< Yeremia 10 >

1 “Sikilizeni neno ambalo BWANA anawaambieni, enyi nyumba ya Israeli.
Sikieni lile ambalo Bwana, anena nanyi ee nyumba ya Israeli.
2 BWANA asema hivi, 'msijifunze njia za mataifa, na msishangazwe na ishara za mbinguni, kwa kuwa mataifa hushangazwa na haya.
Hili ndilo asemalo Bwana: “Usijifunze njia za mataifa wala usitishwe na ishara katika anga, ingawa mataifa yanatishwa nazo.
3 Kwa kuwa desturi za watu ni ubatili. Kwa kuwa mtu mmoja hukata mti msituni; kazi ya mikono ya mtu na shoka.
Kwa maana desturi za mataifa hazina maana, wanakata mti msituni, na fundi anauchonga kwa patasi.
4 Kisha huzipamba kwa fedha na dhahabu. Huikaza kwa misumari na nyundo ili isitikisike.
Wanaparemba kwa fedha na dhahabu, wanakikaza kwa nyundo na misumari ili kisitikisike.
5 Sanamu hizi ni mfano wa sanamu za kutishia ndege katika shamba la matango, kwa kuwa haziwezi kusema chochote. Hubebwa, kwa kuwa haziwezi hata kusogea hatua moja. Usiwaogope, Kwani hawawezi kutenda maovu wala mema.”
Sanamu zao ni kama sanamu iliyowekwa shambani la matango kutishia ndege nazo haziwezi kuongea; sharti zibebwe sababu haziwezi kutembea. Usiziogope; haziwezi kudhuru, wala kutenda lolote jema.”
6 Hakuna aliye kama wewe, BWANA. Wewe ni mkuu, na jina lako lina nguvu.
Hakuna aliye kama wewe, Ee Bwana; wewe ni mkuu, jina lako ni lenye nguvu katika uweza.
7 Ni nani asiyekuwa na hofu juu yako, wafalme wa mataifa? Kwa kuwa hiki ndicho unachostahili, kwa kuwa hakuna wa kuwa kama wewe kati ya wote wenye hekima katika mataifa yote au katika hali yao ya enzi.
Ni nani ambaye haimpasi kukuheshimu wewe, Ee Mfalme wa mataifa? Hii ni stahili yako. Miongoni mwa watu wote wenye hekima katika mataifa na katika falme zao zote, hakuna aliye kama wewe.
8 Wote wako sawa, ni kama wanyama na wapumbavu, wanafunzi wa samamu ambazo si chochote isipokuwa miti tu.
Wote hawana akili, tena ni wapumbavu, wanafundishwa na sanamu za miti zisizofaa lolote.
9 Wanaleta fedha iliyofuliwa kutoka Tarshishi, na dhahabu kutoka Ufazi iliyotengenezwa na sonara, ni kazi ya ustadi. Mavazi yao ni ya rangi ya samawi na urujuani. Watu wao stadi waliyafanya haya yote.
Huleta fedha iliyofuliwa kutoka Tarshishi na dhahabu kutoka Ufazi. Kile ambacho fundi na sonara wametengeneza huvikwa mavazi ya rangi ya samawi na urujuani: vyote vikiwa vimetengenezwa na mafundi stadi.
10 Lakini BWANA ni Mungu wa kweli. Yeye ni Mungu aliye hai na mfalme wa milele. Matetemeko yako katika hasira yake, na mataifa hayawezi kuvumilia hasira yake.
Lakini Bwana ni Mungu wa kweli, yeye ndiye Mungu aliye hai, Mfalme wa milele. Anapokasirika, dunia hutetemeka, mataifa hayawezi kustahimili hasira yake.
11 Utawaambia hivi, “Miungu ambayo haikuumba mbingu na nchi itaangamia katika dunia hii na chini ya mbingu.”
“Waambie hivi: ‘Miungu hii, ambayo haikuumba mbingu na dunia, itaangamia kutoka dunia na kutoka chini ya mbingu.’”
12 Aliyeiumba dunia kwa nguvu zake aliumba nchi kavu kwa hekima zake na kuzitandaza mbingu kwa fahamu zake.
Lakini Mungu aliiumba dunia kwa uweza wake, akaweka misingi ya ulimwengu kwa hekima yake, na akazitandaza mbingu kwa ufahamu wake.
13 Sauti yake ndiyo itengenezayo muungurumo wa maji mbinguni, naye huzileta mbingu katika mwisho wa dunia. Hutengeneza radi kwa ajili ya mvua na kutuma upepo kutoka katika hazina yake.
Atoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma; huyafanya mawingu yainuke kutoka miisho ya dunia. Hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua, naye huuleta upepo kutoka ghala zake.
14 Kila mtu amekuwa mjinga, hawana maarifa. Kila mfua chuma ameaibishwa kwa sanamu zake. Maana sanamu yake ya kuyeyushwa ni uongo; hakuna pumzi ndani yake.
Kila mmoja ni mjinga na hana maarifa, kila sonara ameaibishwa na sanamu zake. Vinyago vyake ni vya udanganyifu, havina pumzi ndani yavyo.
15 Ni ubatili tu, ni kazi ya udanganyifu; zitapotea wakati wa hukumu.
Havifai kitu, ni vitu vya kufanyia mzaha tu, hukumu yavyo itakapowadia, vitaangamia.
16 Lakini Mungu ni fungu la Yakobo, si kama hawa, kwa kuwa yeye ndiye aliyeviumba vitu vyote. Israeli ni kabila ya urithi wake; BWANA wa majeshi ndiye jina lake.
Yeye aliye Fungu la Yakobo sivyo alivyo, kwani ndiye Muumba wa vitu vyote, pamoja na Israeli, kabila la urithi wake: Bwana Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake.
17 Kusanya vitu vyako na uiache nchi, wewe ambaye umekuwa ukiishi katika mazingiwa haya.
Kusanyeni mali na vitu vyenu mwondoke nchi hii, enyi mnaoishi katika hali ya kuzingirwa na jeshi.
18 Kwa kuwa BWANA asema hivi, “Tazama, Ni tayari kuwatupa wakazi wa nchi nje wakati huu. Nitawasababishia huzuni, na itakuwa hivyo.”
Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana: “Wakati huu, nitawatupa nje kwa nguvu wote waishio katika nchi hii; nitawataabisha ili waweze kutekwa.”
19 Ole wangu! Kwa sababu ya mifupa yangu iliyovunjika, Jeraha zangu zimeumia. Kwa hiyo nilisema. “Hakika haya ni maumivu, lakini lazima nivumilie.”
Ole wangu mimi kwa ajili ya kuumia kwangu! Jeraha langu ni kubwa! Lakini nilisema, “Kweli hii ni adhabu yangu, nami sharti niistahimili.”
20 Hema yangu imeharibiwa, na kamba za hema yangu zote zimekatwa. Wamewachukua watoto wangu wote, Kwa hiyo hawaishi tena. Hakuna tena mtu wa kuitandaza hema yangu au wa kuziinua pazia za hema yangu.
Hema langu limeangamizwa; kamba zake zote zimekatwa. Wana wangu wametekwa na hawapo tena; hakuna hata mmoja aliyebaki wa kusimamisha hema langu wala wa kusimamisha kibanda changu.
21 Kwa kuwa wachungaji wamekuwa wapumbavu. Hawamtafuti BWANA. Kwa hiyo hawana mafanikio; Kondoo wao wote wamesambaa.
Wachungaji hawana akili wala hawamuulizi Bwana, hivyo hawastawi na kundi lao lote la kondoo limetawanyika.
22 Taarifa imewadia, “Tazama! inakuja, tetemeko kubwa linakuja kutoka katika nchi ya kaskazini kuifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa, na maficho ya mbweha.
Sikilizeni! Taarifa inakuja: ghasia kubwa kutoka nchi ya kaskazini! Hii itafanya miji ya Yuda ukiwa, makao ya mbweha.
23 Ninajua, BWANA, kwamba njia ya mtu haiji kutoka kwake. Wala hakuna mtu atembeaye anayeongoza hatua zake mwenyewe.
Ninajua, Ee Bwana, kwamba maisha ya mwanadamu si yake mwenyewe; hawezi kuziongoza hatua zake mwenyewe.
24 Ee BWANA, unirudi, kwa hukumu za haki, si kwa hasira zako vinginevyo utaniangamiza.
Unirudi, Ee Bwana, lakini kwa kipimo cha haki: si katika hasira yako, usije ukaniangamiza.
25 Mwaga hasira zako kwa mataifa ambao hawakujui na katika familia ambazo hawakuiti kwa jina lako. Kwa kuwa wamemla Yakobo na kumwangamiza kabisa na kuyafanya makao yake kuwa ukiwa.
Umwage ghadhabu yako juu ya mataifa wasiokujua wewe, juu ya mataifa wasioliitia jina lako. Kwa kuwa wamemwangamiza Yakobo; wamemwangamiza kabisa na kuiharibu nchi yake.

< Yeremia 10 >