< Luka 11 >
1 Ilitokea wakati Yesu alipokuwa anaomba mahali fulani, mmoja wa mwanafunzi wake alimwambia, “Bwana, tufundishe sisi kuomba kama Yohana alivyo wafundisha wanafunzi wake'.
Siku moja, Yesu alikuwa mahali fulani akiomba. Alipomaliza kuomba, mmoja wa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana, tufundishe kuomba, kama vile Yohana alivyowafundisha wanafunzi wake.”
2 Yesu akawaambia, Msalipo, semeni, 'Baba, Jina lako litakazwe. Ufalme wako uje.
Akawaambia, “Mnapoomba, semeni: “‘Baba yetu (uliye mbinguni), jina lako litukuzwe, ufalme wako uje. (Mapenzi yako yafanyike hapa duniani kama huko mbinguni.)
3 Utupe mkate wetu wa kila siku.
Utupatie kila siku riziki yetu.
4 Utusamehe makosa yetu, kama nasi tunavyowasamehe wote waliotukosea. Usituongoze katika majaribu.”
Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa na sisi huwasamehe wote wanaotukosea. Wala usitutie majaribuni (bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu).’”
5 Yesu akawaambia, “Ni nani kwenu atakuwa na rafiki, ambaye atamuendea usiku, na kumwambia, Rafiki niazime mikate mitatu.
Kisha akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu mwenye rafiki yake, naye akamwendea usiku wa manane na kumwambia, ‘Rafiki, nikopeshe mikate mitatu.
6 Kwa sababu rafiki yangu amenijia sasa hivi kutoka safarini, nami sina cha kumuandalia.'
Kwa sababu rafiki yangu amekuja kutoka safarini, nami sina kitu cha kumpa.’
7 Na yule aliyeko ndani akamjibu, usinitaabishe, Mlango umekwisha kufungwa, na watoto wangu, pamoja nami tumekwisha kulala kitandani. Siwezi kuamka na kukupa wewe mikate.
“Kisha yule aliyeko ndani amjibu, ‘Usinisumbue. Mlango umefungwa, nami na watoto wangu tumelala. Siwezi kuamka nikupe chochote.’
8 Nawaambia, japo kuwa haamki na kukupatia mikate kama rafiki yake, kwa sababu ya kuendelea kumgongea bila aibu, ataamka na kukupatia vipande vingi vya mikate kulingana na mahitaji yako.
Nawaambia, ingawa huyo mtu hataamka na kumpa hiyo mikate kwa sababu ni rafiki yake, lakini kwa sababu ya kuendelea kwake kuomba, ataamka na kumpa kiasi anachohitaji.
9 Nami pia nawaambieni, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata, pigeni hodi nanyi mtafunguliwa.
“Kwa hiyo nawaambia: Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni nanyi mtafunguliwa mlango.
10 Kwa kuwa kila mtu aombaye atapokea, na kila mtu atafutaye atapata, na kila mtu apigaye hodi, mlango utafunguliwa kwake.
Kwa kuwa kila aombaye hupewa; naye kila atafutaye hupata; na kila abishaye hufunguliwa mlango.
11 Ni baba yupi miongoni mwenu, mwanaye akimuomba samaki atampa nyoka badala yake?
“Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba samaki, atampa nyoka badala yake?
12 Au akimuomba yai atampa nge badala yake?
Au mtoto akimwomba yai atampa nge?
13 Kwa hiyo, ikiwa ninyi mlio waovu mnajuwa kuwapa watoto wenu zawadi nzuri, je si zaidi sana Baba yenu wa mbinguni kwamba atawapa Roho Mtakatifu hao wamuombao?”
Basi ikiwa ninyi mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa Roho Mtakatifu wale wamwombao!”
14 Baadaye, Yesu akawa anakemea pepo, na mtu mwenye pepo alikuwa bubu. Ikawa pepo lilipomtoka, mtu huyo aliweza kuongea. Umati wakastaajabu sana.
Basi Yesu alikuwa anamtoa pepo mchafu kutoka kwa mtu aliyekuwa bubu. Yule pepo mchafu alipomtoka yule mtu aliyekuwa bubu, akaanza kuongea, nao umati wa watu ukashangaa.
