< Ayubu 32 >

1 Hivyo hawa watu watatu walikoma kumjibu Ayubu kwasababu alikuwa ni mwenye haki katika macho yake mwenyewe.
Basi watu hawa watatu wakaacha kumjibu Ayubu, kwa kuwa alikuwa mwadilifu machoni pake mwenyewe.
2 Ndipo iliwaka hasira ya Elihu mwana wa Barakeli Mbuzi, wa familia ya Ramu, iliwaka dhidi ya Ayubu kwa kuwa alijihesabia haki mwenyewe kuliko Mungu.
Lakini Elihu mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi wa jamaa ya Ramu, akamkasirikia sana Ayubu, kwa sababu ya kujihesabia haki mwenyewe badala ya Mungu.
3 Hasira ya Elihu iliwaka pia kinyume cha marafiki zake watatu kwasababu hawakupata jibu kwa ajili ya Ayubu, na bado walimhukumu Ayubu.
Pia aliwakasirikia hao rafiki watatu wa Ayubu, kwa sababu hawakuweza kupata njia ya kuthibitisha ya kuwa hayo maneno ya Ayubu hayakuwa ya kweli, nao bado walikuwa wamemlaumu.
4 Sasa Elihu alikuwa amemsubiri Ayubu ili aweze kuzungumza naye kwa kuwa watu wengine walikuwa wakubwa kuliko yeye.
Basi Elihu alikuwa amesubiri kwanza waongee na Ayubu kwa sababu walikuwa na umri mkubwa kumliko yeye.
5 Hata hivyo, wakati Elihu alipoona ya kuwa hapakuwa na jibu katika midomo ya watu hawa watatu, hasira yake iliwaka.
Lakini alipoona watu hao watatu hawakuwa na kitu zaidi cha kusema, hasira yake ikaamka.
6 Ndipo Elihu mwana wa Barakeli Mbuzi alinena na kusema, “Mimi ni mdogo, na ninyi ni wazee. Hii ndio sababu nilijizuia na sikuthubutu kuzungumza mawazo yangu mwenyewe.
Basi Elihu mwana wa Barakeli wa kabila la Buzi akasema: “Mimi ni mdogo kwa umri, nanyi ni wazee; ndiyo sababu niliogopa, sikuthubutu kuwaambia kile ninachojua.
7 Nilisema, “Urefu wa siku utazungumza; na wingi wa miaka utatufundisha hekima.
Nilifikiri, ‘Yafaa umri useme, nao wingi wa miaka ungefundisha hekima.’
8 Lakini kuna roho ndani ya mtu; pumzi ya Mwenye nguvu humpa yeye ufahamu.
Lakini ni Roho iliyoko ndani ya mwanadamu, pumzi ya Mwenyezi, ndiyo impayo yeye ufahamu.
9 Si tu watu wakubwa ndio wenye hekima, wala watu wazee pekee ambao hufahamu haki.
Sio wazee peke yao walio na hekima, sio wenye umri mkubwa peke yao wanaofahamu lililo sawa.
10 Hivyo basi nakwambia wewe, “Nisikilizeni mimi; Nitakwambia pia uelewa wangu.'
“Kwa hiyo nasema: Nisikilizeni mimi; mimi nami nitawaambia lile ninalojua.
11 Tazama, niliyasubiria maneno yenu; nilisikiliza hoja zenu wakati mlipokuwa mnafikiri juu ya kile cha kusema.
Nilingojea mlipokuwa mnaongea, nilizisikiliza hoja zenu; mlipokuwa mkitafuta maneno ya kusema,
12 Hakika, niliwajali sana ninyi, lakini, tazama, hakuna hata mmoja wenu aliyeweza kumshawishi Ayubu wala ambaye aliweza kumjibu maneno yake.
niliwasikiliza kwa makini. Lakini hakuna hata mmoja wenu aliyethibitisha kwamba Ayubu amekosa; hakuna hata mmoja wenu aliyeweza kujibu hoja zake.
13 Iweni waangalifu msije mkasema, 'Tumepata hekima!' Mungu atakuwa amemshinda Ayubu; mtu wa kawaida hawezi akafanya hivyo.
Msiseme, ‘Tumepata hekima; Mungu na amthibitishe kuwa mwongo, wala si mwanadamu.’
14 Kwa kuwa Ayubu hajasema mojamoja maneno yake juu yangu, basi sitamjibu kwa maneno yenu.
Lakini Ayubu hajayapanga maneno yake dhidi yangu, nami sitamjibu kwa kutumia hoja zenu.
15 Hawa watu watatu wamep igwa bumbuwazi; hawawezi kuendelea kumjibu Ayubu; hawana neno zaidi la kusema.
“Wametiwa hofu na hawana la zaidi la kusema; maneno yamewaishia.
16 Je ninapaswa kusubiria kwasababu hawazungumzi, kwa kuwa wamesimama pale kimya na wala hawajibu zaidi?
Je, ningoje sasa kwa sababu wamekuwa kimya, kwa vile sasa wanasimama bila kuwa na la kujibu?
17 La, nitajibu pia upande wangu; Nitawaambia pia ufahamu wangu.
Mimi nami nitakuwa na la kusema; mimi nami nitasema lile nilijualo.
18 Kwa kuwa nimejawa na maneno mengi, roho ndani yangu inanisukuma.
Kwa kuwa nimejawa na maneno, nayo Roho iliyomo ndani yangu yanisukuma;
19 Tazama, kifua changu ni kama divai yenye chachu ambayo haina tundu; kama viriba vipya, kiko tayari kupasuka.
ndani yangu niko kama chupa iliyojazwa divai, kama kiriba kipya cha divai kilicho tayari kupasuka.
20 Nitazungumza ili kwamba niweze kuburudishwa; nitafungua kimya changu na kusema.
Ni lazima niseme ili niweze kutulia; ni lazima nifumbue midomo yangu nipate kujibu.
21 Sitaonesha upendeleo; wala sitatoa sifa za majina kwa mtu yeyote.
Sitampendelea mtu yeyote, wala sitajipendekeza kwa mtu yeyote;
22 Kwa kuwa sijui namna ya kutoa sifa; kama nitafanya hivyo, Muumba wangu atanikatilia mimi mbali.
kwa kuwa kama ningekuwa stadi wa kujipendekeza, Muumba wangu angeniondolea mbali kwa upesi.

< Ayubu 32 >