< Yeremia 15 >

1 Kisha Bwana akaniambia, “Hata kama Musa au Samweli walisimama mbele yangu, bado sitawafikiria watu hawa. Watoe mbele yangu, ili waweze kuondoka.
Kisha Bwana akaniambia: “Hata kama Mose na Samweli wangesimama mbele zangu, moyo wangu usingewaelekea watu hawa. Waondoe mbele za macho yangu! Waache waende!
2 Ikiwa watakuambia, 'Tunapaswa kwenda wapi?' Kisha uwaambie, 'Bwana asema hivi Wale wanaotakiwa kufa wanapaswa kufa; wale waliotayarishwa kwa upanga wanapaswa kwenda kwa upanga. Wale waliopelekwa kwa njaa wanapaswa kwenda kwa njaa; na wale waliopelekwa uhamisho wanapaswa kuhamishwa.'
Nao kama wakikuuliza, ‘Twende wapi?’ Waambie, ‘Hili ndilo Bwana asemalo: “‘Wale waliowekwa kwa ajili ya kufa, wakafe; waliowekwa kwa ajili ya upanga, kwa upanga; waliowekwa kwa ajili ya njaa, kwa njaa: waliowekwa kwa ajili ya kutekwa, watekwe.’”
3 Kwa kuwa nitawapa kwa makundi manne-hili ndilo tamko la Bwana-upanga wa kuua wengine, mbwa wararue, ndege wa angani na mnyama mkali wale na kuangamiza.
Bwana asema, “Nitatuma aina nne za waharabu dhidi yao: nazo ni upanga ili kuua na mbwa ili wakokote mbali, ndege wa angani na wanyama wa nchi ili kula na kuangamiza.
4 Nitawafanyia jambo lenye kutisha kwa falme zote za dunia, kwa sababu Manase mwana wa Hezekia, mfalme wa Yuda, alifanya huko Yerusalemu.
Nitawafanya wawe machukizo kwa falme zote za dunia kwa sababu ya kile alichofanya Manase mwana wa Hezekia mfalme wa Yuda huko Yerusalemu.
5 Kwa maana ni nani atakayewahurumia, Yerusalemu? Ni nani atakayeomboleza kwa ajili yako? Nani atakayegeuka kuuliza kuhusu ustawi wako?
“Ni nani atakayekuhurumia, ee Yerusalemu? Ni nani atakayeomboleza kwa ajili yako? Ni nani atakayesimama ili kuuliza kuhusu hali yako?
6 Umeniacha-hili ndilo tamko la Bwana-umerudi nyuma. Kwa hiyo nitawapiga kwa mkono wangu na kukuangamiza. Nimechoka kuwahurumia.
Umenikataa mimi,” asema Bwana. “Unazidi kukengeuka. Hivyo nitanyoosha mkono wangu juu yako na kukuangamiza, siwezi kuendelea kukuonea huruma.
7 Kwa hiyo nitawapepea kwa kipepeo katika milango ya nchi. Nitawafukuza. Nitawaangamiza watu wangu kwani hawakurudi na kuziacha njia zao.
Nitawapepeta kwa uma wa kupepetea kwenye malango ya miji katika nchi. Nitaleta msiba na maangamizi juu ya watu wangu, kwa maana hawajabadili njia zao.
8 Nitawafanya wajane wao kuwa zaidi ya mchanga wa bahari. Dhidi ya mama wa vijana nitamtuma mwangamizi mchana. Nitafanya mshtuko na hofu ghafla kuanguka juu yao.
Nitawafanya wajane wao kuwa wengi kuliko mchanga wa bahari. Wakati wa adhuhuri nitamleta mharabu dhidi ya mama wa vijana wao waume; kwa ghafula nitaleta juu yao maumivu makuu na hofu kuu.
9 Mama aliyezaa watoto saba ataharibika. Atashuka. Jua lake limekuchwa wakati bado ni siku. Yeye atakuwa na aibu na kufedheheka, kwa kuwa nitawatoa wale waliosalia kwa upanga mbele ya maadui zao-hili ndilo tamko la Bwana.”
Mama mwenye watoto saba atazimia na kupumua pumzi yake ya mwisho. Jua lake litatua kungali bado mchana, atatahayarika na kufedheheka. Wale wote waliobaki nitawaua kwa upanga mbele ya adui zao,” asema Bwana.
10 Ole wangu, mama yangu! Kwa maana umenizaa, mimi ambaye ni mtu wa kushindana na hoja katika nchi yote. Sijakopesha, wala hakuna mtu aliyenikopesha, lakini wote wananilaani.
