< Yoshua 20 >

1 Baada ya hayo, Yahweh akamwambia Yoshua,
Ndipo Bwana akamwambia Yoshua,
2 “Waambia watu wa Israeli, na kusema, 'Chagueni miji ya makimbilio ambayo niliwaambia kupitia kwa Musa.
“Waambie Waisraeli, watenge miji mikubwa ya kukimbilia, kama nilivyokuagiza kupitia Mose,
3 Fanyeni hivi ili mtu akiua mtu bila kukusudia aweze kwenda huko. Miji hii itakuwa ni sehemu ya kukimbilia kutoka kwa mtu yeyote yule anayetaka kulipiza kisasi kwa damu ya mtu aliyeuliwa.
ili mtu yeyote atakayemuua mtu kwa bahati mbaya na pasipo kukusudia aweze kukimbilia huko na kujiepusha na mlipiza kisasi wa damu.
4 Atakimbilia kwa mji mmoja miongoni mwa miji hiyo na atasimama mlangoni mwa lango la mji, na ataeleza kesi yake kwa wazee wa mji ule. Kisha watamwingiza ndani ya mji na watampatia sehemu yake ya kuishi miongoni mwao.
“Anapokimbilia mojawapo ya hii miji mikubwa atasimama kwenye maingilio ya lango la mji mkuu na kueleza wazee wa mji kuhusu shauri lake. Kisha watampokea katika mji wao na kumpa mahali pa kuishi nao.
5 Na kama mtu akija akataka kulipiza kisasi kwa damu ya mtu yule ambaye aliuliwa, ndipo watu wa mji hawatatakiwa kumtoa kwa wenye mamlaka mtu huyo aliyeua. Hawaruhusiwi kufanya hivyo kwasababu alimwua jirani bila kukusudia na hakuwa na chuki naye hapo awali.
Kama mlipiza kisasi wa damu akimfuatilia, wasimkabidhi yule mshtakiwa, kwa sababu alimuua jirani yake bila kukusudia, na bila kuwa na nia ya kudhuru.
6 Ni lazima akae katika mji ule mpaka pale atakapokuwa amesimama mbele ya kusanyiko kwa ajili ya kuhukumiwa, hadi pale atakapokufa mtu yule anayetumika katika nafasi ya kuhani mkuu katka siku hizo. Na kisha mtu yule aliyeua bila kukusudia aweza kurudi nyumbani kwake, katika mji ule ulikotoka.
Huyu aliyeua atakaa kwenye mji mkubwa huo mpaka awe amesimama kukabili mashtaka yake mbele ya kusanyiko na mpaka kuhani mkuu anayehudumu kwa wakati huo atakapokufa. Ndipo atakapoweza kurudi nyumbani kwake katika mji ambao aliukimbia.”
7 Kwahiyo, Waisraeli wakaichaguia Kedeshi iliyoko Galilaya katika nchi ya milima ya Nafutali, Shekemu katika nchi ya milima ya Efraimu, na Kiriathi Arba (ambayo ndio Herbroni) katika nchi ya milima ya Yuda.
Basi wakatenga Kedeshi katika Galilaya kwenye nchi ya vilima ya Naftali, Shekemu katika nchi ya vilima ya Efraimu, na Kiriath-Arba (yaani Hebroni) kwenye nchi ya vilima ya Yuda.
8 Katika ng'ambo ya Yordani mashariki mwa Yeriko, walichagua mji wa Bezeri huko nyikani katika nyanda za kabila la Rubeni; na Ramothi Gileadi kutoka kabila la Gadi; na Golani katika Bashani, kutoka katika kabila la Manase.
Katika upande wa mashariki mwa Yordani ya Yeriko wakatenga Bezeri katika jangwa katika uwanda wa juu katika kabila la Reubeni, Ramothi katika Gileadi katika kabila la Gadi, na Golani huko Bashani katika kabila la Manase.
9 Hii ni miji iliyochaguliwa kwa ajili ya watu wote wa Israeli na kwa ajili ya wageni wanaoishi miongoni mwao, ili kwamba mtu yeyote amwuaye mtu bila kukusudia aweza kukimbilia huko kwa ajili ya kupata usalama. Mtu huyu hatakufa kwa mkono wa mtu yule anayetake kulipiza kisasi cha damu iliyomwagwa, mpaka hapo kwanza mtuhumiwa atakaposimama mbele ya kusanyiko la watu.
Mwisraeli yeyote au mgeni yeyote aishiye miongoni mwao aliyemuua mtu kwa bahati mbaya, angeweza kukimbilia katika miji mikubwa hiyo iliyotengwa na asiuawe na mlipiza kisasi wa damu kabla hajasimama kukabili mashtaka mbele ya kusanyiko.

< Yoshua 20 >