwa, na njaa na tauni katika maeneo mbalimbali. Kutakuwa na matukio ya kutisha na ishara za kutisha kutoka mbinguni.
12 Lakini kabla ya mambo haya yote, wataweka mikono yao juu yenu na kuwatesa, kuwapeleka kwenye masinagogi na magereza, kuwaleta mbele za wafalme na wenye mamlaka kwa sababu ya jina langu.
13 Hii itawafungulia fursa kwa ushuhuda wenu.
14 Kwahiyo amueni mioyoni mwenu kutoandaa utetezi wenu mapema,
15 kwa sababu nitawapa maneno na hekima, ambayo adui zenu wote hawataweza kuipinga au kuikana.
16 Lakini mtakataliwa pia na wazazi wenu, ndugu zenu, jamaa zenu na rafiki zenu, na watawaua baadhi yenu.
17 Mtachukiwa na kila mmoja kwa sababu ya jina langu.
18 Lakini hakuna hata unywele mmoja wa vichwa vyenu utakaopotea.
19 Katika kuvumilia mtaziponya nafsi zenu.
20 Mtakapoona Yerusalemu imezungukwa na majeshi, basi jueni kwamba uharibifu wake umekaribia.
21 Hapo wale walioko Yudea wakimbilie milimani, na wale walioko katikati ya jiji waondoke, na msiwaache walioko vijijini kuingia.
22 Maana hizi ni siku za kisasi, ili kwamba mambo yote yaliyoandikwa yapate kutimilika.
23 Ole ni kwa wale walio na mimba na kwa wale wanyonyeshao katika siku hizo! Kwa maana kutakuwa na adha kuu juu ya nchi, na ghadhabu kwa watu hawa.
24 Na wataanguka kwa ncha ya upanga na watachukuliwa mateka kwa mataifa yote, na Yerusalem itakanyagwa na watu wa mataifa, mpaka wakati wa watu wa mataifa utakapotimilika.
25 Kutakuwa na ishara katika jua, mwezi na nyota. Na katika nchi kutakuwa na dhiki ya mataifa, katika kukata tamaa kutokana na mlio wa bahari na mawimbi.
26 Kutakuwa na watu wakizimia kwa hofu na katika kutarajia mambo yatakoyo tokea juu ya dunia. Kwa maana nguvu za mbingu zitatikiswa.
27 Kisha watamwona Mwana wa Adamu akija mawinguni katika nguvu na utukufu mkuu.
28 Lakini mambo haya yatakapoanza kutokea, simameni, inueni vichwa vyenu, kwa sababu ukombozi wenu umesogea karibu.”
29 Yesu akawaambia kwa mfano, “Uangalieni mtini, na miti yote.
30 Inapotoa machipukizi, mnajionea wenyewe na kutambua kwamba kiangazi tayari kiko karibu.
31 Vivyo hivyo, mnapoona mambo haya yanatokea, ninyi tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu umekaribia.
32 Kweli, nawaambieni, kizazi hiki hakitapita, mpaka mambo haya yote yatakapotokea.
33 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
34 Lakini jiangalieni wenyewe, ili kwamba mioyo yenu isije ikalemewa na ufisadi, ulevi, na mahangaiko ya maisha haya. Kwa sababu ile siku itawajia ghafla
35 kama mtego. Kwasababu itakuwa juu ya kila mmoja aishiye katika uso wa dunia nzima.
36 Lakini mwe tayari wakati wote, mwombe kwamba mtakuwa imara vya kutosha kuyaepuka haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu.”
37 Hivyo wakati wa mchana alikuwa akifundisha hekaluni na usiku alitoka nje, na kwenda kukesha katika mlima unaoitwa wa Mzeituni.
38 Watu wote walimjia asubuhi na mapemaili kumsikiliza ndani ya hekalu.