Ole wangu, mama yangu, kwamba ulinizaa, mtu ambaye ulimwengu wote unashindana na kugombana naye! Sikukopa wala sikukopesha, lakini kila mmoja ananilaani.
11 Bwana akasema “Je sitakuokoa kwa manufaa? Kwa hakika nitawafanya maadui wako waombe msaada wakati wa msiba na dhiki.
Bwana akasema, “Hakika nitakuokoa kwa kusudi jema, hakika nitawafanya adui zako wakuombe msaada nyakati za maafa na nyakati za dhiki.
12 Je, mtu anaweza kusaga chuma? Hasa chuma kutoka kaskazini iliyochanganywa na shaba?
“Je, mtu aweza kuvunja chuma, chuma kitokacho kaskazini, au shaba?
13 Nitawapa adui zako utajiri wako na hazina yako kama nyara za bure. Nitafanya hili kwa sababu ya dhambi zako zote zilizofanywa ndani ya mipaka yako yote.
Utajiri wako na hazina zako nitavitoa kuwa nyara, bila gharama, kwa sababu ya dhambi zako zote katika nchi yako yote.
14 Ndipo nitakufanya utumikie adui zako katika nchi ambayo huijui, maana moto utawaka, ukawaka katika ghadhabu yangu juu yako.”
Nitakufanya uwe mtumwa wa adui zako katika nchi usiyoijua, kwa kuwa katika hasira yangu moto umewashwa utakaowaka juu yako daima.”
15 Wewe mwenyewe wajua, Bwana! Unikumbuke na kunisaidia. Ukanilipie kisasi kwa ajili ya wanaonifuata. Katika uvumilivu wako usiniondoe. Utambue kwamba nimekuwa na aibu kwa ajili yako. Maneno yako yamepatikana, na nikayala.
Wewe unafahamu, Ee Bwana, unikumbuke na unitunze mimi. Lipiza kisasi juu ya watesi wangu. Kwa uvumilivu wako usiniondolee mbali; kumbuka jinsi ninavyoshutumiwa.
16 Maneno yako yalikuwa furaha kwangu, furaha yangu kwa moyo wangu; kwa maana jina lako linatangazwa juu yangu, Bwana, Mungu wa majeshi.
Maneno yako yalipokuja, niliyala; yakawa shangwe yangu na furaha ya moyo wangu, kwa kuwa nimeitwa kwa jina lako, Ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote.
17 Sikuketi katika mkutano wa wale waliosherehekea au waliofurahi. Nimeketi kwa faragha kwa sababu ya mkono wako wenye nguvu, kwa maana umenijaza na hasira.
Kamwe sikuketi katika kundi la wafanyao sherehe, wala kamwe sikujifurahisha pamoja nao; niliketi peke yangu kwa sababu mkono wako ulikuwa juu yangu, na wewe ulikuwa umenijaza hasira.
18 Kwa nini maumivu yangu yanaendelea na jeraha langu halitibiki, linakataa kuponywa? Je, utakuwa kama maji ya udanganyifu kwangu, maji yanayokauka?
Kwa nini maumivu yangu hayakomi, na jeraha langu ni la kuhuzunisha, wala haliponyeki? Je, utakuwa kwangu kama kijito cha udanganyifu, kama chemchemi iliyokauka?
19 Kwa hiyo Bwana asema hivi, “Yeremia, Ikiwa utatubu, nitakurejesha, nawe utasimama mbele yangu na kunitumikia. Kwa maana ukitenganisha mambo ya kipumbavu kwa vitu vya thamani, utakuwa kama kinywa changu. Watu watakuja kwako, lakini wewe mwenyewe usirudi kwao.
Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana: “Kama ukitubu, nitakurejeza ili uweze kunitumikia; kama ukinena maneno yenye maana, wala si ya upuzi, utakuwa mnenaji wangu. Watu hawa ndio watakaokugeukia, wala si wewe utakayewageukia wao.
20 Nitakufanya kama ukuta wa shaba usioweza kuingilika kwa watu hawa, nao watapigana vita dhidi yako. Lakini hawatakushinda, kwa kuwa mimi ni pamoja nawe ili kuokoa na kukuponya-hili ndilo tamko la Bwana-
Nitakufanya wewe uwe ukuta kwa watu hawa, ngome ya ukuta wa shaba; watapigana nawe lakini hawatakushinda, kwa maana mimi niko pamoja nawe kukuponya na kukuokoa,” asema Bwana.
21 kwa maana nitakuokoa mikononi mwa waovu na kukukomboa katika mkono wa mshindani.”
“Nitakuokoa kutoka mikono ya waovu, na kukukomboa kutoka makucha ya watu wakatili.”

< Yeremia 15 >