< Yoshua 14 >
1 Maeneo haya ya nchi ambayo watu wa Israeli waliyapokea kama urithi wao katika nchi ya Kanaani. Urith huu uligawanywa kwao na Eliazeri kuhani, na Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi wa makabila ya mababu wa familia zao kati ya watu wa Israeli.
2 Urithi wao ulichaguliwa kwa kupiga kura kwa makabila tisa na nusu, kama vile Yahweh alivyoagiza kwa mkono wa Musa.
3 Kwa kuwa Musa alikuwa amewapa urithi makabila mawili na nusu ng'ambo ya Yordani, lakini Walawi hawakupewa urithi wowote.
4 Kabila la Yusufu kwa uhalisia yalikuwa makabila mawili, Manase na Efraimu. Na hakuna sehemu yoyote ya urithi waliyopewa Walawi katika nchi, lakini walipewa miji ya kuishi ndani yake pamoja na sehemu ya malisho ya mifugo yao na kwa ajili ya riziki zao.
5 Watu wa Israeli walifanya hivyo kama vile Yahweh alivyomwagiza Musa, basi waliiganywa nchi.
6 Kisha kabila la Yuda lilikuja kwa Yoshua huko Giligali. Kalebu mwana wa Yefune Mkenizi, akamwambia,”Unajua kile Yahweh alichomwambia Musa mtu wa Mungu juu yako na mimi huko Barnea.
7 Nilikuwa na umri wa miaka arobani wakati Musa mtumishi wa Yahweh aliponituma kutoka Kadeshi Barnea kuipeleleza nchi. Nilimletea taarifa tena kama nilivyotakiwa kufanya katika moyo wangu.
8 Lakini ndugu zangu walioenda pamoja nami waliifanya mioyo ya watu iyeyuke kwa woga. Lakini mimi nilimfuata Yahweh kabisa.
9 Musa aliapa katika siku hiyo akisema, “Hakika nchi ambayo miguu yako imetembea juu yake itakuwa urithi wako na kwa watoto wako milele, kwasababu umemfuata kabisa Yahweh Mungu wangu.
10 Tazama! sasa, Yahweh amenihifadhi hai kwa miaka hii arobaini na tano, kama alivyosema - tangu kipindi kile Yahweh alivyomwambia Musa neno hili, wakati huo Waisraeli walikuwa wakitembea jangwani. Tazama! sasa katika siku hii ya leo nina miaka themanini na mitano.
11 Bado hata siku hii ya leo nina nguvu kama nilivyokuwa katika siku ile ambayo Musa alinituma. Nguvu zangu za sasa ni sawa na nguvu zangu za kipindi kile, kwa ajili ya vita na kwa kwenda na kwa kuja.
12 Sasa basi, nipe nchi hii ya milima, ambayo Yahweh aliniahidi katika siku hiyo. Kwa kuwa ulisikia katika siku hiyo kuwa Wanakimu walikuwa huko katika miji yenye ngome. Itakuwa kwamba Yahweh atakuwa pamoja nami na ya kwamba nitawafukuzia mbali, kama vile Yahweh alivyosema.”
13 Kisha Yoshua alimbariki Kalebu mwana wa Yefune na alimpa Hebroni kama urithi wake.
14 Hivyo Hebroni ikawa urithi wa Kalebu mwana wa Yefune Mkenizi hata leo, kwasababu alimfuata kabisa Yahweh, Mungu wa Israeli.
15 Basi, jina la Hebroni hapo mwanzo lilikuwa ni Kiriathi Arba ( Arba ambaye alikuwa ni mtu mkuu miongoni mwa Wanakim). Kisha nchi ikawa na raha bila vita.