< Mambo ya Walawi 27 >

1 Yahweh akazungumza na Musa na akasema,
Bwana akamwambia Mose,
2 “Zungumza na watu wa Israeli na uwaambie, 'Iwapo mtu yeyote anatoa kiapo maalum cha kuwa mnathiri kwa Yahweh, tumieni tathmini zifuatazo:
“Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Kama mtu yeyote ataweka nadhiri maalum ili kuweka watu wakfu kwa Bwana, kwa kutoa kiasi cha thamani inayolingana,
3 Viwango vyenu vya thamani kwa mwanaume aliye na umri kati ya miaka ishirini na miaka sitini yaweza kuwa shekeli hamsini za fedha, kulingana na vipimo vya shekeli ya mahali pa patakatifu.
thamani ya kukomboa mwanaume mwenye kati ya umri wa miaka ishirini na miaka sitini itakuwa shekeli hamsini za fedha, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu;
4 Kwa mwanamke wa umri uleule viwango vyenu vya thamani yapasa viwe shekeli thelathini vya fedha.
ikiwa ni mwanamke, weka thamani yake kwa shekeli thelathini.
5 Tangu wenye umri wa miaka mitano mpaka wa miaka ishirini viwango vyenu vya thamani kwa mwananume vitakuwa shekeli ishirini za fedha, na kwa mwanamke ni shekeli kumi za fedha,
Kama ni mtu mwenye umri wa miaka kati ya mitano na ishirini, weka thamani ya mwanaume kuwa shekeli ishirini, na mwanamke shekeli kumi.
6 Kwa wenye umri wa tangu mwezi mmoja mpaka miaka mitano viwango vyenu vya thamani kwa mawanaume vitakuwa shekeli tano za fedha na kwa mwanamke shekeli tatu za fedha.
Kama ni mtu mwenye umri kati ya mwezi mmoja na miaka mitano, weka thamani ya mwanaume kuwa shekeli tano za fedha, na ile ya mwanamke kuwa shekeli tatu za fedha.
7 Tangu wenye umri wa miaka sitini na zaidi kwa mwanaume viwango vyenu vya thamani vitakuwa shekeli kumi na tano, na kwa mwanamke ni shekeli kumi.
Kama ni mtu mwenye miaka sitini na zaidi, weka thamani ya mwanaume kuwa shekeli kumi na tano, na mwanamke shekeli kumi.
8 Lakini kama mtu atoaye kiapo cha mnadhiri hawezi kulipa kiwango hicho cha thamani, kisha huyo mtu anayetolewa lazima atapelekwa kwa kuhani, naye kuhani atamthamanisha huyo atolewaye kwa kiasi anachoweza kutoa yule anayetoa kiapo cha mnadhiri.
Kama mtu yeyote anayeweka nadhiri ni maskini mno kuweza kulipa kiasi kilichowekwa, atampeleka huyo mtu kwa kuhani, ambaye ataweka thamani yake kulingana na kile mweka nadhiri anachoweza kulipa.
9 Iwapo mtu anataka kutoa sadaka ya mnyama kwa Yahweh, na iwapo Yahweh ataikubali, kisha huyo mnyama atatengwa kwake.
“‘Kama kile mtu alichokiwekea nadhiri ni mnyama anayekubalika kama sadaka kwa Bwana, mnyama wa namna hiyo aliyetolewa kwa Bwana anakuwa mtakatifu.
10 Mtu huyo hataruhusiwa kumtoa madhabahuni au kumbadilisha huyo mnyama, mzuri kwa mbaya au mbaya kwa mzuri. endapo atatoa mnyama badala ya mwingine, kisha wanyama hao wawili; yule anayetolewa na yule anayebadilishwa wanakuwa watakatifu.
Mtu haruhusiwi kumbadilisha au kutoa mnyama mzuri kwa mbaya, au mnyama mbaya kwa mzuri. Kama atatoa mnyama badala ya mwingine, wanyama wote wawili, yaani yule aliyetolewa na yule aliyebadiliwa, ni watakatifu.
11 Hata hivyo, iwapo kile mtu amishaapa kumtolea Yahweh kwa uhalisia siyo kisafi, kwa hiyo, Yahweh hatakikubali, naye huyo mtu atalazimika kumleta huyo mnyama kwa kuhani.
Kama alichokiwekea nadhiri ni mnyama aliye najisi kiibada, yaani yule asiye kubalika kuwa sadaka kwa Bwana, huyo mnyama lazima aletwe kwa kuhani,
12 Kuhani atamthamanisha, kwa thamani ya soko la mnyama. Thamani yoyote kuhani atakayoiweka juu ya mnyama, hiyo ndiyo itakuwa thamani yake.
ambaye ataamua ubora wa mnyama huyo, kama ni mzuri au mbaya. Thamani yoyote atakayoweka kuhani, hivyo ndivyo itakavyokuwa.
