< Hosea 1 >
1 Hili ni neno la Bwana lililofika kwa Hosea mwana wa Beeri siku za Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda, na katika siku za Yeroboamu mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli.
2 Wakati Bwana alipozungumza kwanza kupitia Hosea, akamwambia, “Nenda ukajitwalie mke ambaye ni kahaba. Atakuwa na watoto ambao ni matokeo ya ukahaba wake. Kwa maana nchi inafanya uzinzi mkubwa kwa kumwacha Bwana.”
3 Basi Hosea akaenda akamwoa Gomeri binti Diblaimu, naye akachukua mimba, akazaa mtoti mwanamume.
4 Bwana akamwambia Hosea, Mwite jina lake Yezreeli. Kwa maana kwa muda mfupi nitaiadhibu nyumba ya Yehu kwa sababu ya kumwaga damu huko Yezreeli; nami nitamaliza ufalme wa nyumba ya Israeli.
5 Itatokea siku ile nitakapovunja upinde wa Israeli katika bonde la Yezreeli.
6 Gomeri akachukua mimba tena akamzaa binti. Ndipo Bwana akamwambia Hosea, “Mwite jina lake Lo Ruhama; kwa maana sitawahurumia tena nyumba ya Israeli, nisije nikawasamehe kwa njia yoyote.
7 Hata hivyo nitawahurumia nyumba ya Yuda, nami nitawaokoa mwenyewe, Bwana, Mungu wao. Sitawaokoa kwa upinde, upanga, vita, farasi, au wapanda farasi. '
8 Baada ya Gomeri kumwachisha Lo Ruhama, alipata mimba na kuzaa mtoto mwingine mwanamume.
9 Ndipo Bwana akasema, “Mwite jina la Lo Ami; kwa kuwa ninyi si watu wangu, wala mimi si Mungu wenu.”
10 Hata hivyo idadi ya watu wa Israeli itakuwa kama mchanga wa bahari, ambayo haiwezi kupimwa au kuhesabiwa. Itakuwa pale ambapo waliambiwa, “Ninyi si watu wangu,” wataambiwa, “Ninyi ni watu wa Mungu aliye hai.”
11 Watu wa Yuda na watu wa Israeli watakusanyika pamoja. Wao wataweka kiongozi mmoja wao wenyewe, na watatoka kutoka nchi, kwa maana itakuwa siku ya Yezreeli kuu.