< Yohana 1 >
1 Mwanzoni kulikuwako Neno, na Neno alikuwa pamoja na Mungu, na Neno alikuwa Mungu.
Hapo Mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa na Mungu, naye alikuwa Mungu.
2 Huyu, Neno, Mwanzoni alikuwa pamoja na Mungu.
Tangu mwanzo Neno alikuwa na Mungu.
3 Vitu vyote vilifanyika kupitia yeye, na pasipo yeye hakuna hata kitu kimoja kilichokuwa kimefanyika.
Kwa njia yake vitu vyote viliumbwa; hakuna hata kiumbe kimoja kilichoumbwa pasipo yeye.
4 Ndani yake kulikuwa uzima, na huo uzima ulikuwa nuru ya wanadamu wote.
Yeye alikuwa chanzo cha uhai na uhai huo ulikuwa mwanga wa watu.
5 Nuru yang'aa gizani, wala giza halikuizimisha.
Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza halikuweza kuushinda.
6 Palikuwa na mtu aliyetumwa kutoka kwa Mungu, ambaye jina lake alikuwa Yohana.
Mungu alimtuma mtu mmoja jina lake Yohane,
7 Alikuja kama shahidi kushuhudia kuhusu ile nuru, ili kwamba wote waweze kuamini kupitia yeye.
ambaye alikuja kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Alikuja ili kwa ujumbe wake watu wote wapate kuamini.
8 Yohana hakuwa ile nuru, bali alikuja ili ashuhudie kuhusu ile nuru
Yeye hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga.
9 Hiyo ilikuwa nuru ya kweli ambayo ilikuwa inakuja katika dunia nayo humtia nuru kila mmoja
Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote.
10 Alikuwa katika dunia, na dunia iliumbwa kupitia yeye, na dunia haikumjua.
Basi, Neno alikuwako ulimwenguni; na kwa njia yake ulimwengu uliumbwa, lakini ulimwengu haukumtambua.
11 Alikuja kwa vitu vyake, na watu wake hawakumpokea.
Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea.
12 Bali kwa wale wengi waliompokea, ambao waliamini jina lake, kwa hao aliwapa haki ya kuwa wana wa Mungu,
Lakini wale wote waliompokea na kumwamini, hao aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu.
13 Ambao walizaliwa, sio kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili, wala kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu mwenyewe.
Hawa wamekuwa watoto wa Mungu si kwa uwezo wa kibinadamu, wala kwa nguvu za kimwili, wala kwa mapenzi ya mtu, bali Mungu mwenyewe ndiye baba yao.
14 Naye Neno alifanyika mwili na akaishi miongoni mwetu, tumeuona utukufu wake, utukufu kama wa mtu pekee wa kipekee aliyekuja kutoka kwa Baba, amejaa neema na kweli.
Naye Neno akawa mwanadamu, akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu wake yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli.
15 Yohana alishuhudia kuhusu yeye, na alipaza sauti akisema, “Huyu ndiye ambaye nilisema habari zake nikisema, “Yule ajaye baada yangu ni mkuu kuliko mimi, kwa sababu amekuwako kabla yangu.”
Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, “Huyu ndiye niliyemtaja wakati niliposema: Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa.”
16 Kwa kuwa kutoka katika utimilifu wake, sisi sote tumepokea bure kipawa baada ya kipawa.
Kutokana na ukamilifu wake sisi tumepokea neema mfululizo.
17 Kwa kuwa sheria ililetwa kupitia Musa. Neema na kweli vilikuja kupitia Yesu Kristo.
Maana Mungu alitoa Sheria kwa njia ya Mose, lakini neema na kweli vimekuja kwa njia ya Kristo.
18 Hakuna mwanadamu aliyemwona Mungu wakati wowote. Mtu pekee ambaye ni Mungu, aliye katika kifua cha Baba, amemfanya yeye ajulikane.
Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote ule. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu.
19 Na huu ndio ushuhuda wa Yohana wakati makuhani na walawi waliotumwa kwake na Wayahudi kumwuliza, “Wewe ni nani?”
Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu walipowatuma makuhani wa Walawi kwake wamwulize: “Wewe u nani?”
20 Bila kusitasita na hakukana, bali alijibu, “Mimi sio Kristo.”
Yohane hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, “Mimi siye Kristo.”