13 Na kama mmiliki anapenda kumkomboa, kisha tano ya thamani yake itaongezwa kwenye gharama yake ya ukombozi.
Kama mwenye mnyama atapenda kumkomboa mnyama huyo, lazima aongeze sehemu ya tano ya thamani yake.
14 Mtu aitengapo nyumba yake iwe zawadi takatifu kwa Yahweh, kisha kuhani ataweka thamani yake ama iwe ni nzuri au mbaya. Thamani yoyote itakayowekwa na kuhani juu yake, ndiyo itakuwa thamani yake.
“‘Kama mtu ataweka nyumba yake wakfu kama kitu kitakatifu kwa Bwana, kuhani ataamua ubora wa nyumba hiyo, kama ni nzuri au mbaya. Thamani yoyote kuhani atakayoweka, basi hivyo ndivyo itakavyokuwa.
15 Lakini kama mmiliki wake anayeitenga nyumba yake anapenda kuikomboa, atalazimika kuongeza sehemu ya tano ya thamani yake kwenye gharama ya ukombozi wake, nayo nyumba itakuwa yake.
Kama mtu aliyeweka nyumba yake wakfu ataikomboa, lazima aongeze sehemu ya tano ya thamani yake, nayo nyumba itakuwa yake tena.
16 Iwapo mtu anatenga sehemu ya ardhi yake mwenye, kisha tathmini yake itakuwa katika uwiano kwa kiwango cha kiasi cha mbegu inayotakiwa kuipanda katika ardhi hiyo—homeri moja ya mbegu za shairi ambayo itathamanishwa kwa shekeli hamsini za fedha.
“‘Kama mtu anaweka sehemu ya ardhi ya jamaa yake wakfu kwa Bwana, thamani yake itawekwa kulingana na kiasi cha mbegu inayohitajiwa kupandwa katika ardhi hiyo, yaani homeri moja ya mbegu za shayiri kwa shekeli hamsini za fedha.
17 Na kama analitenga shamba lake katika mwaka wa Yubile, tathmini yake ya awali itabaki kuwa ileile.
Kama akiweka shamba lake wakfu katika Mwaka wa Yubile, ile thamani iliyokwisha wekwa itakuwa iyo hiyo.
18 Lakini endapo atalitenga shamba hilo baada ya mwaka wa Yubile, kisha kuhani atalazimika kukokotoa thamani yake kwa idadi ya miaka inayobaki mpaka mwaka wa Yubile, na thamani yake lazima ishushwe.
Lakini kama akiweka shamba lake wakfu baada ya Yubile, kuhani ataweka thamani kulingana na idadi ya miaka iliyobaki kufikia Mwaka wa Yubile unaofuata, na thamani yake iliyoamuliwa itapunguzwa.
19 Iwapo mtu anayelitenga shamba lake anapenda kuliko, mboa, naye atalazimika kuongeza sehemu ya tano kwenye thamani, nalo shamba litakuwa lake tena.
Kama mtu anayeweka wakfu shamba anataka kulikomboa, lazima aongeze sehemu ya tano ya thamani yake, nalo shamba litakuwa lake tena.
20 Iwapo halikomboi shamba, au iwapo amishaliuza shamba kwa mtu mwingine, haliwezi kukombolewa tena.
Kama pengine halikomboi shamba hilo, au kama ameliuza kwa mtu mwingine, kamwe haliwezi kukombolewa.
21 Badala yake, shamba hilo litakapoachwa huru katika mwaka wa Yubile, litakuwa zawadi takatifu kwa Yahweh, kama lilivyo shamba lililotolewa kabisa kwa Yahweh. Nalo litakuwa mali ya kuhani.
Shamba hilo litakapoachiwa mwaka wa Yubile, litakuwa takatifu, kama shamba lililotolewa kwa Bwana, nalo litakuwa mali ya makuhani.
22 Iwapo mtu anatenga shamba alilolinunua, lakini hilo shamba siyo sehemu ya ardhi ya familia yake,
“‘Kama mtu ameweka wakfu kwa Bwana shamba alilonunua, ambalo si sehemu ya ardhi ya jamaa yake,
23 kuhani atafanya tathmini yake mpaka mwaka wa Yubile, na mtu huyo lazima atalipa thamani yake katika siku hiyo hiyo kuwa zawadi takatifu kwa Yahweh.
kuhani ataamua thamani yake hadi Mwaka wa Yubile, naye huyo mtu atalazimika kulipa thamani yake siku hiyo kama kitu kitakatifu kwa Bwana.
