< Ayubu 29 >

1 Ayubu akaendelea na kusema,
Ayubu akaendelea na hoja yake, akasema:
2 Ee, ningekuwa kama nilivyokuwa miezi iliyopita wakati Mungu aliponiagalia,
“Tazama jinsi ninavyoitamani miezi iliyopita, zile siku ambazo Mungu alikuwa akinilinda,
3 taa yake ilipowaka kichwani pangu, na pale nilipotembea gizani kwa nuru yake.
wakati taa yake iliniangazia kichwani changu, na kwa mwanga wake Mungu nikapita katikati ya giza!
4 Ee, kwamba ningekuwa kama nilivyokuwa katika siku za ujana wangu uhusiano wangu na Mungu ulivyokuwa mzuri,
Natamani siku zile nilizokuwa katika ustawi wangu, wakati urafiki wa Mungu wa ndani ulipoibariki nyumba yangu,
5 wakati Mwenyezi alipokuwa pamoja nami, na wanangu walipokuwa karibu nami,
wakati Mwenyezi alikuwa pamoja nami, nao watoto wangu walikuwa wamenizunguka,
6 wakati maisha yangu yalipokuwa yamejawa na utele, na mwamba uliponichuruzishia chemichemi za mafuta.
wakati njia yangu ilikuwa imenyweshewa siagi, nao mwamba ukanimiminia vijito vya mafuta ya zeituni.
7 Nilipokwenda langoni mwa mji, nilipokaa katika eneo la mji,
“Wakati nilipokwenda kwenye lango la mji na kuketi katika kiwanja,
8 vijana waliniona na walikaa mbali kwa kuniheshimu, na wazee waliinuka na kusimama kwa ajili yangu.
vijana waliniona wakakaa kando, nao wazee walioketi wakasimama;
9 Wana wa mfalme waliacha kuongea nilipofika; wangeweka mkono wao katika vinywa vyao.
wakuu wakaacha kuzungumza na kuziba vinywa vyao kwa mikono yao;
10 Sauti za waheshimiwa zililazimishwa, na ndimi zao hazikuweza kuongea vinywani mwao.
wenye vyeo wakanyamazishwa, nazo ndimi zao zikagandamana na makaakaa ya vinywa vyao.
11 Kwani baada ya kunisikia, wangenibariki; waliponiona, wangeniona na kuniheshimu
Yeyote aliyenisikia alinena mema juu yangu, nao walioniona walinisifu,
12 kwa maana nilikuwa nikiwasaidia masikini waliokuwa wakiteseka, na yatima, asiye na msaada.
kwa sababu nilimwokoa maskini aliyeomba msaada, naye yatima aliyekuwa hana wa kumsaidia.
13 Baraka zao waliokuwa karibu kuangamia zilinipata; niliufanya moyo wa mjane kuimba kwa furaha.
Mtu aliyekuwa karibu kufa alinibariki, nami niliufanya moyo wa mjane kuimba.
14 Nilijivika utakatifu, nao ulinifunika; haki yangu ilikuwa kama kanzu na kilemba.
Niliivaa haki kama vazi langu; uadilifu ulikuwa joho langu na kilemba changu.
15 Niliwasaidia vipofu; niliwasaidia walemavu.
Nilikuwa macho ya kipofu na miguu kwa kiwete.
16 Niliwasaidia wahitaji; niliwasaidia hata wasionijua.
Nilikuwa baba kwa mhitaji; nilimtetea mgeni.
17 Nilimnyamazisha mwovu; nilimpokonya manusura kutoka katika meno yake.
Niliyavunja meno makali ya waovu, na kuwapokonya wahanga kwenye meno yao.
18 Kisha nilisema nitakufa mahali salama; nitazizidisha siku zangu kama mchanga.
“Nikafikiri, ‘Nitafia katika nyumba yangu mwenyewe, nazo siku zangu zitakuwa nyingi kama chembechembe za mchanga.
19 Mizizi yangu imeenea majini, na umande kukaa usiku wote katika matawi yangu.
Mizizi yangu itafika mpaka kwenye maji, nao umande utakaa juu ya matawi yangu usiku kucha.
20 Heshima yangu ni mpya daima, na nguvu za upinde wangu zipo katika mkono wangu kila wakati.
Utukufu wangu utabakia kuwa mpya ndani yangu, upinde wangu daima utaendelea kuwa mpya mkononi mwangu.’
21 Watu walinisikiliza; walinisubiri; walisikiliza ushauri wangu.
“Watu walinisikiliza kwa tumaini, wakingojea ushauri wangu kwa utulivu.
22 Nilipo maliza kuongea hawakunena tena, maneno yangu yaliwatia nguvu kama mvua.
Baada ya mimi kuzungumza, hawakusema zaidi; maneno yangu yaliingia masikioni mwao kwa makini.
23 Waliningoja kama kungoja mvua; waliyathamini maneno yangu, kama walivyotamani mvua iliyokawia.
Waliningojea kama manyunyu ya mvua na kuyapokea maneno yangu kama ardhi inyonyavyo mvua ya vuli.
24 Niliwafurahia bila wao kutarajia; hawakukataa uzuri wa uso wangu.
Walipokata tamaa niliwaonyesha uso wa furaha; nuru ya uso wangu ilikuwa ya thamani kwao.
25 Nilikuwa kama mfalme wao na kuwachagulia cha kufanya; nilikuwa kama mfalme katika jeshi lake, kama awafarijiye waombolezaji mazishini.
Niliwachagulia njia na kukaa kama mkuu wao; niliishi kama mfalme katikati ya majeshi yake; nikawa kama yeye anayewafariji waombolezaji.

< Ayubu 29 >