< Ayubu 6 >
1 Kisha Ayubu akajibu na kusema,
Kisha Ayubu akajibu:
2 “Oo, laiti maumivu yangu makubwa yangepimwa; laiti misiba yangu yote mikubwa ingewekwa kwenye mizani!
“Laiti uchungu wangu ungeweza kupimwa, nayo taabu yangu yote ingewekwa kwenye mizani!
3 Kwa kuwa sasa ungekuwa mzito kuliko mchanga wa baharini. Kwa sababu hiyo maneno yangu yamekuwa ya haraka.
Kwa kuwa hakika ingekuwa nzito kuliko mchanga wa bahari zote, kwa hiyo si ajabu maneno yangu yamekuwa ya haraka.
4 Kwa kuwa mishale ya Mwenyezi ipo ndani yangu, moyo wangu umelewa sumu; Vitisho vya Mungu vimejipanga vyenyewe dhidi yangu.
Mishale ya Mwenyezi iko ndani yangu, roho yangu inakunywa sumu yake; vitisho vya Mungu vimejipanga dhidi yangu.
5 Je punda mwitu hulia akiwa na malisho? Au ng'ombe huwa dhaifu wakati wa njaa ambapo anachakula?
Je, punda-mwitu hulia akiwa na majani, au ngʼombe dume hulia akiwa na chakula?
6 Je inawezekana kitu kisicho na ladha kulika bila chumvi? Au kuna radha yoyote katika ute mweupe wa yai?
Je, chakula kisicho na ladha huliwa bila chumvi, au upo utamu katika ute mweupe wa yai?
7 Nakataa kuvigusa; kwangu mimi vinafanana na chakula kichukizacho.
Ninakataa kuvigusa; vyakula vya aina hii hunichukiza.
8 Oo, kama nigeweza kupata haja yangu; oo, kama Mungu angeridhia jambo nilitamanilo sana:
“Laiti ningepata haja yangu, kwamba Mungu angenijalia hilo nililotarajia,
9 kama Mungu ingempendeza kuniangamiza mara moja, kwamba angeulegeza mkono wake na kuyakatilia mbali maisha yangu!
kwamba Mungu angekuwa radhi kuniponda, kuuachia mkono wake na kunikatilia mbali!
10 Hii ingeweza kuwa faraja yangu hata sasa - hata kama nafurahia sana maumivu yasiyopungua: kwa kuwa sikuyakana maneno yake Mtakatifu.
Ndipo bado ningekuwa na hii faraja, furaha yangu katika maumivu makali: kwamba sikuwa nimeyakana maneno yake yeye Aliye Mtakatifu.
11 Nguvu yangu ni ipi, hata nijaribu kusubiri? Mwisho wangu ni upi, utakao refusha maisha yangu?
“Ninazo nguvu gani, hata niendelee kutumaini? Matazamio yangu ya mbele ni nini, hata niendelee kuwa mvumilivu?
12 Je nguvu zangu ni nguvu za mawe? Au mwili wangu umeumbwa kwa shaba nyeusi?
Je, mimi nina nguvu za jiwe? Je, mwili wangu ni shaba?
13 Je si kweli kwamba sina msaada ndani yangu, na kwamba hekima imeondolewa mbali nami?
Je, ninao uwezo wowote wa kujisaidia mimi mwenyewe, wakati ambapo mafanikio yamefukuziwa mbali nami?
14 Kwa mtu ambaye yu karibu kuzirai, inapasa uaminifu uonyeshwe na rafiki zake; hata kwake yeye aachaye kumcha Mwenyezi.
“Mtu anayekata tamaa angetazamia moyo wa kujitoa wa rafiki zake, hata kama akiacha uchaji wa Mwenyezi.
15 Lakini ndugu zangu wamekuwa waaminifu kwangu kama mkondo wa maji jangwani, mfano wa mifereji ya maji ipitayo mpaka pasipo kitu,
Lakini ndugu zangu sio wa kutegemewa, ni kama vijito vya msimu, ni kama vijito ambavyo hufurika
16 ambayo imekuwa mieusi kwa sababu ya barafu juu yake, na kwa sababu ya theluji ambayo hujificha yenyewe ndani yake.
wakati vimefunikwa barafu iyeyukayo, ambavyo hujazwa na theluji inayoyeyuka,
17 Wakati zikiyeyuka, hutoweka; kukiwa na joto, hutoweka mahali hapo.
lakini hukauka majira ya ukame, na wakati wa hari hutoweka katika mikondo yake.
18 Misafara ambayo husafiri kwa njia yao hugeuka na maji; huzurura jangwani na kisha hupotea.
Misafara hugeuka kutoka njia zake; hukwea kwenda kwenye nchi ya ukiwa na kuangamia.
19 Misafara kutoka Tema huitazama, wakati majeshi ya Sheba huitarajia.
Misafara ya Tema inatafuta maji, wafanyabiashara wa Sheba wanaosafiri hutazama kwa matarajio.
20 Wamevunjika moyo kwa sababu walitumaini kupata maji. Wakaenda huko, lakini walidanganywa.
Wamedhikika, kwa sababu walikuwa na matumaini; wanafika huko, lakini wanahuzunika kwa kukosa walichotarajia.
21 Kwa sasa ninyi rafiki si kitu kwangu; mmeona hali yangu ya kutisha nanyi mwaogopa.
Sasa nanyi mmethibitika kwamba hamna msaada wowote; mnaona jambo la kutisha, nanyi mnaogopa.
22 Je nilisema kwenu, 'Nipeni kitu furani?' Au, 'nitoleeni zawadi katika mali zenu?'
Je, nimewahi kusema, ‘Toeni kitu kwa ajili yangu, au mnilipie fidia kutoka mali zenu,
23 Au, 'Niokoeni toka mkononi mwa mtesi wangu?' Au, 'Nitoleeni fidia kwa watesi wangu?'
au niokoeni mikononi mwa adui, au nikomboeni kutoka makucha ya wasio na huruma’?
24 Nifundishe, nami nitaishika amani yangu; nifanye nifahamu wapi nilipokosea.
“Nifundisheni, nami nitanyamaza kimya; nionyesheni nilikokosea.
25 Jinsi gani maneno ya kweli yanavyo umiza! Lakini hoja zenu, jee hasa zimenionya nini mimi?
Tazama yalivyo ya kuumiza maneno ya kweli! Lakini mabishano yenu yanathibitisha nini?
26 Je mnapanga kuyakemea maneno yangu, mnayachukulia maneno ya mtu mwenye kukata tamaa sawa na upepo?
Je, mna maana ya kuyasahihisha ninayosema, na kuyafanya maneno ya mtu anayekata tamaa kama upepo?
27 Hasa, mna piga kura kwa ajili ya yatima, na kupatana bei juu ya rafiki yenu kama bidhaa.
Mngeweza hata kupiga kura kwa ajili ya yatima, na kubadilishana rafiki yenu na mali.
28 Sasa, kwa sababu hiyo, tafadhari nitazame, kwa hakika sitasema uongo usoni penu.
“Lakini sasa kuweni na huruma mkaniangalie mimi. Je, ningeweza kusema uongo mbele zenu?
29 Rudini, nawasihi; lisiwepo neno la uonevu na nyinyi; Hasa, rudini, sababu zangu ni za haki.
Tulizeni hasira, msiwe wadhalimu; angalieni tena, kwa maana nimehatarisha uadilifu wangu.
30 Je mna uovu ulimini mwangu? Je kinywa changu hakiwezi kungundua madhara?
Je, pana uovu wowote midomoni mwangu? Je, kinywa changu hakiwezi kupambanua hila?