< Mambo ya Walawi 21 >
1 Yahweh akamwambia Musa, “Zungumza na makuhani, wana wa Aroni, nawe waambie, 'hakuna hata mmoja miongoni mwenu atakayejitia unajisi kwa wale wanaokufa miongoni mwa watu wake,
2 isipokuwa yule aliye ndugu wa karibu—mama yake, baba yake, mwanawe, bintiye, nduguye,
3 au dada yake bikira anayemtegemea, kwa kuwa hana mume—kwake huyo anaweza kujitia unajisi.
4 Lakini hatajitia unajisi na kujichafu kwa ajili ya jamaa wengine.
5 Makuhanai hawatanyoa vichwa vyo wala kunyoa pembeni mwa ndevu zao, wala hawatachanja chale miili yao.
6 Watakuwa watakatifu kwa Mungu wao, wala hawataliaibisha jina la Mungu wao, kwa sababu makuhani hutoa sadaka ya Yahweh ya chakula, mkate wa Mungu wao. Kwa hiyo makuhani lazima wawe watakatifu.
7 Hawataoa mwanamke aliye kahaba na aliyetiwa unajisi, na hawataoa mwanamke aliyetalikiwa kutoka kwa mume wake kwa sababu wametengwa kwa ajili ya Mungu wao.
8 Utamtenga kwa sababu yeye ndiye anayetoa mkate kwa Mungu wako. Ni lazima awe mtakatifu, kwa sababu—Mimi, Yahweh, ndimi niwatakasaye nyinyi—pia Mimi mwenyewe ni mtakatifu.
9 Binti yeyote wa kuhani anayejitia unajisi kwa kujifanya kahaba anajifedhehesha mwenyewe. Ni lazima ateketezwe kwa moto.
10 Mtu ambaye ni kuhani mkuu miongoni mwa nduguze, ambaye mafuta ya upako yamekwisha kumiminwa kichwani pake, na ambaye amekwisha kuwekwa wakfu ili kuvaa mavazi maalum ya kuhani mkuu, kamwe hataziacha wazi nywele zake wala hatazirarua nguo zake.
11 Hataingia kamwe mahali popote ambapo kuna maiti na kujitia unajisi, hata kama ni maiti ya baba yake au ya mama yake.
12 Kuhani mkuu hataondoka eneo takatifu la hema la kukutania au kupatia unajisi patakatifu pa Mungu wake, kwa sababu amewekwa wakfu kuwa kuhani mkuu kwa kutiwa mafuta ya upako ya Mungu wake. Mimi ndimi Yahweh.
13 Kuhani mkuu nilazima aoe bikira kuwa mke wake.
14 Hataoa mjene, mwanamke mtalaka au mwanamke aliye kahaba. Anaweza kuoa mwanamke bikira kutoka kwa watu wake,
15 kwa hiyo asiwatia unajisi watoto wake miongoni mwa watu wake. kwa kuwa Mimi Yahweh, ndimi ninayemfanya yeye mtakatifu.”
16 Yahweh akamwambia Musa, akasema,
17 Zungumza na Aroni na umwambie, 'mtu yeyote wa ukoo wako katika vizazi vyako vyote mwenye kasoro mwilini mwake, asisogee kutoa chakula kwa Mungu wake.
18 Mtu yeyote mwenye kasoro mwilini mwake asimkaribie Yahweh,
19 mtu kama vile: kipofu au mtu asiyeweza kutembea, mtu aliyeharibiwa uso au kupungukiwa na viungo mwilini, mtu aliye na mguu au mkono wenye ulemavu,
20 mtu mwenye kibiongo mgongoni mwake au aliye na kimo kidogo au wembamba usio wa kawaida, au mtu mwenye kasoro machoni mwake, au mwenye ugonjwa, kidonda, upele, au yule ambaye korodani zake zimeharibiwa.
21 Hakutakuwa na mtu miongoni mwa ukoo wa Aroni kuhani mkuu mwenye kasoro mwilini atakayekaribia kutoa matoleo yatakayoteketezwa kwa moto kwa ajili ya Yahweh. Mtu kama huyo mwenye kasoro mwilini hatakaribia ili kutoa mkate wa Mungu wake.
22 Anaweza kula chakula cha Mungu wake, ama iwe baadhi ya vile vilivyo vitakatifu sana au vile vitakatifu.
23 Hata hivyo, hataingia ndani ya pazia wala kuisogelea madhabahu, kwa sababu ana kasoro mwilini mwake, ili kwamba asipanajisi mahali patakatifu pangu, kwa kuwa Mimi ndimi Yahweh anayewafanya watakatifu.”
24 Kwa hiyo Musa akamwambia maneno haya Aroni, wanawe, na watu wote wa Israeli.