< Ayubu 21 >
1 Kisha Ayubu akajibu na kusema,
Ndipo Ayubu akajibu:
2 “Sikilizeni hotuba yangu kwa makini, hii na iwe faraja yenu.
“Yasikilizeni maneno yangu kwa makini; hii na iwe faraja mnayonipa mimi.
3 Nimeteswa, lakini pia nitasema; nikisha kusema, endeleeni kudhihaki.
Nivumilieni ninapozungumza, nami nikishazungumza, endeleeni kunidhihaki.
4 Lakini kwangu mimi, malalamikio yangu ni kwa mtu? Kwa nini nisiwe mwenye subira?
“Je, kwani malalamiko yangu yanaelekezwa kwa mwanadamu? Kwa nini nisikose subira?
5 Nitazameni na mshangae, nanyi wekeni mkono wenu midomoni mwenu.
Niangalieni mkastaajabu; mkaweke mkono juu ya vinywa vyenu.
6 Ninapoyafikiria mateso yangu, ninaumizwa, mwili wangu unaogopa.
Ninapowaza juu ya hili, ninaogopa, nao mwili wangu unatetemeka.
7 Kwa nini waovu wanaendelea kuishi, wanazeeka, na kuwa na uwezo katika madaraka?
Kwa nini waovu wanaendelea kuishi, wakifikia umri wa uzee na kuendelea kuwa na nguvu?
8 Wazao wao wanathibitishwa mbele zao, na uzao wao unaimarika machoni pao.
Huwaona watoto wao wakithibitika wakiwa wamewazunguka, wazao wao mbele za macho yao.
9 Nyumba zao ziko salama mbali na hofu; wala fimbo ya Mungu haiko juu yao.
Nyumba zao zi salama wala hakuna hofu; fimbo ya Mungu haiko juu yao.
10 Dume lao la ng'ombe linazalisha; halishindwi kufanya hivyo; ng'ombe wao anazaa na hafishi ndama wake akiwa mchanga.
Madume yao ya ngʼombe huvyaza bila kushindwa kamwe; ngʼombe wao huzaa wala hawaharibu mimba.
11 Wanawapeleka wadogo wao kama kundi la kondoo, na watoto wao hucheza.
Huwatoa watoto wao nje kama kundi; wadogo wao huchezacheza.
12 Wanaimba kwa tari na vinubi na hufurahi kwa muziki na zomari.
Huimba nyimbo kwa matari na kwa kinubi, nao huifurahia sauti ya filimbi.
13 Wanatumia siku zao katika mafanikio, na wanashuka kuzimu kwa utulivu. (Sheol )
Huitumia miaka yao katika mafanikio nao hushuka kaburini kwa amani. (Sheol )
14 Wanamwambia Mungu, 'Ondoka kwetu kwani hatutaki ufahamu wowote juu ya njia zako.
Lakini humwambia Mungu, ‘Tuache sisi!’ Hatuna haja ya kufahamu njia zako.
15 Mwenye enzi ni nani, hata tumwabudu? Tutafaidika na nini tukimwabudu? Tutapata faida gani ikiwa tutamwomba?
Mwenyezi ni nani hata tumtumikie? Tutapata faida gani kumwomba?
16 Tazama, je mafanikio yao hayamo katika mikono yao wenyewe? Sina cha kufanya na ushauri wa waovu.
Lakini kufanikiwa kwao hakupo mikononi mwao wenyewe, hivyo najitenga mbali na shauri la waovu.
17 Mara ngapi taa za waovu huzimwa, au kwamba majanga huja juu yao? Mara ngapi inatokea kwamba Mungu husambaza huzuni kwao kwa hasira?
“Lakini ni mara ngapi taa ya waovu huzimwa? Ni mara ngapi maafa huwajia, yale yawapatayo ambayo Mungu huwapangia katika hasira yake?
18 Ni mara ngapi inatokea kwamba wanakuwa kama mabua mbele ya upepo au kama makapi yanayopeperushwa na dhoruba?
Ni mara ngapi huwa kama majani makavu mbele ya upepo, kama makapi yachukuliwayo na dhoruba?
