< Ayubu 31 >
1 Nimefanya patano na macho yangu; ni kwa namna gani tena napaswa kumtazama mwanamwali kwa tamaa?
“Nimefanya agano na macho yangu yasimtazame msichana kwa kumtamani.
2 Ni sehemu gani kutoka kwa Mungu juu, na urithi gani kutoka kwake mwenye nguvu aliye juu?
Kwa kuwa fungu la mwanadamu ni gani kutoka kwa Mungu juu, urithi wake kutoka kwa Mungu Mwenye Nguvu Aliye juu?
3 Nilikuwa nafikiri kwamba majanga ni kwa watu wasio na haki, na misiba ni kwa ajili ya watu watendao mabaya.
Je, si uharibifu kwa watu waovu, maangamizi kwa wale watendao mabaya?
4 Je Mungu hazioni njia zangu na kuzihesabu hatua zangu zote?
Je, yeye hazioni njia zangu na kuihesabu kila hatua yangu?
5 Kama nimetembea katika udanganyifu, kama mguu wangu umeharakisha katika uongo,
“Kama nimeishi katika uongo au mguu wangu umekimbilia udanganyifu,
6 na nipimwe katika vipimo vilivyo sawa ili kwamba Mungu aujue uadilifu wangu.
Mungu na anipime katika mizani za uaminifu, naye atajua kwamba sina hatia:
7 Kama hatua zangu zimegeuka kutoka katika njia sahihi, kama moyo wangu umetembea kwa kufuata macho yangu, na kama doa lolote la uchafu limeng'ang'ania katika mikono yangu,
kama hatua zangu zimepotoka kutoka kwenye njia, kama moyo wangu umeongozwa na macho yangu, au kama mikono yangu imetiwa unajisi,
8 na kisha mimi nipande na mtu mwingine na ale; mavuno na yang'olewe katika shamba langu.
basi wengine na wale nilichokipanda, nayo yale yote niliyootesha na yangʼolewe.
9 Na kama moyo wangu umevutiwa na mwanamke mwingine, ikiwa nimelala na mke wa jirani yangu katika hali ya kusubiria katika mlango wake,
“Kama moyo wangu umeshawishiwa na mwanamke, au kama nimevizia mlangoni mwa jirani yangu,
10 na ndipo mke wangu na asage nafaka kwa mwanaume mwingine, na wanaume wengine na walale naye.
basi mke wangu na asage nafaka ya mwanaume mwingine, nao wanaume wengine walale naye.
11 Na kwa hilo litakuwa ni kosa kubwa; kwa kweli, utakuwa ni uovu wa kuadhibiwa na waamuzi.
Kwa kuwa hilo lingekuwa aibu, naam, dhambi ya kuhukumiwa.
12 Kwa kuwa ni moto ambao unateketeza kila kitu kwa uharibifu, na kwamba utaunguza mavuno yangu yote.
Ni moto uwakao kwa Uharibifu; ungekuwa umengʼoa mavuno yangu.
13 Ikiwa nilikataa ombi la haki kutoka kwa watumishi wangu wa kiume na wa kike wakati walipohojiana nami,
“Kama ningewanyima haki watumishi wangu wanaume au vijakazi wangu, walipokuwa na manungʼuniko dhidi yangu,
14 kisha nini basi ningefanya wakati Mungu anapoinuka ili kunishitaki mimi? Atakapokuja kunihukumu, nitamjibuje?
nitafanya nini Mungu atakaponikabili? Nitamjibu nini nitakapoitwa kutoa hesabu?
15 Je yeye aliyenifanya mimi tumboni hakuwafanya wao pia? Je yeye si yeye yule aliyetuumba sisi wote katika tumbo?
Je, yeye aliyeniumba tumboni mwa mama yangu, si ndiye aliwaumba? Je, si ni yeye huyo mmoja aliyetuumba sote ndani ya mama zetu?
16 kama nimewanyima watu masikini matakwa yao, au kama nimesababisha macho ya wajane yafifie kwa kulia,
“Ikiwa nimewanyima maskini haja zao, au kuyaacha macho ya wajane yadhoofike,
17 au ikiwa kama nimekula kipande changu na sijawaruhusu wale wasio na baba kukila pia -
kama nimekula chakula changu mwenyewe, bila kuwashirikisha yatima;
18 kwasababu tangu ujana wangu yatima walikua pamoja nami kama kuwa na baba, nami nimemwongoza mama yake, mjane, tangu katika tumbo la mama yangu mwenyewe.
lakini tangu ujana wangu nimemlea yatima kama ambavyo baba angefanya, nami tangu kuzaliwa kwangu nimewaongoza wajane:
19 ikiwa nimemwona yeyote akiangamia kwa kwa kukosa mavazi, au kama nimemwona mtu mhitaji akiwa hana nguo;
kama nilimwona yeyote akiteseka kwa kukosa nguo, au mtu mhitaji asiye na mavazi
20 ikiwa moyo wake haujanibariki kwasababu amekuwa hajatiwa joto na sufu ya kondoo zangu,
ambaye wala moyo wake haukunibariki kwa kumpatia joto kwa mavazi ya manyoya ya kondoo zangu,
21 ikiwa nimeinua juu mkono wangu kinyume na watu wasio na baba kwa kuwa niliona msaada wangu katika lango la mji, na kisha kuleta mashitaka dhidi yangu.
na kama nimeinua mkono wangu dhidi ya yatima, nikijua kuwa nina ushawishi mahakamani,
22 Ndipo bega langu na lianguake kutoka katika sehemu yake, na mkono wangu uvunjike katika kiungo chake.
basi mkono wangu na unyofoke toka begani mwangu, nao na uvunjike kutoka kiungio chake.