24 Katika mwaka wa Yubile, shamba litarejeshwa kwa mtu yule ambaye lilikuwa limenunuliwa, kwa mmiliki wa ardhi.
Katika Mwaka wa Yubile, shamba litarudishwa kwa mtu yule ambaye lilinunuliwa kutoka kwake, yule ambaye ardhi ilikuwa mali yake.
25 Tathmani yote lazima ifanywe kwa uzani wa shekeli ya mahali pa patakatifu. Gera ishirini kwa shekeli moja.
Kila thamani lazima iwekwe kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, gera ishirini kwa shekeli.
26 Asiwepo mtu atakayetenga mzaliwa wa kwanza miongoni mwa wanyama, kwa kuwa wazaliwa wote wa kwanza wa wanyama tayari ni mali ya Yahweh; iwe ni maksai au kondoo, ni wa Yahweh.
“‘Lakini hakuna mtu atakayeweka wakfu mzaliwa wa kwanza wa mnyama, kwa kuwa mzaliwa wa kwanza tayari ni mali ya Bwana; awe ngʼombe au kondoo, ni wa Bwana.
27 Na kama ni mnyama aliye najisi, kisha mmiliki wake anaweza kumnunua tena sawasawa na thamani yake, na sehemu ya tano lazima itaongezwa kwenye thamani hiyo. Na kama mnyama hakombolewi, naye atauzwa kwa thamani iliyowekwa.
Kama ni mmoja wa wanyama walio najisi, aweza kumnunua kwa bei iliyowekwa, akiongeza sehemu ya tano ya thamani yake. Kama hatamkomboa, mnyama huyo atauzwa kwa bei iliyowekwa.
28 Hakutakuwa na kitu amabacho mtu anakitoa kwa Yahweh, kutoka katika vyote alivyonavyo, iwe ni mwanadamu au mnyama, au ardhi ya familia yake, ambacho chaweza kuuzwa au kukombolewa. Kila kitu kitolewacho ni kitakatifu sana kwa Yahweh.
“‘Lakini chochote kile mtu alicho nacho na akakiweka wakfu kwa Bwana, iwe ni binadamu, au mnyama, au ardhi ya jamaa, hakiwezi kuuzwa au kukombolewa. Chochote kilichowekwa wakfu ni kitakatifu sana kwa Bwana.
29 Hakuna fidia inayoweza kulipwa kwa ajili ya mtu aliyetolewa ili kuangamizwa. Mtu huyo sharti auawe
“‘Mtu yeyote aliyewekwa wakfu ili kuangamizwa, hawezi kukombolewa. Mtu kama huyo lazima auawe.
30 Zaka yote iliyo ya ardhini, iwe nafaka ichipukayo juu ya ardhi au tunda kutoka kwenye miti, ni mali ya Yahweh. Ni takatifu kwa Yahweh.
“‘Zaka ya kila kitu kutoka shambani, iwe ni nafaka kutoka kwa ardhi, au tunda kutoka kwa miti, ni mali ya Bwana; ni takatifu kwa Bwana.
31 Iwapo mtu anakomboa chochote cha zaka yake, atalazimika kuongeza sehemu ya tano kwenye thamani yake.
Kama mtu akikomboa chochote cha zaka yake, lazima aongeze sehemu ya tano ya thamani yake.
32 Na kwa kila mnyama wa kumi wa kundi la ng'ombe au la kondoo, yeyote anayepita chini ya fimbo ya mchungaji, atatengwa kwa ajili ya Yahweh.
Zaka yote ya kundi la ngʼombe au la kondoo na mbuzi, kila mnyama wa kumi apitaye chini ya fimbo ya yule awachungaye, atakuwa mtakatifu kwa Bwana.
33 Mchungaji hatatafuta wanyma waliobora au wabaya kabisa, na haruhusiwi kubadili mnyama mmoja kwa mnyama mwingine. Iwapo anambadilisha kwa namna yoyote ile, kisha wote wawili yule wa kwanza na huyo aliyebadiliwa watakuwa watakatifu. Mnyama huyo atolewaye hawezi kukombolewa.'”
Yule mnyama wa kumi hatachaguliwa kwa kigezo cha uzuri au ubaya, naye haruhusiwi kubadiliwa. Ikiwa atabadiliwa, basi mnyama yule wa kwanza na huyo aliyebadiliwa wote watahesabiwa kuwa watakatifu, na haiwezekani kuwakomboa.’”
34 Hizi ndizo amri ambazo Yahweh alimpa Musa kwenye mlima Sinai kwa ajili ya watu wa Israeli.
Haya ndiyo maagizo Bwana aliyompa Mose juu ya Mlima Sinai kwa ajili ya Waisraeli.

< Mambo ya Walawi 27 >