< Yohana 4 >
1 Basi Yesu alipofahamu kuwa Mafarisayo wamesikia kuwa Yesu alikuwa anafuasa na kuwabatiza zaidi ya Yohana,
2 (ingawa Yesu mwenyewe alikuwa habatizi ila wanafunzi wake),
3 alitoka Judea na akaenda Galilaya.
4 Hivyo ilikuwa muhimu kupitia Samaria.
5 Na akafika kwenye mji wa Samaria, unaoitwa Sikari, karibu na eneo ambalo Yakobo alimpa mwanae Yusufu.
6 Na kisima cha Yakobo kilikuwa hapo. Yesu alikuwa amechoka kwa ajili ya safari na akakaa karibu na kisima. Ilikuwa muda wa mchana.
7 Mwanamke Msamaria alikuja kuteka maji, na Yesu akamwambia, “Nipe maji ninywe.”
8 Kwa sababu wanafunzi wake walikuwa wameenda zao mjini kununua chakula.
9 Yule mwanamke akamwambia, “Inakuaje wewe Myahudi, kuniomba mimi mwanamke Msamaria, kitu cha kunywa?” Kwa sababu Wayahudi hawachangamani na Wasamaria.
10 Yesu akamjibu, “Kama ungelijua karama ya Mungu, na yule anayekuambia 'Nipe maji, ' ungelimwomba, na angelikupa maji ya uzima.”
11 Mwanamke akajibu, “Bwana hauna ndoo ya kuchotea, na kisima ni kirefu. Utayapata wapi Maji ya Uzima?
12 Je wewe ni mkuu, kuliko baba yetu Yakobo, ambaye alitupa kisima hiki, na yeye mwenyewe na watoto wake pamoja na mifugo yake wakanywa maji ya kisima hiki?”
13 Yesu akajibu, “Yeyote anywae maji haya atapata kiu tena,
14 lakini yeye atakaye kunywa maji nitakayompa hatapata kiu tena. Badala yake maji nitakayompa yatakuwa chemchemi inayobubujika hata milele.” (aiōn , aiōnios )
15 Yule mwanamke akamwambia, “Bwana, nayaomba maji hayo ili nisipate kiu, na nisihangaike kuja hapa kuchota maji.”
16 Yesu akamwambia, “Nenda kamwite mumeo, kisha urudi.”
17 Mwanamke akamwambia, “Sina mume.” Yesu akajibu, “Umesema vyema, 'Sina mume;'
18 kwa maana umekuwa na wanaume watano, na mmoja ambaye unaye sasa sio mume wako. Katika hili umesema kweli!”
19 Mwanamke akamwambia, “Bwana naona yakuwa wewe ni nabii.
20 Baba zetu waliabudu katika mlima huu. Lakini ninyi mwasema ya kuwa Yerusalemu ndiyo sehemu ambayo watu wanapaswa kuabudu.”
21 Yesu akamjibu, “Mwanamke, niamini, wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba katika mlima huu au Yerusalemu.
22 Ninyi watu mwaabudu kile msichokijua, lakini sisi twaabudu tunachokijua, kwa sababu wokovu watoka kwa Wayahudi.”
23 Hatahivyo, wakati unakuja, na sasa upo hapa, wakati waabuduo kweli watamwabudu Baba katika roho na kweli, kwa sababu Baba anawatafuta watu wa namna hiyo kuwa watu wake wanao mwabudu.
24 Mungu ni Roho, na wale wanaomwabudu wanapaswa kumwabudu kwa roho na kweli.”
25 Mwanamke akamwambia, “Ninajua kuwa Masihi anakuja, (aitwaye Kristo). Huyo atakapokuja atatwambia yote.”
26 Yesu akamwambia, “Mimi unayesema nami ndiye.”
27 Wakati huo huo wanafunzi wake wakarudi. Nao walishangaa kwa nini alikuwa akizungumza na mwanamke, lakini hakuna aliyethubutu kumuuliza, “Unataka nini?” au “Kwa nini unazungumza naye?”
