< Yohana 1 >
1 Mwanzoni kulikuwako Neno, na Neno alikuwa pamoja na Mungu, na Neno alikuwa Mungu.
Hapo mwanzo alikuwako Neno, huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.
2 Huyu, Neno, Mwanzoni alikuwa pamoja na Mungu.
Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu.
3 Vitu vyote vilifanyika kupitia yeye, na pasipo yeye hakuna hata kitu kimoja kilichokuwa kimefanyika.
Vitu vyote viliumbwa kwa yeye, wala pasipo yeye hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa.
4 Ndani yake kulikuwa uzima, na huo uzima ulikuwa nuru ya wanadamu wote.
Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima na huo uzima ulikuwa nuru ya watu.
5 Nuru yang'aa gizani, wala giza halikuizimisha.
Nuru hungʼaa gizani nalo giza halikuishinda.
6 Palikuwa na mtu aliyetumwa kutoka kwa Mungu, ambaye jina lake alikuwa Yohana.
Alikuja mtu mmoja aliyetumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana.
7 Alikuja kama shahidi kushuhudia kuhusu ile nuru, ili kwamba wote waweze kuamini kupitia yeye.
Alikuja kama shahidi apate kuishuhudia hiyo nuru, ili kwa kupitia kwake watu wote waweze kuamini.
8 Yohana hakuwa ile nuru, bali alikuja ili ashuhudie kuhusu ile nuru
Yeye mwenyewe hakuwa ile nuru, bali alikuja kuishuhudia hiyo nuru.
9 Hiyo ilikuwa nuru ya kweli ambayo ilikuwa inakuja katika dunia nayo humtia nuru kila mmoja
Kwamba nuru halisi, imwangaziayo kila mtu ilikuwa inakuja ulimwenguni.
10 Alikuwa katika dunia, na dunia iliumbwa kupitia yeye, na dunia haikumjua.
Huyo Neno alikuwako ulimwenguni na ingawa ulimwengu uliumbwa kupitia kwake, haukumtambua.
11 Alikuja kwa vitu vyake, na watu wake hawakumpokea.
Alikuja kwa walio wake, lakini wao hawakumpokea.
12 Bali kwa wale wengi waliompokea, ambao waliamini jina lake, kwa hao aliwapa haki ya kuwa wana wa Mungu,
Bali wote waliompokea, aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake.
13 Ambao walizaliwa, sio kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili, wala kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu mwenyewe.
Hawa ndio wasiozaliwa kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali kwa mapenzi ya Mungu.
14 Naye Neno alifanyika mwili na akaishi miongoni mwetu, tumeuona utukufu wake, utukufu kama wa mtu pekee wa kipekee aliyekuja kutoka kwa Baba, amejaa neema na kweli.
Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli.
15 Yohana alishuhudia kuhusu yeye, na alipaza sauti akisema, “Huyu ndiye ambaye nilisema habari zake nikisema, “Yule ajaye baada yangu ni mkuu kuliko mimi, kwa sababu amekuwako kabla yangu.”
Yohana alishuhudia habari zake, akapaza sauti, akisema, “Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuniliko mimi, kwa kuwa alikuwepo kabla yangu.’”
16 Kwa kuwa kutoka katika utimilifu wake, sisi sote tumepokea bure kipawa baada ya kipawa.
Kutokana na ukamilifu wake, sisi sote tumepokea neema juu ya neema.
17 Kwa kuwa sheria ililetwa kupitia Musa. Neema na kweli vilikuja kupitia Yesu Kristo.
Kwa kuwa sheria ilitolewa kwa mkono wa Mose, lakini neema na kweli imekuja kupitia Yesu Kristo.
18 Hakuna mwanadamu aliyemwona Mungu wakati wowote. Mtu pekee ambaye ni Mungu, aliye katika kifua cha Baba, amemfanya yeye ajulikane.
Hakuna mtu yeyote aliyemwona Mungu wakati wowote, ila ni Mungu Mwana pekee, aliye kifuani mwa Baba ndiye ambaye amemdhihirisha.
19 Na huu ndio ushuhuda wa Yohana wakati makuhani na walawi waliotumwa kwake na Wayahudi kumwuliza, “Wewe ni nani?”
Huu ndio ushuhuda wa Yohana wakati Wayahudi walipowatuma makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu kumuuliza, “Wewe ni nani?”
20 Bila kusitasita na hakukana, bali alijibu, “Mimi sio Kristo.”
Yohana alikiri waziwazi pasipo kuficha akasema, “Mimi si Kristo.”
