< Yoshua 9 >
1 Kisha wafalme wote walioishi ng'ambo ya mto Yordani katika nchi ya milima, na katika nchi za chini katika pwani za Bahari Kuu mbele ya Lebanoni - Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi -
2 hawa waliungana pamoja chini ya amri moja kuinua vita dhidi ya Yoshua na Israeli.
3 Waliposikia wenyeji wa Gibeoni juu ya mambo aliyoyafanya Yoshua katika Yeriko na Ai,
4 walipanga mpango wa udanganyifu. Walienda kama wajumbe. Walichukua magunia yaliyochakaa na kuyaweka juu ya punda. Walichukua pia viriba vilivyochakaa na kuchanika chanika na vilivyozibwa zibwa.
5 Walivaa miguuni mwao viatu vilivyozeeka na kutoboka toboka, na walivaa nguo kuukuu, zilichanika chanika. Na mikate yote katika chombo ilikuwa mikavu na yenye uvundo.
6 Kisha wakamwendea Yoshua katika kambi huko Giligali na wakamwambia yeye pamoja wa watu wa Israeli wakisema, “
7 Tumesafiri kutoka nchi ya mbali, basi fanyeni agano nasi.” Watu wa Israeli wakawaamba Wahivi, “Huenda mnaishi karibu nasi. Twawezeje kufanya agano nanyi?”
8 Wakamwambia Yoshua, “Sisi ni watumishi wako.”Yoshua akawauliza, “Ninyi ni akina nani? Mnatokea wapi?
9 Wakamwambia, “Watumishi wako wamekuja hapa kutokea nchi ya mbali, kwasababu ya jina la Yahweh Mungu wako. Tumesikia habari kumhusu na kuhusu kila kitu alichokifanya Misri -
10 na kila kitu alichokifanya kwa wafalme wawili wa Waamori katika upande mwingine wa Yordani - kwa mfalme Sihoni wa Heshiboni, na kwa Ogu wa Bashani aliyekuwa katika Ashitarothi.
11 Wazee wetu na wenyeji wote wa nchi yetu walituambia,” Chukueni chakula mikononi mwenu kwa ajili ya safari. Nendeni mkakutane nao, na kisha muwambie, “Sisi ni watumishi wenu. Fanyeni agano pamoja nasi.”
12 Huu ni mkate wetu, ulikuwa wa moto tulipouchukua kutoka katika nyumba zetu katika siku ile tulipotoka kuja kwenu. Lakini sasa, tazama, imekuwa kavu na yenye ukungu.
13 Viriba hivi vilikuwa vipya tulipovijaza, na tazama, sasa vinavuja. Nguo zetu na viatu vyetu vimechakaa na kuwa vikuukuu kwasababu ya safari ndefu.”
14 kwahiyo, Waisraeli wakatwaa sehemu ya vyakula vyao, lakini walifanya hivyo bila ya kumwuliza Yahweh ili awaongoze.
15 Yoshua akafanya amani pamoja nao na kufanya agano pamoja nao ili waishi. Viongozi wa watu nao pia wakawaapia.
16 Siku tatu baada ya Waisraeli kufanya agano pamoja nao, waligundua kuwa walikuwa ni majirani zao na ya kwamba waliishi karibu nao.
17 Kisha watu wa Israeli walisafiri na kufika katika miji yao katika siku ya tatu. Miji yao ilikuwa Gibeoni, Kefira, Beerothi, na Kiriathi Yearimu.
18 Watu wa Israeli wahakushambulia kwasababu viongozi wao walikuwa wamewaapia mbele za Yahweh, Mungu wa Israeli. Waisraeli wote walikuwa wananung'unika kinyume na viongozi wao.
19 Lakini viongozi wote waliawaambia watu wote wa Israeli, “Tumeapa kwa Yahweh, Mungu wa Israeli kwa ajili yao, na sasa hatuwezi kuwadhuru.
20 Hiki ndicho tutakachowafanyia: Tutawaacha waishi ili tuepuke ghadhabu ambayo yaweza kuja juu yetu kwasababu ya kiapo tulichowaapia.”
21 Viongozi wakawaambia watu, “Waacheni waishi.” Hivyo Wagibeoni wakawa wakata kuni na wachota maji wa Waisraeli wote, kama vile viongozi walivyosema juu yao.
22 Yoshua aliwaita na kuwaambia, “Kwanini mlitudanya wakati mliposema, “Tuko mbali sana nanyi' wakati mnaishi hapa hapa miongoni mwetu?
23 Na kwasababu hii, mmelaaniwa na baadhi yenu mtakuwa watumwa siku zote, wenye kukata kuni na kuchota maji kwa ajli ya nyumba ya Mungu wangu.”
24 Walimjibu Yoshua na kusema, “Ni kwasababu watumishi wako waliambiwa kwamba Yahweh Mungu wenu alimwagiza Musa mtumishi wake kuwapa ninyi nchi yote, na kuwateteza wenyeji wote wa nchi mbele yenu - hivyo tuliogopa kwasababu yenu kwa ajili ya maisha yetu. Ndio maana tulifanya jambo hili.
25 Tazama sasa, mnatumiliki chini ya utawala wenu. Chochote kilichochema na haki kwenu kutufanyia, fanyeni.”
26 Basi Yoshua aliwafanyia hivi: aliwaondoa katika mamlaka ya watu wa Israeli, na Waisraeli hawakuwaua.
27 Siku hiyo Yoshua aliwafanya Wagibeoni kuwa wakata kuni na wachotaji wa maji kwa jamii, na kwa madhabahu ya Yahweh hadi leo katika sehemu ambayo Yahweh huichagua.