15 Lakii watu wengine wakasema, huyu anaondo mapepo kwa Beelzebul, mkuu wa mapepo
Lakini wengine wakasema, “Anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli, yule mkuu wa pepo wachafu wote.”
16 Wengine walimjaribu na kumtaka awaonyeshe ishara kutoka mbinguni.
Wengine ili kumjaribu wakataka awaonyeshe ishara kutoka mbinguni.
17 Lakini Yesu aliyatambua mawazo yao na kuwaambia, “Kila ufalme utakaogawanyika itakuwa ukiwa, na nyumba iliyo gawanyika itaanguka.
Yesu akajua mawazo yao, naye akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia. Nayo nyumba iliyogawanyika dhidi yake yenyewe itaanguka.
18 Kama Shetani atakuwa amegawanyika, ufalme wake utasimamaje? Kwa sababu mwasema natoa mapepo kwa Belzebuli
Kama Shetani amegawanyika mwenyewe, ufalme wake utasimamaje? Nawaambia haya kwa sababu ninyi mnadai ya kuwa mimi ninatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli.
19 Kama mimi natoa mapepo kwa Belzebuli, je wenzenu wanatoa mapepo kwa njia gani? Kwa sababu hii, wao watawahukumu ninyi.
Kama mimi natoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, wafuasi wenu nao je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao ndio watakaowahukumu.
20 Lakini, kama natoa mapepo kwa kidole cha Mungu, basi uflame wa Mungu umewajia.
Lakini kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa kidole cha Mungu, basi Ufalme wa Mungu umewajia.
21 Mtu mwenye nguvu aliye na silaha akilinda nyumba yake, vitu vyake vitakaa salama.
“Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha anapoilinda nyumba yake, mali yake iko salama.
22 Lakini akivamiwa na mtu mwenye nguvu zaidi, Yule mtu mwenye nguvu atamnyang'anya silaha zake, na kuzichukua mali zake zote.
Lakini mtu mwenye nguvu zaidi kumliko akimshambulia na kumshinda, yeye humnyangʼanya silaha zake zote alizozitegemea, na kuchukua nyara.
23 Yeye asiye pamoja nami yuko kinyume nami, na yeye asiyekusanya pamoja nami hutapanya.
“Mtu asiyekuwa pamoja nami yu kinyume nami, na mtu ambaye hakusanyi pamoja nami, hutawanya.
24 Pepo mchafu amtokapo mtu, huenda na kutafuta mahali pasipo na maji ili ajipumzishe. Atakapokuwa amekosa, husema, 'nitarudi nilipotoka.
“Pepo mchafu amtokapo mtu, hutangatanga katika sehemu zisizo na maji akitafuta mahali pa kupumzika, lakini hapati. Ndipo husema, ‘Nitarudi kwenye nyumba yangu nilikotoka.’
25 Akirudi na kukuta nyumba imefagiliwa na imekaa vizuri.
Naye arudipo na kuikuta ile nyumba imefagiliwa na kupangwa vizuri,
26 Hivyo huenda na kutafuta mapepo saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe na kuwaleta waje wakae mahali pale. Na hali ya mtu huyo huwa mbaya kuliko ilivyokuwa mara ya kwanza.”
ndipo huenda na kuchukua pepo wachafu wengine saba wabaya kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo. Nayo hali ya mwisho ya yule mtu huwa ni mbaya kuliko ile ya kwanza.”
27 Ilitokea kwamba alipokuwa akisema maneno hayo, mwanamke fulani alipasa sauti yake zaidi ya wote kwanye mkutano wa watu na kusema “Limebarikiwa tumbo lililo kuzaa na matiti uliyoyanyonya”
Ikawa Yesu alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katikati ya ule umati wa watu akapaza sauti akasema, “Limebarikiwa tumbo lililokuzaa na matiti uliyonyonya!”
28 Lakini yeye akasema, wamebarikiwa wale wasikio neno la Mungu na kulitunza.
Yesu akajibu, “Wamebarikiwa zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulitii.”
29 Wakati umati wa watu wanakusanyika na kuongezeka, Yesu akaanza kusema “Kizazi hiki ni kizazi cha uovu. Hutafuta ishara, na hakuna ishara watayopewa zaidi ya ile ishara ya Yona.
Umati wa watu ulipokuwa unazidi kuongezeka, Yesu akaendelea kusema, “Hiki ni kizazi kiovu. Kinatafuta ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ya Yona.
