< Yohana 21 >
1 Baada ya mambo hayo Yesu alijidhihirisha tena kwa wanafunzi katika Bahari ya Tiberia; hivi ndivyo alivyojidhihirisha mwenyewe:
2 Simon Petro alikuwa pamoja na Thomaso aitwaye Didimas, Nathanaeli wa kana ya Galilaya, wana wa Zebedayo na wanafunzi wengine wawili wa Yesu.
3 Simon Petro akawaambia, “Mimi naenda kuvua samaki.” Nao wakamwambia, “Sisi, pia tutaenda nawe.” Wakaenda wakaingia kwenye mashua, lakini usiku huo wote hawakupata chochote.
4 Na asubuhi kulipokucha, Yesu alisimama ufukweni, nao wanafunzi hawakutambua kuwa alikuwa Yesu.
5 Kisha Yesu akawambia, “Vijana, mna chochote cha kula?” Nao wakamjibu, “Hapana.”
6 Akawambia, “Shusheni wavu upande wa kuume wa mashua, nanyi mtapata kiasi.” Kwa hiyo wakashusha wavu nao hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa cha samaki.
7 Basi yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro, “Ni Bwana.” Naye Simon Petro aliposikia kuwa ni Bwana, akajifunga vazi lake (maana hakuwa amelivaa vizuri), kisha akajitupa baharini.
8 Wale wanafunzi wengine wakaja kwenye mashua (kwani hawakuwa mbali na pwani, yapata mita mia moja kutoka ufukweni), nao walikuwa wakivuta zile nyavu zilizokuwa zimejaa samaki.
9 Walipofika ufukweni, waliona moto wa mkaa pale na juu yake kulikuwa na samaki pamoja na mkate.
10 Yesu akawambia, “Leteni baadhi ya samaki mliovua sasa hivi.”
11 Basi Simon Petro akapanda na kuukokota ule wavu uliokuwa umejaa samaki wakubwa, kiasi cha samaki 153; japo walikuwa wengi, ule wavu haukuchanika.
12 Yesu akawaambia, “Njoni mpate kifungua kinywa.” Hakuna hata mmoja wa wanfunzi aliyethubutu kumwuliza, “Wewe ni nani?” Walijua kuwa alikuwa ni Bwana.
13 Yesu akaja, akachukua ule mkate, kisha akawapa, akafanya vivyo hivyo na kwa wale samaki.
14 Hii ilikuwa mara ya tatu kwa Yesu kujidhihirisha kwa wanafunzi wake baada ya kufufuka toka wafu.
15 Baada ya kuwa wamefungua kinywa, Yesu akamwambia Simon Petro, “Simon mwana wa Yohana je, wanipenda mimi kuliko hawa?” Petro akajibu, “Ndiyo, Bwana; “Wewe wajua kuwa mimi nakupenda.” Yesu akamwambia, “Lisha wanakondoo wangu.”
16 Akamwambia mara ya pili, “Simon mwana wa Yona, je, wanipenda?” Petro akamwambia, “Ndiyo, Bwana; wewe wajua kuwa nakupenda. “Yesu akamwambia, “Chunga kondoo wangu.”
17 Akamwambia tena mara ya tatu, “Simon, mwana wa Yohana, Je wanipenda?” Naye Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, “Je Wewe wanipenda?” Naye akamwambia, “Bwana, unajua yote; unajua kuwa nakupenda.” Yesu akamwambia, Lisha kondoo wangu.
18 Amini, amini, nakuambia, ulipokuwa kijana ulizoea kuvaa nguo mwenyewe na kwenda kokote ulikotaka; lakini utakapokuwa mzee, utanyosha mikono yako, na mwingine atakuvalisha nguo na kukupeleka usikotaka kwenda.”
19 Yesu alisema haya ili kuonesha ni aina gani ya kifo ambacho Petro angemtukuza Mungu. Baada ya kuwa amesema haya, akamwambia Petro, “Nifuate.”
20 Petro aligeuka na kumwona yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akawafuata- Huyu ndiye aliyekuwa amajiegemeza kwenye kifua cha Yesu wakati wa chakula cha jioni na kumwuliza, “Bwana, ni nani atakayekusaliti?”
21 Petro alimwona na kisha akamwuliza Yesu, “Bwana, Huyu mtu atafanya nini?”
22 Yesu akamjibu, “Kama nataka abaki mpaka nitakapokuja, hilo linakuhusu nini?” Nifuate.”
23 Kwa hiyo habari hii ikaenea miongoni mwa wale ndugu, kwamba mwanafunzi huyo hatakufa. Lakini Yesu hakumwambia Petro kuwa, mwanafunzi huyo hafi, “Kama nataka yeye abaki mpaka nitakapokuja yakuhusu nini?”
24 Huyu ndiye mwanafunzi atoaye ushuhuda wa mambo haya, na ndiye aliye andika mambo haya, na tunajua ya kuwa ushuhuda wake ni kweli.
25 Kuna mambo mengine mengi ambayo Yesu aliyafanya. Kama kila moja lingeandikwa, nadhani kwamba ulimwengu wenyewe usingetosha kuviweka vitabu ambavyo vingeandikwa.