23 Kwa kuwa niliogopa uharibifu kutoka kwa Mungu; kwasababu ya mawazo ya ukuu wake, nisingeweza kufanya mambo hayo.
Kwa kuwa niliogopa uharibifu kutoka kwa Mungu, nami kwa kuuogopa utukufu wake sikuweza kufanya mambo kama hayo.
24 Kama ningeifanya dhahabu kuwa tumaini langu, na kama ningesema kwa dhahabu safi, 'wewe unanifanya kuwa na tumaini';
“Kama nimeweka tumaini langu kwenye dhahabu, au kuiambia dhahabu safi, ‘Wewe ndiwe salama yangu,’
25 na kama nimefurahi kwasababu ya utajiri wangu ulikuwa mkubwa, kwa kuwa mkono wangu umepata mali nyingi, na kisha kuleta mashitaka dhidi yangu!
kama nimefurahia wingi wa utajiri wangu, ustawi ambao mikono yangu ilikuwa imepata,
26 Ikiwa nimeliona jua lilipowaka, au mwezi ukitembea katika mng'ao wake,
kama nimelitazama jua katika kungʼaa kwake au mwezi ukienda kwa fahari yake,
27 na kama moyo wangu umevutwa kwa siri, ili kwamba mdomo wangu umeubusu mkono wangu katika ibada yao -
hivyo moyo wangu kushawishiwa kwa siri, au kubusu mkono wangu kwa kuviheshimu,
28 hili nalo pia lingekuwa ni ubaya wa kuadhibiwa na waamuzi, kwa kuwa ningekuwa nimemkana Mungu aliyejuu.
basi hiyo pia ingekuwa dhambi ya kuhukumiwa, kwa kuwa ningekuwa si mwaminifu kwa Mungu aishiye juu sana.
29 Ikiwa nimefurahia uharibifu wa yeyote ambaye ananichukia mimi, au kuwapa hongera wakati majanga yanapowapata, ndipo ulete mashitaka dhidi yangu!
“Kama nimeshangilia msiba wa adui yangu, au kutazama kwa furaha taabu iliyomjia,
30 Kwa kweli sijauruhusu hata mdomo wangu kutenda dhambi kwa kuuomba uhai wake kwa laana.
lakini sikuruhusu kinywa changu kufanya dhambi kwa kuomba laana dhidi ya maisha yake;
31 Ikiwa watu wa hema yangu hawajasema,' Nani aweza kumpata mtu ambaye hayashibishwa na chakula cha Ayubu?
kama watu wa nyumbani mwangu kamwe hawakusema, ‘Ni nani ambaye hajashibishwa na nyama ya Ayubu?’
32 (hata mgeni hajawahi kukaa katika pembe ya mji, kwa kuwa siku zote nimefungua milango yangu kwa ajili ya wasafiri), na kama haiko hivyo, ndipo mlete mashitaka kinyume nami!
Lakini hakuna mgeni aliyelala njiani, kwa maana mlango wangu ulikuwa wazi kwa msafiri;
33 Ikiwa, kama binadamu nimezificha dhambi zangu kwa kuficha hatia ndani ya kanzu yangu -
kama nimeifunika dhambi yangu kama wanadamu wengine wafanyavyo, kwa kuficha hatia yangu moyoni mwangu,
34 kwa kuwa niliogopa kusanyiko kubwa, kwasababu ya matwezo ya familia yaliniogopesha, hivyo basi nilinyamaza kimya na sikuweza kwenda nje, basi nileteni mashitaka dhidi yangu!
kwa sababu ya kuogopa umati wa watu, na hivyo kuwa na hofu ya kudharauliwa na jamaa, nikanyamaza kimya nisitoke nje ya mlango:
35 Ee, kama nilikuwa na mtu wa kunisikiliza! Ona, hii ni saini yangu; na Mwenye nguvu na anijibu! Ikiwa nilikuwa na shitaka rasmi ambalo adui yangu ameliandika!
(“Laiti kama angekuwepo mtu wa kunisikia! Tazama sasa ninatia sahihi kwenye utetezi wangu: Mwenyezi na anijibu; mshtaki wangu na aweke mashtaka yake kwenye maandishi.
36 Hakika ningelibeba hadharani juu ya bega langu; ningeliweka juu kama taji.
Hakika ningeyavaa begani mwangu, ningeyavaa kama taji.
37 Ningemweleza hesabu ya hatua zangu; na kama mwana wa mfalme mwenye kujiamini ningepanda kwenda kwake.
Ningempa hesabu ya kila hatua yangu, ningemwendea kama mwana wa mfalme.)
38 Kama nchi yangu ingelia dhidi yangu, na matuta yake yaomboleza pamoja,
“Kama nchi yangu inalia dhidi yangu, na mifereji yake yote imelowana kwa machozi,
39 ikiwa nimekula mavuno yake bila kulipia au kama nimesababisha wamiliki wake kupoteza maisha yao,
kama nimekula mazao yake bila malipo, au kuvunja mioyo ya wapangaji wake,
40 ndipo miiba na iote badala ya ngano na magugu badala ya shayiri.” Maneno ya Ayubu yamemalizika.
basi miiba na iote badala ya ngano, na magugu badala ya shayiri.” Mwisho wa maneno ya Ayubu.