< Yoshua 13 >
1 Sasa Yoshua alikuwa mzee wakati Yahweh alipomwambia, “Umekuwa mzee, lakini bado kuna nchi kubwa ya kuteka.
Yoshua alipokuwa mzee na umri wake ukiwa umesogea sana, Bwana akamwambia, “Wewe ni mzee sana, na bado kumesalia sehemu kubwa sana za nchi ambazo ni za kutwaliwa.
2 Nchi iliyosalia ndio hii: mikoa yote ya Wafilisti, na mikoa ile ya Wageshuri,
“Nchi iliyosalia ni hii: maeneo yote ya Wafilisti na Wageshuri:
3 (tangu Shihori, iliyoko mashariki mwa Misri, na upande wa kaskazini kuelekea mpaka wa Ekroni, inayofikiriwa kuwa ni mali ya Wakanaani; wafalme watano wa Wafilisti, wale wafalme wa Gaza, Ashidodi, Ashikeloni, Gathi na Ekroni - miliki ya Waavi.
kutoka Mto Shihori ulioko mashariki mwa Misri, kuelekea kaskazini kwenye eneo la Ekroni, ambayo yote ilihesabika kama ya Wakanaani (maeneo yale matano ya watawala wa Kifilisti, ambayo ni Gaza, Ashdodi, Ashkeloni, Gathi na Ekroni: ndiyo nchi ya Waavi);
4 Katika upande wa kusini, kulisalia nchi yote ya Wakanaani, na Meara ambayo ni miliki ya Wasidoni, hadi Afeki, hata mpaka wa Waamori;
kuanzia kusini, nchi yote ya Wakanaani, kuanzia Ara ambayo ni ya Wasidoni, ikienea hadi Afeki, na eneo la Waamori,
5 nchi ya Wagebali, Lebanoni kuelekea upande wa mapambazuko ya jua, kutoka Baali- Gadi chini ya Mlima Hermoni mpaka Lebo Hamathi.
eneo la Wagebali; Lebanoni yote kuelekea mashariki, kuanzia Baal-Gadi chini ya Mlima Hermoni hadi Lebo-Hamathi.
6 Pia, wenyeji wote wa nchi ya milima kutoka Lebanoni hadi Misrefothi - Maimu, pamoja na watu wa Sidoni. Nitawafukuza mbele ya jeshi la Israeli. Uwe na uhakika wa kuwapa Waisraeli nchi kama urithi, kama nilivyokuagiza.
“Na kuhusu wakaaji wote katika maeneo ya milima, kuanzia Lebanoni hadi Misrefoth-Maimu, pamoja na eneo lote la Wasidoni, mimi mwenyewe nitawafukuza watoke mbele ya Waisraeli. Hakikisha umegawa nchi hii kwa Israeli kuwa urithi, kama nilivyokuagiza,
7 Igawanye nchi hii kama urithi kwa makabila tisa na kwa nusu ya kabila la Manase.
sasa basi, ligawanye eneo hili kwa yale makabila tisa na ile nusu ya kabila la Manase kuwa urithi.”
8 Pamoja na nusu nyingine ya kabila la Manase, Wareubeni na Wagadi wamekwisha kupokea urithi wao ambao Musa aliwapa katika upande wa mashariki wa Yordani,
Ile nusu nyingine ya Manase, Wareubeni na Wagadi, walishapokea urithi Mose aliokuwa amewapa mashariki mwa Yordani, sawasawa na mtumishi wa Bwana alivyowagawia.
9 kutoka Aroeri, iliyo katika ukingo wa bonde la mto Arnoni (kujumuisha na mji ambao uko katikati ya bonde), kwa nyanda zote za Medeba hadi Diboni;
Eneo lao lilienea toka Aroeri, iliyoko ukingoni mwa Bonde la Arnoni kuanzia mji ulio katikati ya bonde, likijumlisha nchi ya uwanda wa juu wote wa Medeba mpaka Diboni,
10 miji yote ya Sihoni, mfalme wa Waamori, ambaye alitawala katika Heshiboni, hata mpaka wa Waamori,
nayo miji yote ya Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala Heshboni, hadi mpakani mwa Waamoni.