28 Hivyo mwanamke akauacha mtungi wake na akaenda mjini na akawambia watu,
29 “Njooni mwone mtu aliyeniambia mambo yangu yote niliyoyatenda, je yawezekana akawa ndiye Kristo?”
30 Wakatoka mjini wakaja kwake.
31 Wakati wa mchana wanafunzi wake walimsihi wakisema, “Rabi kula chakula.”
32 lakini yeye aliwambia, “Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi.”
33 Wanafunzi wakaambizana, hakuna aliyemletea kitu chochotekula,”Je walileta?”
34 Yesu akawambia, “Chakula changu ni kufanya mapenzi yake yeye aliyenituma na kutimiza kazi yake.
35 Je, hamsemi, 'Bado miezi mitano na mavuno yatakuwa tayari?' Ninawambieni tazameni mashamba yalivyo tayari kwa mavuno!
36 Yeye avunaye hupokea mishahara na kukusanya matunda kwa ajili ya uzima wa milele, ili kwamba yeye apandaye naye avunaye wafurahi pamoja. (aiōnios )
37 Kwa kuwa msemo huu ni wa kweli, 'Mmoja apanda na mwingine avuna.'
38 Niliwatuma kuvuna ambacho hamkukihangaikia, Wengine wamefanya kazi na ninyi mmeingia katika furaha ya kazi yao.”
39 Wasamaria wengi katika mji ule walimwani kwa sababu ya taarifa ya yule mwanamke aliyekuwa akishuhudia, “Aliyeniambia mambo yote niliyoyafanya.”
40 Hivyo Wasamaria walipokuja walimsihi akae pamoja nao na akakaa kwao kwa siku mbili.
41 Na wengi zaidi wakamwamini kwa sababu ya neno lake.
42 Wakamwambia yule mwanamke, “Tunaamini sio tu kwa maneno yako, kwa sababu sisi wenyewe tumesikia, na sasa twafahamu kuwa hakika yeye ni mwokozi wa ulimwengu.”
43 Baada ya siku hizo mbili, akaondoka na kuelekea Galilaya.
44 Kwa sababu yeye mwenyewe alikuwa ametangaza kuwa nabii hana heshima katika nchi yake mwenyewe.
45 Alipokuja kutoka Galilaya, Wagalilaya walimkaribisha. Walikuwa wameona mambo yote aliyoyafanya Yerusalemu kwenye sikukuu, kwa sababu na wao pia walikuwa wamehudhuria kwenye sikukuu.
46 Alikuja tena Kana ya Galilaya huko alikoyabadilisha maji kuwa divai. Palikuwa na ofisa ambaye mwana wake alikuwa ni mgonjwa huko Kapernaumu.
47 Aliposikia kuwa Yesu alitoka Judea na kwenda Galilaya, alienda kwa Yesu na kumsihi atelemke amponye mwanawe, ambaye alikuwa karibu kufa.
48 Ndipo Yesu akamwambia, “Ninyi msipoona ishara na maajabu hamwezi kuamini.
49 Kiongozi akasema, “Bwana shuka chini kabla mwanangu hajafa.”
50 Yesu akamwambia, “Nenda mwanao ni mzima.” Yule mtu akaamini neno alilolisema Yesu na akaenda zake.
51 Alipokuwa akishuka, watumishi wake walimpokea na kumwambia mwana wake alikuwa mzima.
52 Hivyo akawauliza ni muda gani alipata nafuu. Wakajibu, “Jana muda wa saa saba homa ilipomwacha.”
53 Ndipo baba yake akatambua kuwa ni muda ule ule Yesu aliosema, “Mwana wako ni mzima.” Hivyo yeye na familia yake wakaamini.
54 Hii ilikuwa ni ishara ya pili aliyoifanya Yesu alipotoka Yudea kwenda Galilaya.