< Ayubu 38 >
1 Ndipo Yahweh alimwita Ayubu kutoka katika dhoruba kali na kumwambia,
Kisha Bwana akamjibu Ayubu kutoka upepo wa kisulisuli. Akasema:
2 “Huyu ni nani aletaye giza katika mipango kwa njia ya maneno bila maarifa?
“Nani huyu atiaye mashauri yangu giza kwa maneno yasiyo na maarifa?
3 Basi sasa jifunge kiunoni mwako kama mwanaume kwa kuwa nitakuuliza maswali, nawe lazima unijibu.
Jikaze kama mwanaume; nitakuuliza swali, nawe unijibu.
4 Wewe ulikuwa wapi wakati nilipoitandaza misingi ya dunia? Niambie, kama unao ufahamu zaidi.
“Ulikuwa wapi nilipoweka misingi ya dunia? Niambie, kama unafahamu.
5 Je ni nani aliyeamuru vipimo vyake? Niambie, kama unajua, ni nani alivinyosha vipimo juu yake?
Ni nani aliyeweka alama vipimo vyake? Hakika wewe unajua! Ni nani aliyenyoosha kamba ya kupimia juu yake?
6 Misingi yake ilitandazwa juu ya nini? Ni nani aliyeliweka jiwe lake la pembeni
Je, misingi yake iliwekwa juu ya nini, au ni nani aliyeweka jiwe la pembeni,
7 wakati nyota za asubuhi zilipoimba pamoja na wana wote wa Mungu walipopiga kelele kwa furaha?
wakati nyota za asubuhi zilipoimba pamoja, na malaika wote walipokuwa wakipiga kelele kwa furaha?
8 Ni nani huifunga bahari kwa milango wakati inapofurika, kana kwamba inatoka katika tumbo,
“Ni nani aliyeifungia bahari milango ilipopasuka kutoka tumbo,
9 wakati nilipoyafanya mawingu kuwa ni mavazi yake, na giza nene kuwa mkanda wake wa kujifungia?
nilipoyafanya mawingu kuwa vazi lake, na kuyafungia katika giza nene,
10 Hapo ilikuwa wakati nilipoweka bahari mpaka wangu, na nilipoweka makomeo yake na milango,
nilipoamuru mipaka yake, na kuiweka milango yake na makomeo mahali pake,
11 na wakati nilipoiambia, 'Unaweza kuja hapa kutoka mbali, lakini si zaidi; na hapa ndipo nitauweka mpaka kwa fahari ya mawimbi yako.'
niliposema, ‘Unaweza kufika mpaka hapa wala si zaidi; hapa ndipo mawimbi yako yenye kiburi yatakapokomea’?
12 Je tangu mwanzo wa siku zako, ulishawahi kuigiza asubuhi ianze, na kuyafanya mapambazuko yajue sehemu yake katika mpangilio wa vitu,
“Umepata kuiamrisha asubuhi ipambazuke, au kuyaonyesha mapambazuko mahali pake,
13 ili kwamba ishikilie sehemu za dunia ili watu waovu watikiswe mbali nayo.
yapate kushika miisho ya dunia, na kuwakungʼuta waovu waliomo?
14 Dunia imebadilishwa katika mwonekano kama udongo unavyobadilika chini ya muhuri; vitu vyote husimama juu yake dhahiri kama cha kibindo cha nguo.
Dunia hubadilika kama udongo wa mfinyanzi chini ya lakiri; sura yake hukaa kama ile ya vazi.
15 'Mwanga' wao umeondolewa kutoka kwa watu waovu; na mkono wao ulioinuliwa umevunjwa.
Waovu huzuiliwa nuru yao, nao mkono wao ulioinuliwa huvunjwa.
16 Je umeshaenda kwenye vyanzo vya maji ya bahari? Je umeshatembea sehemu za chini kabisa za kilindi?
“Je, umepata kufika kwenye chemchemi za bahari? Au kutembea mahali pa ndani pa vilindi?
17 Je malango ya mauti yamefunuliwa kwako? Je umeshaona malango ya uvuli wa mauti?
Umewahi kuonyeshwa malango ya mauti? Umewahi kuiona milango ya uvuli wa mauti?
18 Je umeifahamu dunia katika upana wake? Niambie kama unayajua yote hayo.
Je, wewe unafahamu ukubwa wa dunia? Niambie kama unajua haya yote.
19 Je iko wapi njia ya sehemu ya kupumzikia kwa mwanga, na kama ilivyo kwa giza, iko wapi sehemu yake?
“Njia ya kufika kwenye makao ya nuru ni ipi? Nako maskani mwa giza ni wapi?
20 Je unaweza kuuongoza mwanga na giza katika sehemu zake za kazi? Waweza kuitambua njia ya kurudi katika nyumba zao?
Je, unaweza kuvirudisha kwenye makao yake? Unajua njia za kufika maskani mwake?
