< Hosea 9 >

1 Usifurahi, Israeli, kwa furaha kama watu wengine. Kwa maana haukuwa mwaminifu, umemuacha Mungu wako. Unapenda kulipa mshahara kwa kahaba kwenye sakafu zote za nafaka.
Usifurahie, ee Israeli; usishangilie kama mataifa mengine. Kwa kuwa hukuwa mwaminifu kwa Mungu wako; umependa ujira wa kahaba kwenye kila sakafu ya kupuria nafaka.
2 Lakini sakafu na divai hazitawalisha; divai mpya itampungukia.
Sakafu za kupuria nafaka na mashinikizo ya kukamulia divai havitalisha watu, divai mpya itawapungukia.
3 Hawawezi kuendelea kuishi katika nchi ya Bwana; badala yake, Efraimu atarudi Misri, na siku moja watakula chakula kichafu katika Ashuru.
Hawataishi katika nchi ya Bwana, Efraimu atarudi Misri na atakula chakula kilicho najisi huko Ashuru.
4 Hawatamtolea Bwana sadaka za divai, wala hawatamfurahisha. Dhabihu zao zitakuwa kwao kama chakula cha matanga wote wanaolila watakuwa wamejisikia. Maana chakula chao kitakuwa chao pekee; hautakuingia nyumbani mwa Bwana.
Hawatammiminia Bwana sadaka ya divai wala dhabihu zao hazitampendeza. Dhabihu kama hizo zitakuwa kwao kama mkate wa waombolezaji; nao wote wazilao watakuwa najisi. Chakula hiki kitakuwa kwa ajili yao wenyewe; kisije katika Hekalu la Bwana.
5 Utafanya nini siku ya sikukuu iliyowekwa rasmi, siku ya sikukuu ya Yahweh?
Mtafanya nini katika siku ya sikukuu zenu zilizoamriwa, katika siku za sikukuu za Bwana?
6 Kwa maana, angalia, wamekimbia uharibifu, Misri itawakusanya, na Nofu itawazika. Maana hazina zao za pesa za fedha zitakuwa nao, na miiba itajaza hema zao.
Hata ikiwa wataokoka maangamizi, Misri atawakusanya, nayo Memfisi itawazika. Hazina zao za fedha zitasongwa na michongoma, nayo miiba itafunika mahema yao.
7 Siku za adhabu zinakuja; siku za kulipiza kisasi zinakuja. Waisraeli wote wajue mambo haya. Nabii ni mpumbavu, na mtu aliyevuviwa ni mwendawazimu, kwa sababu ya uovu wako mkubwa na uadui mkubwa.
Siku za adhabu zinakuja, siku za malipo zimewadia. Israeli na afahamu hili. Kwa sababu dhambi zenu ni nyingi sana na uadui wenu ni mkubwa sana, nabii anadhaniwa ni mpumbavu, mtu aliyeongozwa na Mungu anaonekana mwendawazimu.
8 Nabii ndiye mlinzi wa Mungu wangu juu ya Efraimu. Lakini mtego wa ndege ni juu ya njia zake zote, na uadui umo katika nyumba ya Mungu wake.
Nabii, pamoja na Mungu wangu, ndiye mlinzi juu ya Efraimu, hata hivyo mitego inamngojea katika mapito yake yote, na uadui katika nyumba ya Mungu wake.
9 Wamejiharibu wenyewe kama siku za Gibea. Mungu atawakumbusha uovu wao, naye atawaadhibu dhambi zao.
Wamezama sana katika rushwa, kama katika siku za Gibea. Mungu atakumbuka uovu wao na kuwaadhibu kwa ajili ya dhambi zao.
10 Bwana asema, “Nilipoikuta Israeli, ilikuwa kama kutafuta zabibu jangwani. Kama matunda ya kwanza ya msimu kwenye mtini, nimewaona baba zenu. Lakini wakaenda Baal Peori, nao wakajitoa kwenye sanamu ya aibu. Walikuwa chukizo kama sanamu waliyoipenda.
“Nilipompata Israeli, ilikuwa kama kupata zabibu jangwani; nilipowaona baba zenu, ilikuwa kama kuona matunda ya kwanza katika mtini. Lakini walipofika Baal-Peori, walijiweka wakfu kwa ile sanamu ya aibu, nao wakawa najisi kama kitu kile walichokipenda.
11 Na kwa ajili ya Efraimu, utukufu wao utatoka kama ndege. Hakutakuwa na kuzaa, hakuna mimba, wala achukuaye mimba.
Utukufu wa Efraimu utaruka kama ndege: hakuna kuzaa, hakuna kuchukua mimba, hakuna kutunga mimba.
12 Ingawa wameleta watoto, nitawachukua ili asibaki hata mmoja. Ole wao nikiwaacha!
Hata wakilea watoto, nitamuua kila mmoja. Ole wao nitakapowapiga kisogo!
13 Nimeiona Efraimu, kama vile Tiro, alipandwa katika mlima, lakini Efraimu atatoa watoto wake kwa mtu atakayewaua.
Nimemwona Efraimu, kama Tiro, aliyeoteshwa mahali pazuri. Lakini Efraimu wataleta watoto wao kwa mchinjaji.”
14 Wape, Bwana-utawapa nini? Wape tumbo lenye kuharibu mimba na matiti ambayo haitoi maziwa.
Wape, Ee Bwana, je, utawapa nini? Wape matumbo ya kuharibu mimba na matiti yaliyokauka.
15 'Kwa sababu ya uovu wao wote huko Gilgali, ndivyo nilipowachukia. Kwa sababu ya matendo yao ya dhambi, nitawafukuza nje ya nyumba yangu. Sitawapenda tena; maofisa wao wote ni waasi.
“Kwa sababu ya uovu wao wote huko Gilgali, niliwachukia huko. Kwa sababu ya matendo yao ya dhambi, nitawafukuza katika nyumba yangu. Sitawapenda tena, viongozi wao wote ni waasi.
16 Efraimu ni mgonjwa, na mizizi yao imekauka; hawazai matunda. Hata ikiwa wana watoto, nitawaua watoto wao wapendwa.
Efraimu ameharibiwa, mzizi wao umenyauka, hawazai tunda. Hata kama watazaa watoto, nitawachinja watoto wao waliotunzwa vizuri.”
17 Mungu wangu atawakataa kwa sababu hawakumtii. Watakuwa watu wa kutangatanga kati ya mataifa.
Mungu wangu atawakataa kwa sababu hawakumtii; watakuwa watu wa kutangatanga miongoni mwa mataifa.

< Hosea 9 >