< Mambo ya Walawi 21 >

1 Yahweh akamwambia Musa, “Zungumza na makuhani, wana wa Aroni, nawe waambie, 'hakuna hata mmoja miongoni mwenu atakayejitia unajisi kwa wale wanaokufa miongoni mwa watu wake,
Bwana akamwambia Mose, “Sema na makuhani, wana wa Aroni, uwaambie: ‘Kamwe kuhani asijitie unajisi kwa utaratibu wa kiibada kwa ajili ya mtu wake yeyote anayekufa,
2 isipokuwa yule aliye ndugu wa karibu—mama yake, baba yake, mwanawe, bintiye, nduguye,
isipokuwa jamaa wake wa karibu, kama vile mama yake au baba yake, mwanawe au binti yake, ndugu yake,
3 au dada yake bikira anayemtegemea, kwa kuwa hana mume—kwake huyo anaweza kujitia unajisi.
au dada yake asiyeolewa ambaye anamtegemea kwa kuwa hana mume, kwa ajili ya hao aweza kujitia unajisi.
4 Lakini hatajitia unajisi na kujichafu kwa ajili ya jamaa wengine.
Kamwe asijitie unajisi mwenyewe kutokana na wale watu ambao anahusiana nao kwa kuoana, na hivyo kujitia unajisi.
5 Makuhanai hawatanyoa vichwa vyo wala kunyoa pembeni mwa ndevu zao, wala hawatachanja chale miili yao.
“‘Kamwe makuhani wasinyoe nywele za vichwa vyao wala wasinyoe pembeni mwa ndevu zao, au kuweka chale kwenye miili yao.
6 Watakuwa watakatifu kwa Mungu wao, wala hawataliaibisha jina la Mungu wao, kwa sababu makuhani hutoa sadaka ya Yahweh ya chakula, mkate wa Mungu wao. Kwa hiyo makuhani lazima wawe watakatifu.
Lazima wawe watakatifu kwa Mungu wao, na kamwe wasilinajisi jina la Mungu wao. Kwa sababu ndio wanaotoa sadaka za kuteketezwa kwa moto kwa Bwana, chakula cha Mungu wao, hivyo lazima wawe watakatifu.
7 Hawataoa mwanamke aliye kahaba na aliyetiwa unajisi, na hawataoa mwanamke aliyetalikiwa kutoka kwa mume wake kwa sababu wametengwa kwa ajili ya Mungu wao.
“‘Kamwe wasioe wanawake waliojinajisi kwa ukahaba, au waliopewa talaka na waume wao, kwa sababu makuhani ni watakatifu kwa Mungu wao.
8 Utamtenga kwa sababu yeye ndiye anayetoa mkate kwa Mungu wako. Ni lazima awe mtakatifu, kwa sababu—Mimi, Yahweh, ndimi niwatakasaye nyinyi—pia Mimi mwenyewe ni mtakatifu.
Waoneni kuwa watakatifu, kwa sababu ndio wanaotoa chakula cha Mungu wenu. Kumbukeni kuwa ni watakatifu, kwa sababu Mimi Bwana ni mtakatifu, Mimi niwafanyaye ninyi kuwa watakatifu.
9 Binti yeyote wa kuhani anayejitia unajisi kwa kujifanya kahaba anajifedhehesha mwenyewe. Ni lazima ateketezwe kwa moto.
“‘Ikiwa binti wa kuhani anajitia unajisi kwa kufanya ukahaba, anamwaibisha baba yake; lazima achomwe kwa moto.
10 Mtu ambaye ni kuhani mkuu miongoni mwa nduguze, ambaye mafuta ya upako yamekwisha kumiminwa kichwani pake, na ambaye amekwisha kuwekwa wakfu ili kuvaa mavazi maalum ya kuhani mkuu, kamwe hataziacha wazi nywele zake wala hatazirarua nguo zake.
“‘Kuhani mkuu, yule miongoni mwa ndugu zake ambaye amekwisha kutiwa mafuta kwa kumiminiwa juu ya kichwa chake, na ambaye amewekwa wakfu kuvaa mavazi ya ukuhani, kamwe asiache nywele zake bila kufunikwa, wala asirarue nguo zake.