21 Bila shaka unajua, kwa kuwa ulizaliwa wakati huo; hesabu ya siku zako ni kubwa sana!
Hakika unajua, kwa kuwa ulikuwa umeshazaliwa! Kwani umeishi miaka mingi!
22 Je ulishaingia katika ghala ya barafu, au umeshaiona ghala ya mawe ya mvua,
“Je, umeshawahi kuingia katika ghala za theluji, au kuona ghala za mvua ya mawe,
23 vitu hivi nimeviweka kwa ajili ya siku za mateso, kwa siku za mapigano na vita?
ambazo nimeziweka akiba kwa ajili ya wakati wa taabu, na kwa ajili ya wakati wa vita na mapigano?
24 Je iko wapi njia ya mshindo wa mwanga hutokea au je upepo husambazwa kutoka mashariki juu ya dunia?
Ni ipi njia iendayo mahali umeme wa radi unapotawanyiwa, au mahali upepo wa mashariki unaposambaziwa juu ya dunia?
25 Ni nani aliyezitengeneza mifereji ya gharika ya mvua, au ni nani aliyezifanya njia za milipuko ya radi,
Ni nani aliyepasua mifereji kwa ajili ya maji mengi ya mvua yaendayo kasi na njia ya umeme wa radi,
26 na kuifanya mvua inyeshe juu ya nchi ambazo hakuna mtu aishiye ndani yake, na juu ya jangwa, ambayo ndani yake hakuna mtu yeyote,
ili kusababisha mvua kunyeshea mahali pasipokaliwa na mtu, jangwa lisilo na yeyote ndani yake,
27 kwa kusudi la kutimiza mahitaji ya mikoa iliyo kame na yenye ukiwa, na kuyastawisha majani mororo?
ili kuitosheleza nchi ya ukiwa na jangwa, na majani yaanze kumea ndani yake?
28 Je kuna baba wa mvua? Ni nani aliyeyafanya matone ya umande?
Je, mvua ina baba? Ni nani baba azaaye matone ya umande?
29 Je barafu ilitoka katika tumbo la nani? Na ni nani aliyeizaa theluji nyeupe katika anga?
Barafu inatoka tumbo la nani? Ni nani azaaye ukungu kutoka mbinguni,
30 Maji hujificha menyewe na kuwa kama jiwe; sehemu za juu za vilindi huwa kama barafu.
wakati maji yawapo magumu kama jiwe, wakati uso wa vilindi vya maji unapoganda?
31 Je unaweza kuzifunga minyororo ya Kilimia, au kuvifungua vifundo vya Orioni?
“Je, waweza kuufunga mnyororo wa Kilimia? Waweza kulegeza kamba za Orioni?
32 Je unaweza kuziongoza nyota kutokea katika nyakati zake? Je waweza kuongoza dubu pamoja na watoto wake?
Waweza kuyaongoza makundi ya nyota kwa majira yake, au kuongoza Dubu na watoto wake?
33 Je unazijua sheria za anga? Wewe uliweza kuanzisha sheria za anga juu ya dunia?
Je, unajua sheria zinazotawala mbingu? Waweza kuweka utawala wa Mungu duniani?
34 Je waweza kupaza sauti yako hadi mawinguni, ili kwamba maji mengi ya mvua yakufunike?
“Waweza kuiinua sauti yako mpaka mawinguni, na kujifunika mwenyewe na gharika ya maji?
35 Je waweza kuagiza miali ya mwanga ili itokee, na kukwambia, 'Sisi tupo hapa'?
Je, wewe hutuma umeme wa radi kwenye njia zake? Je, hutoa taarifa kwako kukuambia, ‘Sisi tuko hapa’?
36 Ni nani ameweka hekima katika mawingu au ni nani ameweka ufahamu kwa ukungu?
Ni nani aliyeujalia moyo hekima au kuzipa akili ufahamu?
37 Nani anaweza kuyahesabu mawingu kwa maarifa yake? Na ni nani awezaye kuvimwaga viriba vya anga
Nani mwenye hekima ya kuyahesabu mawingu? Ni nani awezaye kuinamisha magudulia ya mbinguni
38 wakati mavumbi yanapoungana kuwa kitu kigumu na mabonge ya dunia yanaposhikama kwa pamoja?
wakati mavumbi yawapo magumu, na mabonge ya udongo kushikamana pamoja?
39 Je waweza kuwinda mawindo kwa ajili ya simba jike au kutosheleza hamu ya watoto wadogo wa simba
“Je, utamwindia simba jike mawindo, na kuwashibisha simba wenye njaa
40 wakati wanapokwaruza kwaruza katika pango lao na kukaa katika kificho ili kulala katika hali ya kuvizia?
wakati wao wamejikunyata mapangoni mwao, au wakivizia kichakani?
41 Ni nani aletaye mawindo kwa ajili ya kunguru wakati ambapo watoto wao wanapomlilia Mungu na kutangatanga kwa kukosa chakula?
Ni nani ampaye kunguru chakula wakati makinda yake yanamlilia Mungu, yakizungukazunguka kwa ajili ya kukosa chakula?