30 Maana kama Yona alivyokuwa ishara kwa watu wa Ninawi, ndivyo na Mwana wa Adamu atakavyokuwa ishara kwa kizazi hiki
Kwa maana kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa watu wa Ninawi, ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa ishara kwa kizazi hiki.
31 Malkia wa Kusini atasimama siku ya hukumu na watu wa kizazi hiki na kuwahukumu wao, kwani yeye alitoka katika mwisho wa nchi ili aje asikilize hekima za Solomoni, na hapa yuko aliye mkuu kuliko Solomoni.
Malkia wa Kusini atasimama wakati wa hukumu na kuwahukumu watu wa kizazi hiki. Kwa kuwa yeye alikuja kutoka miisho ya dunia ili kuisikiliza hekima ya Solomoni. Na hapa yupo aliye mkuu kuliko Solomoni.
32 Watu wa Ninawi watasimama katika hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki siku ya hukumu watakihukumu, kwani wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na tazama, hapa yuko aliye mkuu kuliko Yona.
Siku ya hukumu, watu wa Ninawi watasimama pamoja na kizazi hiki na kukihukumu; kwa maana wao walitubu waliposikia mahubiri ya Yona. Na tazama, hapa yupo yeye aliye mkuu kuliko Yona.
33 Hakuna Mtu yeyote, awashaye taa na kuiweka sehemu ya chini yenye giza isiyoonekana au chini ya kikapu, ila huwasha na kuweka juu ya kitu ili kila mtu aingiaye aweze kuona mwanga.
“Hakuna mtu yeyote awashaye taa na kuiweka mahali palipofichika au kuifunikia chini ya bakuli. Badala yake huiweka juu ya kinara chake, ili watu wote wanaoingia waone nuru.
34 Jicho lako ni taa ya mwili. Jicho lako likiwa zuri basi mwili wako wote utakuwa kwenye mwanga. Lakini jicho lako likiwa baya basi mwili wako wote utakuwa kwenye giza.
Jicho lako ni taa ya mwili wako. Kama jicho lako ni zima, mwili wako wote pia umejaa nuru. Lakini kama jicho ni bovu, mwili wako wote pia umejaa giza.
35 Kwa hiyo, mjihadhari ili mwanga ulio ndani yenu usitiwe giza.
Kwa hiyo, hakikisha kwamba nuru iliyoko ndani yako isiwe giza.
36 Hivyo basi, kama mwili wako wote uko kwenye mwanga, na hakuna sehemu iliyo katika giza, basi mwili wako utakuwa sawa na taa iwakayo na kutoa mwanga kwenu.”
Basi ikiwa mwili wako wote umejaa nuru, bila sehemu yake yoyote kuwa gizani, basi utakuwa na nuru kama vile taa ikuangazavyo kwa nuru yake.”
37 Alipomaliza kuongea, Farisayo alimwalika akale chakula nyumbani kwake, naye Yesu akaingia ndani na kuwa pamoja nao.
Yesu alipomaliza kuzungumza, Farisayo mmoja alimwalika nyumbani mwake kwa chakula. Yesu akaingia na kuketi katika sehemu yake mezani.
38 Na Mafarisayo wakashangaa kwa jinsi ambavyo hakunawa kwanza kabla ya chakula cha jioni.
Yule Farisayo akashangaa kwamba Yesu hakunawa kwanza kabla ya kula.
39 Lakini Bwana akawaambia, “Ninyi Mafarisayo mnaosha nje ya vikombe na bakuli, lakini ndani yenu mmejaa tamaa na uovu.
Ndipo Bwana akamwambia, “Sasa, enyi Mafarisayo, mnasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa unyangʼanyi na uovu.
40 Ninyi watu msio na ufahamu, Je yeye aliyeumba nje hakuumba na ndani pia?
Enyi wapumbavu! Hamjui kuwa yeye aliyetengeneza nje ndiye alitengeneza na ndani pia?
41 Wapeni masikini yaliyo ndani, na mambo yote yatakuwa safi kwenu.
Basi toeni sadaka ya vile mlivyo navyo, na tazama, vitu vyote vitakuwa safi kwenu.