11 Hataingia kamwe mahali popote ambapo kuna maiti na kujitia unajisi, hata kama ni maiti ya baba yake au ya mama yake.
Kamwe asiingie mahali palipo maiti ndani. Kamwe asijitie unajisi, hata kwa ajili ya baba yake au mama yake,
12 Kuhani mkuu hataondoka eneo takatifu la hema la kukutania au kupatia unajisi patakatifu pa Mungu wake, kwa sababu amewekwa wakfu kuwa kuhani mkuu kwa kutiwa mafuta ya upako ya Mungu wake. Mimi ndimi Yahweh.
wala asiondoke mahali patakatifu pa Mungu wake au kupanajisi, kwa sababu amewekwa wakfu kwa mafuta ya Mungu wake. Mimi ndimi Bwana.
13 Kuhani mkuu nilazima aoe bikira kuwa mke wake.
“‘Mwanamke kuhani atakayemwoa lazima awe bikira.
14 Hataoa mjene, mwanamke mtalaka au mwanamke aliye kahaba. Anaweza kuoa mwanamke bikira kutoka kwa watu wake,
Kamwe asimwoe mjane, au mwanamke aliyepewa talaka, wala mwanamke aliyejinajisi kwa ukahaba, bali atamwoa tu bikira kutoka miongoni mwa watu wake,
15 kwa hiyo asiwatia unajisi watoto wake miongoni mwa watu wake. kwa kuwa Mimi Yahweh, ndimi ninayemfanya yeye mtakatifu.”
na hivyo hatawatia unajisi watoto wake miongoni mwa watu wake. Mimi ndimi Bwana, nimfanyaye mtakatifu.’”
16 Yahweh akamwambia Musa, akasema,
Bwana akamwambia Mose,
17 Zungumza na Aroni na umwambie, 'mtu yeyote wa ukoo wako katika vizazi vyako vyote mwenye kasoro mwilini mwake, asisogee kutoa chakula kwa Mungu wake.
“Mwambie Aroni: ‘Kwa vizazi vijavyo, hakuna mzao wako mwenye dosari atakayekaribia kutoa chakula cha Mungu wake.
18 Mtu yeyote mwenye kasoro mwilini mwake asimkaribie Yahweh,
Hakuna mtu mwenye dosari yoyote awezaye kukaribia: hakuna mtu aliye kipofu au kiwete, au aliyeharibika uso au asiye na viungo kamili,
19 mtu kama vile: kipofu au mtu asiyeweza kutembea, mtu aliyeharibiwa uso au kupungukiwa na viungo mwilini, mtu aliye na mguu au mkono wenye ulemavu,
hakuna mtu mwenye mguu au mkono uliolemaa,
20 mtu mwenye kibiongo mgongoni mwake au aliye na kimo kidogo au wembamba usio wa kawaida, au mtu mwenye kasoro machoni mwake, au mwenye ugonjwa, kidonda, upele, au yule ambaye korodani zake zimeharibiwa.
au mwenye kibiongo au aliyedumaa, au aliye na tatizo la macho, au aliye na uvimbe wenye usaha au majipu, au aliyehasiwa.
21 Hakutakuwa na mtu miongoni mwa ukoo wa Aroni kuhani mkuu mwenye kasoro mwilini atakayekaribia kutoa matoleo yatakayoteketezwa kwa moto kwa ajili ya Yahweh. Mtu kama huyo mwenye kasoro mwilini hatakaribia ili kutoa mkate wa Mungu wake.
Hakuna mzao wa kuhani Aroni mwenye kilema chochote atakayekaribia kutoa sadaka kwa Bwana ya kuteketezwa kwa moto. Kama ana kilema, kamwe asikaribie kutoa chakula cha Mungu wake.
22 Anaweza kula chakula cha Mungu wake, ama iwe baadhi ya vile vilivyo vitakatifu sana au vile vitakatifu.
Anaweza kula chakula kitakatifu sana cha Mungu wake, pia hata chakula kitakatifu.
23 Hata hivyo, hataingia ndani ya pazia wala kuisogelea madhabahu, kwa sababu ana kasoro mwilini mwake, ili kwamba asipanajisi mahali patakatifu pangu, kwa kuwa Mimi ndimi Yahweh anayewafanya watakatifu.”
Lakini kwa sababu ya kilema chake, kamwe asikaribie karibu na pazia wala kukaribia madhabahu, asije akanajisi mahali patakatifu pangu. Mimi ndimi Bwana, niwafanyaye watakatifu.’”
24 Kwa hiyo Musa akamwambia maneno haya Aroni, wanawe, na watu wote wa Israeli.
Basi Mose akamwambia Aroni jambo hili na wanawe, pamoja na Waisraeli wote.

< Mambo ya Walawi 21 >