11 Gileadi na mkoa wa Wageshuri na Maakathi, mlima wote wa Hermoni, Bashani yote mpaka Saleka;
Vilevile ilijumlisha Gileadi, eneo la Wageshuri na Wamaaka, mlima wote wa Hermoni na Bashani yote ikienea hadi Saleka:
12 ufalme wote wa Ogu katika Bashani, aliyetawala katika Ashitarothi na Edrei - hawa ni wale waliosalia katika Refaimu - ambao Musa aliwapiga na kuwafukuzia mbali.
yaani ufalme wote wa Ogu katika Bashani, aliyekuwa ametawala katika Ashtarothi na Edrei, na ndiye pekee alisalia kwa Warefai. Mose alikuwa amewashinda na kuteka nchi yao.
13 Lakini watu wa Israeli hawakuwafukuza Wageshuri wala Wamakathi. Badala yake, Wageshuri na Wamakathi wanaishi miongoni mwa Waisraeli hadi leo.
Lakini Waisraeli hawakuwafukuza watu wa Geshuri na wa Maaka, kwa hiyo wanaendelea kuishi miongoni mwa Waisraeli mpaka leo hii.
14 Kabila la Lawi pekee halikupewa urithi na Musa. Urithi wao ni sadaka za Yahweh, Mungu wa Israeli, zilizotolewa kwa moto, kama Mungu alivyomwagiza Musa.
Lakini kwa kabila la Lawi, Mose hakupeana urithi, kwa kuwa sadaka za kuteketezwa kwa moto zilizotolewa kwa Bwana, Mungu wa Israeli, ndizo zilizokuwa urithi wao, kama alivyowaahidi.
15 Musa aliwapa urithi kabila la Rubeni, ukoo kwa ukoo.
Haya ndiyo maeneo ambayo Mose alikuwa amewapa kabila la Reubeni ukoo kwa ukoo:
16 Miliki yao ilikuwa kutoka Aroeri, juu ya ukingo wa bonde la Mto Arnoni, na mji ulio katikati ya bonde, na nyanda zote za Medeba.
Eneo la Aroeri lililo ukingoni mwa Bonde la Arnoni, na kuanzia mji ulio katikati ya bonde, pia uwanda wote wa juu kupita Medeba
17 Wareubeni walipata pia Heshiboni, na miji yake yote zilizo katika uwanda, Diboni, na Bamathi Baali, na Bethi Baalimeoni,
hadi Heshboni na miji yake yote kwenye uwanda wa juu, ikijumlishwa miji ya Diboni, Bamoth-Baali, Beth-Baal-Meoni,
18 na Yahazi, na Kedemothi, na Mefaathi,
Yahasa, Kedemothi, Mefaathi,
19 na Kiriathaimu, na Sibuma, na Zerethishahari juu ya kilima cha bonde.
Kiriathaimu, Sibma, Sereth-Shahari juu ya kilima kilicho katika bonde,
20 Wareubeni walipata pia Bethi Peori, miteremko ya Pisiga, Bethi Yeshimothi,
Beth-Peori, materemko ya Pisga na Beth-Yeshimothi:
21 miji yote ya uwanda, na ufalme wote wa Sihoni, mfalme wa Waamori, ambaye alikuwa ametawala katika Heshiboni, ambaye Musa alikuwa amemshinda pamoja na viongozi wa Midiani, Evi, Rekemu, Zuri, Huri na Reba, wana wa mfalme wa Sihoni, ambao walikuwa wameishi katika nchi.
miji yote ya uwanda wa juu na eneo lote la utawala wa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala katika Heshboni. Mose alikuwa amemshinda Sihoni, pia watawala wakuu wa Wamidiani, ambao ni Evi, Rekemu, Suri, Huri na Reba, waliokuwa wameungana na Sihoni, ambao waliishi katika nchi ile.
22 Pia, watu wa Israeli walimwua kwa upanga Baalam mwana wa Beori, ambaye alifanya mambo ya uaguzi, miongoni mwa wale waliowaua.
Pamoja na wale waliouawa katika vita, Waisraeli walikuwa wamemuua kwa upanga Balaamu mwana wa Beori aliyekuwa mchawi.
