< Ayubu 34 >
1 Zaidi ya hayo, Elihu aliendelea kusema:
Kisha Elihu akasema:
2 “Sikilizeni maneno yangu, ninyi watu wenye hekima; nisikieni, ninyi mlio na maarifa.
“Sikieni maneno yangu, enyi watu wenye hekima; nisikilizeni mimi, ninyi watu wenye maarifa.
3 Kwa kuwa sikio huyajaribu maneno kama ambavyo kaakaa huonja chakula.
Kwa kuwa sikio huyajaribu maneno kama vile ulimi uonjavyo chakula.
4 Na tujichagulie sisi wenyewe yale yenye adili: na tujigundulie miongoni mwetu yale yaliyo mazuri.
Tujichagulie wenyewe yaliyo sawa, nasi tujifunze pamoja yaliyo mema.
5 Kwa kuwa Ayubu amesema, 'mimi ni mwenye haki, lakini Mungu ameondoa haki zangu.
“Ayubu anasema, ‘Mimi sina hatia, lakini Mungu ameninyima haki yangu.
6 Pamoja na haki zangu, ninaangaliwa kama mwongo. Kidonda changu hakiponyeki, ingawa mimi sina dhambi.'
Ingawa niko sawa, ninaonekana mwongo; nami ingawa sina kosa, kidonda changu hakiponi.’
7 Ni mtu gani aliye kama Ayubu ambaye hunywa dharau kama maji,
Ni mtu gani aliye kama Ayubu, anywaye dharau kama maji?
8 ambaye huzunguka katika ushirika wa watu ambao ni waovu, na ambaye hutembea pamoja na watu waovu?
Ashirikianaye na watenda mabaya na kuchangamana na watu waovu.
9 Kwa kuwa anasema, ' Hakuna faida kwa mtu kujifurahisha kwa kufanya mambo ambayo Mungu anayataka.'
Kwa kuwa anasema, ‘Haimfaidi mwanadamu kitu chochote anapojitahidi kumpendeza Mungu.’
10 Basi nisikilizeni mimi, enyi watu wenye ufahamu: na iwe mbali na Mungu kwamba atatenda uovu;
“Hivyo nisikilizeni mimi, ninyi watu wenye ufahamu. Kamwe Mungu hatendi uovu, Mwenyezi hafanyi kosa.
11 na iwe mbali na Mwenye enzi kwamba atatenda dhambi. Kwa kuwa humlipa mtu kutokana na kazi yake; na humfanya mtu apate thawabu za njia zake mwenyewe.
Humlipa mwanadamu kwa ajili ya lile alilotenda; huleta juu yake kile ambacho matendo yake yanastahili.
12 Kwa hakika, Mungu hatendi uovu, wala Mwenye nguvu hajaIpotosha haki.
Ni jambo lisiloweza kufikiriwa kwamba Mungu angefanya makosa, kwamba Mwenyezi angepotosha hukumu.
13 Ni nani aliyemweka kuwa mtawala wa dunia? Ni nani aliyeiweka dunia yote chini yake?
Je, ni nani aliyemtawaza juu ya dunia? Ni nani aliyemweka kuwa mwangalizi wa ulimwengu wote?
14 Ikiwa aliweka makusudio yake juu yake mwenyewe, na kama amejikusanyia mwenyewe nafsi yake na pumzi yake,
Kama lilikuwa kusudi la Mungu, naye akaiondoa Roho yake na pumzi yake,
15 basi miili yote itateketea pamoja; mwanadamu angerudi mavumbini tena.
wanadamu wote wangeliangamia kwa pamoja, na mtu angerudi mavumbini.
16 Kama sasa mna ufahamu, sikilizeni haya; sikilizeni sauti ya maneno yangu.
“Kama ninyi mnaufahamu, sikieni hili; sikilizeni hili nisemalo.
17 Je yeye anayeichukia haki aweza kutawala? Je mtamhukumu Mungu kuwa ni mwenye makosa, ambaye ni mwenye haki na mwenye nguvu?
Je, yeye aichukiaye haki aweza kutawala? Je, utamhukumu mwenye haki, Aliye na Nguvu Zote?
18 Mungu ambaye humwambia mfalme, ' Wewe ni mbaya; au huwaambia wenye kuheshimiwa, 'Ninyi ni waovu'?
Je, si ni yeye awaambiaye wafalme, ‘Ninyi hamfai kitu,’ nao watu mashuhuri, ‘Ninyi ni waovu,’
19 Mungu ambaye haoneshi upendeleo kwa viongozi na ambaye hawakubali zaidi watu matajiri kuliko masikini, kwa kuwa wote ni kazi ya mikono yake.
yeye asiyependelea wakuu, wala haonyeshi upendeleo kwa matajiri kuliko maskini, kwa kuwa wote ni kazi ya mikono yake?