21 Hivyo wakamuuliza, “kwa hiyo wewe ni nani sasa?” Wewe ni Eliya? Akasema, “Mimi siye.” Wakasema, Wewe ni nabii? Akajibu,” Hapana.”
Wakamuuliza, “Wewe ni nani basi? Je, wewe ni Eliya?” Yeye akajibu, “Hapana, mimi siye.” “Je, wewe ni yule Nabii?” Akajibu, “Hapana.”
22 Kisha wakamwambia, “Wewe ni nani, ili kwamba tuwape jibu waliotutuma”? Wajishuhudiaje wewe mwenyewe?”
Ndipo wakasema, “Basi tuambie wewe ni nani ili tupate jibu la kuwapelekea wale waliotutuma. Wewe wasemaje juu yako mwenyewe?”
23 Akasema, “Mimi ni sauti yake aliaye nyikani: 'Inyosheni njia ya Bwana,' kama nabii Isaya alivyosema.”
Akawajibu kwa maneno ya nabii Isaya, akisema, “Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, ‘Yanyoosheni mapito ya Bwana.’”
24 Basi kulikuwa na watu wametumwa pale kutoka kwa Mafarisayo. Wakamuuliza na kusema,
Basi walikuwa wametumwa watu kutoka kwa Mafarisayo
25 “Kwa nini unabatiza basi kama wewe sio Kristo wala Eliya wala nabii?”
wakamuuliza, “Kama wewe si Kristo, wala si Eliya na wala si yule Nabii, kwa nini basi unabatiza?”
26 Yohana aliwajibu akisema, “Ninabatiza kwa maji. Hata hivyo, miongoni mwenu anasimama mtu msiyemtambua.
Yohana akawajibu, “Mimi ninabatiza kwa maji, lakini katikati yenu yupo mtu msiyemjua.
27 Huyu ndiye ajaye baada yangu. Mimi sisitahili kulegeza kamba za viatu vyake.”
Yeye ajaye baada yangu, sistahili hata kufungua kamba za viatu vyake.”
28 Mambo haya yalitendeka huko Bethania, ng'ambo ya Yordani, mahali ambapo Yohana alikuwa akibatiza.
Mambo haya yote yalitukia huko Bethania, ngʼambo ya Mto Yordani, mahali Yohana alipokuwa akibatiza.
29 Siku iliyofuata Yohana alimwona Yesu akija kwake akasema, “Tazama mwanakondoo wa Mungu aichukuae dhambi ya ulimwengu!
Siku iliyofuata, Yohana alimwona Yesu akimjia akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu!
30 huyu ndiye niliyesema habari zake nikisema, “Yeye ajaye nyuma yangu ni mkuu kuliko mimi, kwa kuwa alikuwa kabla yangu.'
Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Mtu anakuja baada yangu ambaye ni mkuu kuniliko mimi, kwa kuwa alikuwepo kabla yangu.’
31 Sikumtambua yeye, lakini ilifanyika hivyo ili kwamba afunuliwe katika Israeli, kwamba nilikuja nikibatiza kwa maji.”
Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini sababu ya kuja nikibatiza kwa maji ni ili yeye apate kufunuliwa kwa Israeli.”
32 Yohana alishuhudia, “Niliona Roho akishuka kutoka mbinguni mfano wa hua, na ilibaki juu yake.
Kisha Yohana akatoa ushuhuda huu: “Nilimwona Roho akishuka kutoka mbinguni kama hua, akakaa juu yake.
33 Mimi sikumtambua lakini yeye aliyenituma ili nibatize kwa maji aliniambia, 'yule ambaye utaona Roho akishuka na kukaa juu yake, Huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu.'
Mimi nisingemtambua, lakini yeye aliyenituma nibatize kwa maji alikuwa ameniambia, ‘Yule mtu utakayemwona Roho akimshukia na kukaa juu yake, huyo ndiye atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu.’
34 Nimeona na nimeshuhudia kwamba huyu ni Mwana wa Mungu.”
Mimi mwenyewe nimeona jambo hili na ninashuhudia kuwa huyu ndiye Mwana wa Mungu.”
35 Tena siku iliyofuata Yohana alikuwa amesimama pamoja na wanafunzi wake wawili,
Siku iliyofuata, Yohana alikuwa huko tena pamoja na wanafunzi wake wawili.
36 walimwona Yesu akitembea na Yohana akasema, “Tazama, Mwana kondoo wa Mungu!”
Alipomwona Yesu akipita, akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu!”
37 Wanafunzi wawili walimsikia Yohana akisema haya wakamfuata Yesu.
Wale wanafunzi wawili walipomsikia Yohana akisema haya, wakamfuata Yesu.