19 Mnasema, 'Mungu huweka hatia ya mtu kwa watoto wake kuilipa.' Na alipe yeye mwenyewe, ili kwamba aweze kujua hatia yake mwenyewe.
Imesemekana, ‘Mungu huiweka akiba adhabu ya mtu kwa ajili ya wanawe.’ Mungu na amlipe mtu mwenyewe, ili apate kulijua!
20 Acha macho yake yaone uangamivu wake mwenyewe, na acha anywe gadhabu ya Mwenyezi.
Macho yake mwenyewe na yaone maangamizi yake; yeye na ainywe ghadhabu ya Mwenyezi.
21 Kwani anaangaliaje familia yake mbele yake idadi ya miezi yake inapokwisha.
Kwani anajali nini kuhusu jamaa anayoiacha nyuma, miezi yake aliyopangiwa ifikapo mwisho?
22 Je kuna mtu anaweza kumfundisha Mungu maarifa kwa kuwa yeye huwaukumu hata walio juu?
“Je, yuko mtu yeyote awezaye kumfundisha Mungu maarifa, iwapo yeye ndiye ahukumuye hata walio juu ya wote?
23 Mtu mmoja ufa katika nguvu zake kamili, akiwa na utulivu kabisa na kwa amani.
Mtu mmoja hufa akiwa na nguvu zake kamili, akiwa salama na mwenye raha kamili,
24 Mwili wake hauna uhitaji, na kiini cha mifupa yake ina unyevu na afya njema.
mwili wake ukiwa umenawiri, nayo mifupa yake ikiwa imejaa mafuta ndani yake.
25 Mtu mwingine ufa kwa uchungu wa nafsi, bila kujifurahisha kwa jambo lolote jema.
Mtu mwingine hufa katika uchungu wa nafsi, akiwa hajafurahia kamwe jambo lolote zuri.
26 Wanazikwa kaburini wote kwa pamoja, funza wanawafunika wote.
Hao wote hulala mavumbini, nao mabuu huwafunika wote.
27 Tazama, nayajua mawazo yenu, na jinsi mnavyotaka kunikosesha.
“Ninayajua kikamilifu yale mnayoyafikiri, mipango ambayo kwayo mngenitendea mabaya.
28 Kwa kuwa mwasema, 'Iko wapi sasa nyumba ya mwana wa mfalme? Liko wapi kao alipokaa mwovu?'
Mwasema, ‘Iko wapi sasa nyumba ya huyo mtu mkuu, mahema ambayo watu waovu walikaa?’
29 Je hamjawauliza wasafiri? Hamfahamu wanavyoweza kusema,
Je, hamkuwahi kuwauliza hao wanaosafiri? Je, hamkutafakari taarifa zao:
30 kwamba mwovu anaepushwa na siku ya shida, na kwamba anawekwa mbali na siku ya gadhabu?
kwamba mtu mwovu huepushwa kutoka siku ya maafa, kwamba huokolewa kutoka siku ya ghadhabu?
31 Ni nani atakaye ituhumu siku ya mwovu mbele yake? Ni nani atakayemwadhibu kwa alichokifanya?
Ni nani hulaumu matendo yake mbele ya uso wake? Ni nani ampatilizaye kwa yale aliyoyatenda?
32 Hata hivyo atapelekwa kaburini; watu wataliona kaburi lake.
Hupelekwa kaburini, nao ulinzi ukawekwa kwenye kaburi lake.
33 Udongo wa bondeni utakuwa mtamu kwake; watu wote watamfuata, hata kuwe na watu wengi mbele yake.
Udongo ulio bondeni ni mtamu kwake; watu wote watamfuata, nao umati wa watu usiohesabika umemtangulia.
34 Ni jinsi gani basi mtanifariji bila kufikiri, kwa kuwa majibu yenu hayana lolote ila uongo?”
“Hivyo ninyi mnawezaje kunifariji kwa upuzi wenu? Hakuna kilichosalia cha majibu yenu isipokuwa uongo!”