42 Lakini ole wenu Mafarisayo, kwani mnatoa zaka ya mnanaa na mchicha na kila aina ya mboga ya bustani. Lakini mmeacha mambo ya haki na kumpenda Mungu. Ni muhimu zaidi kufanya yaliyo ya haki na kumpenda Mungu, bila kuacha kufanya na hayo mengine pia.
“Lakini ole wenu, Mafarisayo, kwa maana mnampa Mungu zaka za mnanaa, mchicha na kila aina ya mboga, lakini mnapuuza haki na upendo wa Mungu. Iliwapasa kufanya haya ya pili bila kupuuza hayo ya kwanza.
43 Ole wenu Mafarisayo, kwa kuwa mnapenda kukaa katika viti vya mbele kwenye masinagogi na kuamkiwa kwa salamu za heshima sokoni.
“Ole wenu Mafarisayo, kwa sababu ninyi mnapenda kukalia viti vya mbele katika masinagogi, na kusalimiwa kwa heshima masokoni.
44 Ole wenu, kwani mnafanana na makaburi yasiyo na alama ambayo watu hutembea juu yake pasipokujua.”
“Ole wenu, kwa sababu ninyi ni kama makaburi yasiyokuwa na alama, ambayo watu huyakanyaga pasipo kujua.”
45 Mwalimu mmoja wa sheria za Kiyahudi akamjibu na kumwambia, “Mwalimu, unachokisema kinatuudhi pia sisi.”
Mtaalamu mmoja wa sheria akamjibu, akasema, “Mwalimu, unaposema mambo haya, unatutukana na sisi pia.”
46 Yesu akasema, “Ole wenu, waalimu wa sheria! kwani mnawapa watu mizigo mikubwa wasiyoweza kuibeba, walakini ninyi hamgusi mizigo hiyo hata kwa moja ya vidole vyenu.
Yesu akamjibu, “Nanyi wataalamu wa sheria, ole wenu, kwa sababu mnawatwika watu mizigo mizito ambayo hawawezi kubeba, wala ninyi wenyewe hamwinui hata kidole kimoja kuwasaidia.
47 Ole wenu, kwa sababu mnajenga na kuweka kumbukumbu kwenye makaburi ya manabii' ambao waliuwawa na mababu zenu.
“Ole wenu, kwa sababu ninyi mnajenga makaburi ya manabii waliouawa na baba zenu.
48 Hivyo ninyi mwashuhudia na kukubaliana na kazi walizozifanya mababu zenu, kwa sababu hakika waliwauwa manabii ambao mnajenga kumbukumbu katika makaburi yao.
Hivyo ninyi mwashuhudia na mnathibitisha kile baba zenu walichofanya. Wao waliwaua manabii, nanyi mnawajengea makaburi.
49 Kwa sababu hiyo pia, hekima ya Mungu inasema, 'Nitawatumia manabii na mitume nao watawatesa na kuwaua baadhi yao.
Kwa sababu ya jambo hili, Mungu katika hekima yake alisema, ‘Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na wengine watawatesa.’
50 Kizazi hiki kitawajibika kwa damu ya manabii waliouawa tangu kuanza kwa dunia,
Kwa hiyo kizazi hiki kitawajibika kwa ajili ya damu ya manabii iliyomwagwa tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu,
51 Kutoka damu ya Abeli hadi damu ya Zakaria, aliyeuawa katikati ya madhabahu na patakatifu. Ndiyo, nawaambia ninyi, kizazi hiki kitawajibika.
tangu damu ya Abeli mpaka damu ya Zekaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na mahali patakatifu. Naam, nawaambia, kizazi hiki kitawajibika kwa haya yote.
52 Ole wenu waalimu wa sheria za Kiyahudi, kwa sababu mmechukua funguo za ufahamu; nyie wenyewe hamuingii, na wale wanaotaka kuingia mnawazuia.”
“Ole wenu ninyi wataalamu wa sheria, kwa sababu mmeuondoa ufunguo wa maarifa. Ninyi wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wanaingia mkawazuia.”
53 Baada ya Yesu kuondoka pale, Waandishi na Mafarisayo walimpinga na kubishana naye juu ya mambo mengi.
Yesu alipoondoka huko, walimu wa sheria na Mafarisayo wakaanza kumpinga vikali na kumsonga kwa maswali,
54 wakijaribu kumnsana kwa maneno yake.
wakivizia kumkamata kwa kitu atakachosema ili wamshtaki.