< Yohana 17 >
1 Yesu aliyasema mambo haya; kisha akainua macho yake kuelelea mbinguni na akasema, “Baba, saa imewadia; mtukuze mwanao ili na mwana naye akutukuze wewe -
2 kama vile ulivyompatia mamlaka juu ya vyote vyenye mwili ili awape uzima wa milele wale wote uliompatia. (aiōnios )
3 Huu ndio uzima wa milele: kwamba wakujue wewe, Mungu wa kweli na wa pekee, na yeye uliyemtuma, Yesu Kristo. (aiōnios )
4 Nilikutukuza hapa duniani, na kuikamilisha kazi uliyonipa niifanye.
5 Sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja na wewe mwenyewe kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja na wewe kabla ya ulimwengu kuumbwa.
6 Nililifunua jina lako kwa watu ulionipa hapa duniani. Walikuwa watu wako; lakini ulinikabidhi mimi. nao wamelishika neno lako.
7 Sasa wanajua kuwa kila kitu ulichonipa mimi kinatoka kwako,
8 kwa maneno yale uliyonipatia mimi— Nimekwisha wapatia wao maneno hayo. Waliyapokea na kweli wakajua ya kuwa mimi nimetoka kwako, na wakaamini kuwa wewe ndiye uliyenituma.
9 Ninawaombea wao. Siuombei ulimwaengu bali wale ulionipa kwa kuwa wao ni wako.
10 Vitu vyote ambavyo ni vyangu ni vyako, na vile ulivyonavyo wewe ni vyangu; nami ninatukuzwa katika hivyo.
11 Mimi simo tena ulimwenguni, bali wao wamo ulimwenguni, nami sasa naja kwako. Baba Mtakatifu, watunze kwa jina lako lile ulilonipa sisi ili wao nao wawe na umoja, kama vile mimi na wewe tulivyo na umoja.
12 Nilipokuwa nao, niliwalinda kwa jina ulilonipa; Niliwalinda, na hakuna hata mmoja wao aliyepotea isipokuwa mwana wa upotevu, ili kwamba maandiko yatimie.
13 Sasa ninakuja kwako; lakini ninasema haya ulimwenguni ili kwamba furaha yangu ikamilishwe ndani yao wenyewe.
14 Nimewapa neno lako; ulimwengu imewachukia kwa sababu wao si wa ulimwengu, kama vile mimi nisivyokuwa wa ulimwengu
15 Siwaombei kwamba uwatoe ulimwenguni bali uwalinde na yule mwovu.
16 Wao si wa dunia kama vile mimi nisivyokuwa wa ulimwenguni.
17 Uwaweke wakfu kwako mwenyewe katika Kweli; neno lako ndiyo kweli.
18 Ulinituma ulimwenguni, nami nimewatuma ulimwenguni.
19 Kwa ajili yao mimi mwenyewe ninajitoa kwako ili kwamba na wao wajitoe kwako kwa ile kweli.
20 Si hawa tu ninaowaombea, bali na wale watakaoamini kupitia neno lao
21 ili kwamba wao nao wawe na umoja, kama vila wewe Baba, ulivyo ndani yangu nami ndani yako. Nawaombea ili kwamba wao pia waweze kuwa ndani yetu ili ulimwengu uweze kuamini kuwa wewe ndiye uliyenituma.
22 Utukufu ule ulionipa mimi - nimewapa wao, ili kwamba waweze kuwa na umoja, kama vile sisi tulivyo umoja -
23 Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili waweze kukamilishwa katika umoja; ili ulimwengu ujue kuwa hakika wewe ndiye uliyenituma, na kuwapenda, kama vile wewe ulivyonipenda, mimi.
24 Baba, kile ulichonipa mimi - Natamani kwamba wao pia waweze kuwa pamoja nami mahali nilipo ili waweze kuona utukufu wangu, ule ulionipa: kwa kuwa wewe ulinipenda mimi kabla ya kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu.
25 Baba mwenye haki, ulimwengu haukukujua wewe, lakini mimi nakujua wewe; na wanajua kwamba ulinituma.
26 Nililifanya jina lako lijulikane kwao, na nitalifanya lijulikane ili kwamba lile pendo ambalo kwalo ulinipenda mimi liweze kuwa ndani yao, na mimi niweze kuwa ndani yao.”