20 Watakufa kwa muda mfupi; wakati wa usiku watu watatikiswa na watapita; watu wenye nguvu watatwaliwa mbali, lakini si kwa mikono ya wanadamu.
Wanakufa ghafula, usiku wa manane; watu wanatikiswa nao hupita; wenye nguvu huondolewa bila mkono wa mwanadamu.
21 Kwa kuwa macho ya Mungu yako juu ya njia za mtu; anaziona hatua zake zote.
“Macho yake yanazitazama njia za wanadamu; anaona kila hatua yao.
22 Hakuna giza, wala hakuna weusi mzito ambao watenda mabaya wanaweza kujificha wao wenyewe.
Hakuna mahali penye giza nene, wala uvuli mkubwa, ambapo watenda mabaya wanaweza kujificha.
23 Kwa kuwa Mungu hahitaji kumchunguza mtu zaidi; wala hakuna haja kwa mtu yeyote kwenda mbele zake kwa hukumu.
Mungu hana haja ya kumchunguza mtu sana, ili apate kuja mbele zake kwa hukumu.
24 Huwavunja vipande vipande watu wenye nguvu kwa ajili ya njia zao ambazo hazihitaji uchunguzi zaidi; huwaweka watu wengine katika nafasi zao.
Bila kuuliza huwapondaponda wenye nguvu nyingi na kuwaweka wengine mahali pao.
25 Kwa namna hii ana maarifa juu ya matendo yao; huwatupa watu hawa wakati wa usiku; nao wameangamizwa.
Kwa sababu huyaangalia matendo yao yote, huwaondoa usiku, nao wakaangamia.
26 Huwaua kwa matendo yao mabaya kama wakosaji dhahiri mbele za watu wengine
Anawaadhibu kwa ajili ya uovu wao mahali ambapo kila mmoja ataweza kuwaona,
27 kwasababu wamegeuka na kuacha kumfuata yeye na wamekataa kuzisadiki njia zake zozote.
kwa sababu wameacha kumfuata Mungu, nao hawakuiheshimu njia yake hata moja.
28 Na kwa namna hii, wamekifanya kilio cha watu masikini kimfikie; amekisikia kilio cha watu walioteswa.
Wamesababisha kilio cha maskini kifike mbele zake, hivyo akasikia kilio cha wahitaji.
29 Na wakati akaapo kimya, nani aweza kumhukumu kuwa mkosaji? Kama akiuficha uso wake, ni nani awezaye kumjua? Anatawala sawa sawa juu ya taifa na mtu pia,
Lakini kama akinyamaza kimya, ni nani awezaye kumhukumu? Kama akiuficha uso wake, ni nani awezaye kumwona? Ikiwa ni taifa au mtu mmoja, kwake ni sawa,
30 ili kwamba watu wasiomjua Mungu wasije wakatawala, ili kwamba asiwepo mtu wa kuwanasa watu.
ili kumzuia mtu mwovu kutawala, au wale ambao huwategea watu mitego.
31 Fikiria mtu akimwambia Mungu, ' Mimi ni mwenye hatia kabisa, lakini sitatenda dhambi tena;
“Kama mwanadamu akimwambia Mungu, ‘Nimekosa lakini sitatenda dhambi tena.
32 nifunze kile ambacho siwezi kukiona; nimetenda dhambi, lakini sitafanya tena.'
Nifundishe nisichoweza kuona; kama nimekukosea, sitafanya hivyo tena.’
33 Je unadhani kwamba Mungu ataiadhibu dhambi ya mtu huyo, kwa kuwa unayachukia yale ambayo Mungu huyatenda? Ni lazima uchague, siyo mimi. Basi sema yale ambayo unayajua.
Je basi, Mungu atakulipa kwa masharti yako, wakati wewe umekataa kutubu? Yakupasa wewe uamue, wala si mimi; sasa niambie lile ulijualo.
34 Watu wenye ufahamu wataniambia, kwa kweli, kila mtu mwenye hekima ambaye hunisikia atasema,
“Wanadamu wenye ufahamu husema, wenye hekima wanaonisikia huniambia,
35 Ayubu anazungumza bila maarifa; maneno yake hayana hekima.'
‘Ayubu huongea bila maarifa; maneno yake hayana busara.’
36 Kama Ayubu alijaribiwa kwa kitu kidogo kabisa katika kesi yake kwasababu ya kuongea kwake kama watu waovu.
Laiti Ayubu angejaribiwa hadi kikomo cha mwisho, kwa sababu anajibu kama mtu mwovu!
37 Kwa kuwa anaongeza uasi juu ya dhambi yake; anapiga makofi ya dharau kati yetu; anaweka maneno kinyume na Mungu.”
Kwenye dhambi yake huongeza uasi; kwa dharau hupiga makofi miongoni mwetu, na kuzidisha maneno yake dhidi ya Mungu.”