21 Hivyo wakamuuliza, “kwa hiyo wewe ni nani sasa?” Wewe ni Eliya? Akasema, “Mimi siye.” Wakasema, Wewe ni nabii? Akajibu,” Hapana.”
Hapo wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Eliya?” Yohane akajibu, “La, mimi siye.” Wakamwuliza, “Je, wewe ni yule nabii?” Yohane akawajibu, “La!”
22 Kisha wakamwambia, “Wewe ni nani, ili kwamba tuwape jibu waliotutuma”? Wajishuhudiaje wewe mwenyewe?”
Nao wakamwuliza, “Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma.”
23 Akasema, “Mimi ni sauti yake aliaye nyikani: 'Inyosheni njia ya Bwana,' kama nabii Isaya alivyosema.”
Yohane akawajibu, “Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake: Sauti ya mtu imesikika jangwani: Nyoosheni njia ya Bwana.”
24 Basi kulikuwa na watu wametumwa pale kutoka kwa Mafarisayo. Wakamuuliza na kusema,
Hao watu walikuwa wametumwa na Mafarisayo.
25 “Kwa nini unabatiza basi kama wewe sio Kristo wala Eliya wala nabii?”
Basi, wakamwuliza Yohane, “Kama wewe si Kristo, wala Eliya, wala yule nabii, mbona wabatiza?”
26 Yohana aliwajibu akisema, “Ninabatiza kwa maji. Hata hivyo, miongoni mwenu anasimama mtu msiyemtambua.
Yohane akawajibu, “Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, msiyemjua bado.
27 Huyu ndiye ajaye baada yangu. Mimi sisitahili kulegeza kamba za viatu vyake.”
Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu vyake.”
28 Mambo haya yalitendeka huko Bethania, ng'ambo ya Yordani, mahali ambapo Yohana alikuwa akibatiza.
Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ng'ambo ya mto Yordani ambako Yohane alikuwa anabatiza.
29 Siku iliyofuata Yohana alimwona Yesu akija kwake akasema, “Tazama mwanakondoo wa Mungu aichukuae dhambi ya ulimwengu!
Kesho yake, Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, “Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu!
30 huyu ndiye niliyesema habari zake nikisema, “Yeye ajaye nyuma yangu ni mkuu kuliko mimi, kwa kuwa alikuwa kabla yangu.'
Huyu ndiye niliyesema juu yake: Baada yangu anakuja mtu mmoja aliye mkuu zaidi kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa!
31 Sikumtambua yeye, lakini ilifanyika hivyo ili kwamba afunuliwe katika Israeli, kwamba nilikuja nikibatiza kwa maji.”
Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini nimekuja kubatiza kwa maji ili watu wa Israeli wapate kumjua.”
32 Yohana alishuhudia, “Niliona Roho akishuka kutoka mbinguni mfano wa hua, na ilibaki juu yake.
Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa: “Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni na kutua juu yake.
33 Mimi sikumtambua lakini yeye aliyenituma ili nibatize kwa maji aliniambia, 'yule ambaye utaona Roho akishuka na kukaa juu yake, Huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu.'
Mimi sikumjua, lakini yule aliyenituma nikabatize watu kwa maji alikuwa ameniambia: Mtu yule utakayemwona Roho akimshukia kutoka mbinguni na kukaa juu yake, huyo ndiye anayebatiza kwa Roho Mtakatifu.
34 Nimeona na nimeshuhudia kwamba huyu ni Mwana wa Mungu.”
Mimi nimeona na ninawaambieni kwamba huyu ndiye Mwana wa Mungu.”
35 Tena siku iliyofuata Yohana alikuwa amesimama pamoja na wanafunzi wake wawili,
Kesho yake, Yohane alikuwa tena mahali hapo pamoja na wanafunzi wake wawili.
36 walimwona Yesu akitembea na Yohana akasema, “Tazama, Mwana kondoo wa Mungu!”
Alipomwona Yesu akipita akasema, “Tazameni! Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu.”
37 Wanafunzi wawili walimsikia Yohana akisema haya wakamfuata Yesu.
Hao wanafunzi walimsikia Yohane akisema maneno hayo, wakamfuata Yesu.
38 Tena Yesu aligeuka na kuwaona wanafunzi wale wakimfuata, na akawambia, “Mnataka nini?” Wakajibu, “Rabbi, (maana yake 'mwalimu,' unaishi wapi?”