23 Mpaka wa kabila la Rubeni ni Mto Yordani; huu ndio mpaka wao. Huu ulikuwa ni urithi wa kabila la Rubeni, uliotolewa kwa kila ukoo, pamoja na miji na vijiji vyao.
Mpaka wa Wareubeni ulikuwa ni ukingo wa Mto Yordani. Miji hii na vijiji vyake ndiyo iliyokuwa urithi wa Wareubeni ukoo kwa ukoo.
24 Hiki ndicho Musa alilipa kabila la Gadi, ukoo kwa ukoo:
Haya ndiyo maeneo ambayo Mose alikuwa amewapa kabila la Gadi, ukoo kwa ukoo:
25 Himaya yao ilikuwa Yazeri, miji yote ya Gileadi na nusu ya nchi ya Waamoni, hadi Aroeri, iliyo mashariki mwa Raba,
Nchi ya Yazeri, miji yote ya Gileadi na nusu ya nchi ya Amoni iliyoenea hadi Aroeri, karibu na Raba;
26 kutoka Heshiboni hadi Ramathi - Mizipe na Betonimu, kutoka Mahanaimu mpaka himaya ya Debiri.
na kuanzia Heshboni mpaka Ramath-Mispa na Betonimu, na kutoka Mahanaimu hadi eneo la Debiri;
27 Katika bonde, Musa aliwapa Bethi -Haramu, Bethi - Nimra, Sukothi, na Zafoni, ufalme uliobakia wa Sihoni mfalme wa Heshiboni, pamoja na Yordani kama mpaka, katika sehemu za chini za mwisho wa Bahari ya Kinerethi, upande wa mashariki ng'ambo ya Yordani.
na katika bonde, Beth-Haramu, Beth-Nimra, Sukothi na Safoni na sehemu iliyobaki ya eneo la utawala wa Sihoni mfalme wa Heshboni (upande wa mashariki mwa Mto Yordani, eneo inayoishia kwenye Bahari ya Kinerethi).
28 Huu ni urithi wa kabila la Gadi, ukoo kwa ukoo, pamoja na miji na vijiji vyao.
Miji hii na vijiji vyake ilikuwa urithi wa kabila la Gadi ukoo kwa ukoo.
29 Musa aliwapa urithi nusu ya kabila la Manase. Urithi uligawiwa kwa nusu ya kabila la watu wa Manase kutokana na kabila zao.
Haya ndiyo maeneo ambayo Mose alikuwa amewapa hiyo nusu ya kabila la Manase, yaani kwa nusu ya jamaa ya uzao wa Manase, ukoo kwa ukoo:
30 Miliki yao ilikuwa kutoka Mahanaimu, Bashani yote, ufalme wote wa mfalme Ogu wa Bashani, na miji yote ya Yairi, iliyo katika Bashani, miji sitini;
Eneo lililoenea kuanzia Mahanaimu, na kujumlisha Bashani yote, ufalme wote wa Ogu mfalme wa Bashani, makazi yote ya Yairi huko Bashani, miji sitini,
31 nusu ya Gileadi, na Ashitarothi na Edrei (miji ya kifalme ya Ogu katika Bashani). Miji hii iligawanywa kwa ukoo wa Makiri mwana wa Manase -nusu ya watu wa Makiri, walipewa kwa kila familia zao.
nusu ya Gileadi, na Ashtarothi na Edrei (miji ya kifalme ya Ogu katika Bashani). Hii ilikuwa kwa ajili ya wazao wa Makiri mwana wa Manase, kwa ajili ya nusu ya wana wa Makiri, ukoo kwa ukoo.
32 Huu ndio urithi ambao Musa aliowagawia katika nyanda za Moabu, ng'ambo ya Yordani mashariki mwa Yeriko.
Huu ndio urithi alioupeana Mose wakati alipokuwa katika tambarare za Moabu, ngʼambo ya Yordani mashariki mwa Yeriko.
33 Musa hakulipa urithi kabila la Lawi. kwa kuwa Yahweh, Mungu wa israeli, ni urithi wao, kama vile alivyowaambia.
Lakini kwa kabila la Walawi, Mose hakuwapa urithi; Bwana Mungu, Mungu wa Israeli ndiye urithi wao, kama alivyowaahidi.