< Yoshua 16 >
1 Nchi waliyopewa kabila la Yusufu ilianzia katika Yordani huko Yeriko, mashariki mwa chemichemi za Yeriko, kupitia nyikani, kupanda kutoka Yeriko kupitia nchi ya milima ya Betheli.
2 Kisha uliendelea kutoka Betheli hadi Luzi na kupita hata Atarothi, iliyo miliki ya Waarkiti.
3 Kisha ilishuka chini upande wa magharibi kuelekea himaya ya Wayafuleti, hadi kufika miliki ya Loweri Bethi Horoni, na kisha iliendelea hadi Gezeri; na ilikomea katika bahari.
4 Ilikuwa ni kwa njia hii makabila ya Yusufu, yaani Manase na Efraimu yalipata urithi wao.
5 Eneo la kabila la Efraimu ambalo lilikuwa limegawanya kwa koo zao lilikuwa kama ifuatavyo: mpaka wa urithi wao katika upande wa mashariki ulikuwa Atarothi Ada uliopanda kuelekea Bethi Horoni ya juu,
6 na kutoka pale uliendelea hadi katika bahari. Kutoka Mikimethathi katika upande wa Kasikazini ulipinda upande wa mashariki kuelkea Taanathi Shilo na kupita ng'ambo yake katika upande wa mashariki kukabili Yanoa.
7 Kisha ulishuka kutoka Yanoa hadi Atarothi na hata Naara, na kisha ukafika Yeriko, na kuishia katika Yordani.
8 Kutoka Tapua, mpaka uliendelea katika upande wa magharibi hata kijito cha Kana na ulikomea katika bahari. Huu ulikuwa ni urithi wa kabila la Efraimu, uliogawanywa katika koo zao,
9 pamoja na miji yao iliyochaguliwa kwa ajili ya kabila la Efraimu iliyokuwa ndani ya urithi wa kabila la Manase - miji yote pamoja na vijiji vyao.
10 Lakini hawakuwafukuza Wakanaani walioishi katika Gezeri, hivyo basi Wakanaani wanaishi ndani ya Efraimu hadi leo, lakini watu hawa walifanywa kuwa watumwa.