Basi, Yesu aligeuka, na alipowaona hao wanafunzi wanamfuata, akawauliza, “Mnatafuta nini?” Nao wakamjibu, “Rabi (yaani Mwalimu), unakaa wapi?”
39 Akawambia, “Njooni na mwone.”Kisha walikwenda na kuona mahali alipokuwa akiishi; walikaa pamoja naye siku hiyo, kwa kuwa ilikuwa yapata kama saa kumi hivi.
Yesu akawaambia, “Njoni, nanyi mtaona.” Hao wanafunzi wakamfuata, wakaona mahali alipokuwa anakaa, wakashinda naye siku hiyo. Ilikuwa yapata saa kumi jioni.
40 Mmoja wa wale wawili waliomsikia Yohana akiongea na kisha kumfuata Yesu alikuwa ni Andrea, ndugu yake Simoni Petro.
Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa hao wawili waliokuwa wamemsikia Yohane akisema hivyo, wakamfuata Yesu.
41 Akamwona ndugu yake Simoni na akamwambia, “Tumempata Masihi” (ambayo inatafsiriwa Kristo).
Andrea alimkuta kwanza Simoni, ndugu yake, akamwambia, “Tumemwona Masiha” (maana yake Kristo).
42 Akamleta kwa Yesu. Yesu akamtazama na akasema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohana” utaitwa Kefa,” (maana yake 'Petro').
Kisha akampeleka Simoni kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama Simoni akasema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohane. Sasa utaitwa Kefa.” (maana yake ni Petro, yaani, “Mwamba.”)
43 Siku iliyofuata wakati Yesu alipotaka kuondoka kwenda Galilaya, alimpata Filipo na akamwambia, “Nifuate mimi.”
Kesho yake Yesu aliamua kwenda Galilaya. Basi, akamkuta Filipo, akamwambia, “Nifuate.”
44 Filipo alikuwa ni mwenyeji wa Bethsaida, mji wa Andrea na Petro.
Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji wa akina Andrea na Petro.
45 Filipo alimpata Nathanaeli na kumwambia, Tumempata yule ambaye Musa aliandika habari zake katika sheria na Manabii. Yesu mwana wa Yusufu, kutoka Nazareti.
Naye Filipo akamkuta Nathanieli, akamwambia, “Tumemwona yule ambaye Mose aliandika juu yake katika kitabu cha Sheria, na ambaye manabii waliandika habari zake, yaani Yesu Mwana wa Yosefu, kutoka Nazareti.”
46 Nathanaeli akamwambia, “Je kitu chema chaweza kutokea Nazareti?” Filipo akamwambia, Njoo na uone.”
Naye Nathanieli akamwuliza Filipo, “Je, kitu chema chaweza kutoka Nazareti?” Filipo akamwambia, “Njoo uone.”
47 Yesu akamwona Nathanaeli akija kwake na akasema, “Tazama, Mwisraeli kweli kweli asiye na udanganyifu ndani yake!”
Yesu alipomwona Nathanieli akimjia alisema juu yake, “Tazameni! Huyo ni Mwisraeli halisi: hamna hila ndani yake.”
48 Nathanaeli akamwambia, “Umenifahamuje mimi?” Yesu akajibu na akamwambia, “Kabla Filipo hajakuita ulipokuwa chini ya mtini, nalikuona.”
Naye Nathanieli akamwuliza, “Umepataje kunijua?” Yesu akamwambia, “Ulipokuwa chini ya mtini hata kabla Filipo hajakuita, nilikuona.”
49 Nathanaeli akajibu, “Rabi wewe u Mwana wa Mungu! Wewe ni Mfalme wa Israeli”!
Hapo Nathanieli akamwambia, “Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu. Wewe ni Mfalme wa Israeli!”
50 Yesu akajibu akamwambia, Kwa sababu nilikuambia 'nilikuona chini ya mtini' je waamini? utaona matendo makubwa kuliko haya.”
Yesu akamwambia, “Je, umeamini kwa kuwa nimekwambia kwamba nilikuona chini ya mtini? Utaona makubwa zaidi kuliko haya.”
51 Yesu akasema, “Amini amini nawambieni mtaziona mbingu zikifunguka, na kuwaona malaika wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”
Yesu akaendelea kusema, “Nawaambieni kweli, mtaona mbingu zinafunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Mtu.”