< Mambo ya Walawi 19 >
1 Yahweh akazungumza na Musa, akisema.
2 Zungumza na kusanyiko lote la watu wa Israeli na uwaambie, 'Ni lazima muwe watakatifu, kwa kuwa mimi Yahweh Mungu wenu ni mtakatifu.
3 Kila mtu amstahi mama yake na baba yake. Na ni lazima muzishike Sabato zangu. Mimi ndimi Yahweh Mungu wenu.
4 Msizigeukie sanamu zisizo na thamani, wala kujitengenezea wenyewe miungu kutokana na chuma. Mimi ndimi Yahweh Mungu wenu.
5 Unapotoa dhabihu za sadaka ya ushirika kwa Yahweh, utatoa ili kupata kibali.
6 Ni sharti iliwe siku hiyo hiyo uliyoitoa, au siku inayofuata.
7 Kama kinabaki kitu cho chote hata siku ya tatu ni lazima kiteketezwe kwa moto. Kama kitaliwa katika siku ya tatu kitakuwa najisi. Hakitakubalika,
8 lakini kila akilaye ni lazima atachukua hatia yake kwa sababu amekivunjia heshima kilicho kitakatifu kwa Yahweh. Mtu huyo ni lazima akatiliwe mbali na watu wake.
9 Unapovuna mavuno ya ardhi yako, usivune hata pembezo mwa shamba lako kabisa, wala hutakusanya mabaki ya mavuno yako yote.
10 Usikusanye kila zabibu kutoka katika mizabibu yako, wala usiziokote dhabibu zilizoanguka chini katika shamba la mizabibu. Ni lazima uziache kwa ajili ya masikini na kwa ajili ya wageni. Mimi ndimi Yahweh Mungu wako.
11 Usiibe. Usiseme uongo. Msidanganyane.
12 Usiape kwa jina langu kwa uongo na kulinajisi jina la Mungu wako. Mimi ndimi Yahweh
13 Usimgandamize jirani yako wala kumwibia. Usishikilie malipo ya kibarua usiku kucha hata asubuhi.
14 Usimlaani kiziwi au kuweka kikwazo mbele ya kipofu. Badala yake, yakupasa umwogope Mungu wako. Mimi ndimi Yahweh.
15 Usisababishe hukumu ikawa ya uongo. Usionyeshe upendeleo kwa mtu fulani eti kwa kuwa tu yeye ni masikini na usionyeshe upendeleo kwa mtu fulani eti kwa kuwa tu yeye ni mtu muhimu. Badala yake, amua juu ya jirani yako kwa haki.
16 Usiende huku na huko ukisema habari za uchochezi miongoni mwa watu wako, bali tafuta kuyalinda maisha ya jirani yako. Mimi ndimi Yahweh.
17 Usimchukie ndugu yako moyoni mwako. Mkemee jirani yako kwa heshima ili kwamba usishiriki katika dhambi kwa sababu yake.
18 Usijilipize kisasi au kuwa na chuki yoyote dhidi ya mtu yeyote wa watu wako, lakini badala yake mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe. Mimi ndimi Yahweh.
19 Shika amri zangu. Usiwazalishe wanyama wako kwa kutumia wanyama wa aina nyingine tofauti. Usichanganye aina mbili tofauti za mbegu unapopanda shamba lako. Usivae vazi lililofumwa kwa kutumia nyuzi za rangi mbili tofauti zilizochanganywa pamoja.
20 Yeyote anayelala na msichana mtumwa aliyeposwa na mume mwingine, lakini ambaye hajakombolewa au hajaachwa huru, lazima waadhibiwe. Hawatauawa kwa sababu yule msichana hakuwa huru.
21 Ni lazima mtu huyo alete sadaka yake ya hatia kwenye ingilio la hema la kukutania—kondoo dume iwe sadaka ya hatia.
22 Kisha kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa huyo kandoo dume mbele za Yahweh kutokana na dhambi aliyoitenda. Nayo dhambi iliyotendwa itasamehewa.
23 Mtakapoingia katika nchi na kupanda aina zote za miti kwa chakula, kisha mtayahesabu matunda yatakayozaliwa kuwa yamekatazwa kuliwa. Tunda litakatazwa kwako kwa miaka mitatu. Halitaliwa.
24 Lakini katika mwaka wa nne matunda yote yatakuwa matakatiifu, matoleo ya sifa kwa Yahweh.
25 Katika mwaka wa tano unaweza kula tunda, ambalo umelisubiri ili kwamba mti uweze kuzaa zaidi. Mimi ndimi Yahweh Mungu wako.
26 Usile nyama yoyote amabayo damu ingalimo ndani yake. Usiulize kwa roho juu ya wakati ujao,
27 Usitafute kuwadhibiti wengine kwa njia ya nguvu za kichawi. Msifuate tabia za kipagani kama vile kunyoa denge au kunyoa pembe za ndevu zeu.
28 Usiukate mwili wako kwa ajili ya wafu au kuchanja chale juu ya mwili wako. Mimi ndimi Yahweh.
29 Usimwaibishe binti yako kwa kumfanya kahaba, la sivyo taifa litaangukia kwenye ukahaba na nchi itajawa na uovu.
30 Utazitunza Sabato zangu na kupaheshimu mahali patakatifu pa hema langu la kukutania. Mimi ndimi Yahweh.
31 Msiwageukie wale wanaoongea na wafu au roho wachafu. msiwatafute, la sivyo watawanajisi ninyi, Mimi ndimi Yahweh Mungu wenu.
32 Ni lazima usimame mbele za mtu mwenye mvi na uheshimu uwepo wa mzee. Yakupasa umwegope Mungu wako. Mimi ndimi Yahweh.
33 Mgeni anapoishi miongoni mwenu katika nchi yanu, usimtendee lolote lililobaya.
34 Mgeni anayeishi pamoja nanyi ni lazima awe kama mwenyeji Mwisraeli mzaliwa anayeishi kwenu, na sharti umpende kama unavyojipenda wewe mwenyewe, ni kwa sababu wewe ulikuwa mgeni katika nchi ya Misri. Mimi ndimi Yahweh Mungu wako.
35 Unapopima urefu, uzito, au wingi usitumie vipimo vya udanganyifu.
36 Tumia mizani iliyo halali, mawe ya kupimia uzito yaliyo halali, efa halali, hini iliyo halali. Mimi ndimi Yahweh Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya utumwa ya Misri.
37 Utayatii maagizo yangu na sheria zangu zote na kuzitenda. Mimi ndimi Yahweh.