38 Tena Yesu aligeuka na kuwaona wanafunzi wale wakimfuata, na akawambia, “Mnataka nini?” Wakajibu, “Rabbi, (maana yake 'mwalimu,' unaishi wapi?”
Yesu akageuka, akawaona wakimfuata akawauliza, “Mnataka nini?” Wakamwambia, “Rabi,” (maana yake Mwalimu), “Unaishi wapi?”
39 Akawambia, “Njooni na mwone.”Kisha walikwenda na kuona mahali alipokuwa akiishi; walikaa pamoja naye siku hiyo, kwa kuwa ilikuwa yapata kama saa kumi hivi.
Yesu akawajibu, “Njooni, nanyi mtapaona!” Hivyo wakaenda na kupaona mahali alipokuwa anaishi, wakakaa naye siku ile, kwa kuwa ilikuwa yapata saa kumi.
40 Mmoja wa wale wawili waliomsikia Yohana akiongea na kisha kumfuata Yesu alikuwa ni Andrea, ndugu yake Simoni Petro.
Andrea nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliosikia yale Yohana aliyokuwa amesema, naye ndiye alimfuata Yesu.
41 Akamwona ndugu yake Simoni na akamwambia, “Tumempata Masihi” (ambayo inatafsiriwa Kristo).
Kitu cha kwanza Andrea alichofanya ni kumtafuta Simoni nduguye na kumwambia, “Tumemwona Masiya” (yaani, Kristo).
42 Akamleta kwa Yesu. Yesu akamtazama na akasema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohana” utaitwa Kefa,” (maana yake 'Petro').
Naye akamleta kwa Yesu. Yesu akamwangalia na kusema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohana. Utaitwa Kefa” (ambalo limetafsiriwa Petro).
43 Siku iliyofuata wakati Yesu alipotaka kuondoka kwenda Galilaya, alimpata Filipo na akamwambia, “Nifuate mimi.”
Siku iliyofuata Yesu aliamua kwenda Galilaya. Akamkuta Filipo, akamwambia, “Nifuate.”
44 Filipo alikuwa ni mwenyeji wa Bethsaida, mji wa Andrea na Petro.
Basi Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji alikotoka Andrea na Petro.
45 Filipo alimpata Nathanaeli na kumwambia, Tumempata yule ambaye Musa aliandika habari zake katika sheria na Manabii. Yesu mwana wa Yusufu, kutoka Nazareti.
Filipo naye akamkuta Nathanaeli na kumwambia, “Tumemwona yeye ambaye Mose aliandika habari zake katika Sheria na ambaye pia manabii waliandika kumhusu, yaani, Yesu wa Nazareti, mwana wa Yosefu.”
46 Nathanaeli akamwambia, “Je kitu chema chaweza kutokea Nazareti?” Filipo akamwambia, Njoo na uone.”
Nathanaeli akauliza, “Nazareti! Je, kitu chochote chema chaweza kutoka Nazareti?” Filipo akamwambia, “Njoo uone.”
47 Yesu akamwona Nathanaeli akija kwake na akasema, “Tazama, Mwisraeli kweli kweli asiye na udanganyifu ndani yake!”
Yesu alipomwona Nathanaeli anakaribia, akanena habari zake akasema, “Tazama huyu ni Mwisraeli kweli kweli; hana hila ndani yake.”
48 Nathanaeli akamwambia, “Umenifahamuje mimi?” Yesu akajibu na akamwambia, “Kabla Filipo hajakuita ulipokuwa chini ya mtini, nalikuona.”
Nathanaeli akamuuliza, “Umenifahamuje?” Yesu akamjibu, “Nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini, kabla hata Filipo hajakuita.”
49 Nathanaeli akajibu, “Rabi wewe u Mwana wa Mungu! Wewe ni Mfalme wa Israeli”!
Nathanaeli akamwambia, “Rabi, wewe ni Mwana wa Mungu! Wewe ni Mfalme wa Israeli!”
50 Yesu akajibu akamwambia, Kwa sababu nilikuambia 'nilikuona chini ya mtini' je waamini? utaona matendo makubwa kuliko haya.”
Yesu akamwambia, “Unaamini kwa kuwa nilikuambia nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini? Basi utaona mambo makuu zaidi kuliko hilo.”
51 Yesu akasema, “Amini amini nawambieni mtaziona mbingu zikifunguka, na kuwaona malaika wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”
Ndipo akawaambia, “Amin, amin nawaambia, ninyi mtaona mbingu ikifunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”