< Hosea 5 >

1 Sikilizeni haya, makuhani! kuweni makini, nyumba ya Israeli! Sikilizeni, nyumba ya mfalme! Kwa maana hukumu itakuja juu yenu nyote. Mmekuwa mtego huko Mizpa na wavu uliosambazwa juu ya Tabori.
“Sikieni hili, enyi makuhani! Kuweni wasikivu, enyi Waisraeli! Sikieni, ee nyumba ya mfalme! Hukumu hii ni dhidi yenu: Mmekuwa mtego huko Mispa, wavu uliotandwa juu ya Tabori.
2 Waasi husimama sana katika mauaji, lakini nitawaadhibu wote.
Waasi wamezidisha sana mauaji. Mimi nitawatiisha wote.
3 Najua Efraimu, na Israeli hajajificha kwangu. Efraimu, sasa umekuwa kama kahaba; Israeli ni unajisi.
Ninajua yote kuhusu Efraimu, Israeli hukufichika kwangu. Efraimu, sasa umegeukia ukahaba, Israeli amenajisika.
4 Matendo yao hayawataruhusu kumgeukia Mungu, maana mawazo ya uzinzi yako ndani yao, na hawatamjua Bwana.
“Matendo yao hayawaachii kurudi kwa Mungu wao. Roho ya ukahaba imo ndani ya mioyo yao, hawamkubali Bwana.
5 Kiburi cha Israeli kinawashuhudia; Kwa hiyo Israeli na Efraimu watajikwaa kwa hatia zao; na Yuda pia wataanguka pamoja nao.
Kiburi cha Israeli kinashuhudia dhidi yao; Waisraeli, hata Efraimu, wanajikwaa katika dhambi zao; pia Yuda atajikwaa pamoja nao.
6 Watakwenda pamoja na kondoo zao na ng'ombe zao kumtafuta Bwana, lakini hawatamuona, kwa kuwa amejiondoa kutoka kwao.
Wakati wanapokwenda na makundi yao ya kondoo na ngʼombe kumtafuta Bwana, hawatampata; yeye amejiondoa kutoka kwao.
7 Walikuwa wasio waaminifu kwa Bwana, kwa kuwa wamezaa watoto haramu. Sasa sherehe mpya za mwezi zitawaangamiza na mashamba yao.
Wao si waaminifu kwa Bwana; wamezaa watoto haramu. Sasa sikukuu zao za Mwandamo wa Mwezi zitawaangamiza wao pamoja na mashamba yao.
8 Piga tarumbeta huko Gibea, na tarumbeta huko Rama. Sauti ya kilio cha vita huko Beth Aveni 'Tutakufuata, Benyamini!'
“Pigeni tarumbeta huko Gibea, baragumu huko Rama. Paza kilio cha vita huko Beth-Aveni, ongoza, ee Benyamini.
9 Efraimu itakuwa ukiwa siku ya adhabu. Miongoni mwa makabila ya Israeli nimetangaza habari itakayotokea.
Efraimu ataachwa ukiwa katika siku ya kuadhibiwa. Miongoni mwa makabila ya Israeli ninatangaza lile ambalo halina budi kutukia.
10 Viongozi wa Yuda ni kama wale wanaondoao jiwe la mipaka. Nami nitamwaga ghadhabu yangu juu yao kama maji.
Viongozi wa Yuda ni kama wale wanaosogeza mawe ya mpaka. Nitamwaga ghadhabu yangu juu yao kama mafuriko ya maji.
11 Efraimu ameangamizwa; ameangamizwa kwa hukumu, kwa sababu ametembea kwa hiari kufuata sanamu.
Efraimu ameonewa, amekanyagwa katika hukumu kwa kuwa amekusudia kufuatia sanamu.
12 Kwa hiyo nitakuwa kama nondo kwa Efraimu, na kama uozo kwa nyumba ya Yuda.
Mimi ni kama nondo kwa Efraimu, na kama uozo kwa watu wa Yuda.
13 Efraimu alipoona ugonjwa wake, Yuda akaona jeraha lake; Efraimu akaenda Ashuru; Yuda akatuma wajumbe kwa mfalme mkuu. Lakini hakuweza kuwaponya watu au kuponya jeraha lako.
“Wakati Efraimu alipoona ugonjwa wake, naye Yuda vidonda vyake, ndipo Efraimu alipogeukia Ashuru, na kuomba msaada kwa mfalme mkuu. Lakini hawezi kukuponya, wala hawezi kukuponya vidonda vyako.
14 Kwa hiyo nitakuwa kama simba kwa Efraimu, na kama simba kwa nyumba ya Yuda. Mimi, naam mimi, nitapotea na kwenda mbali; Nitawachukua, na hakutakuwa na mtu wa kuwaokoa.
Kwa maana nitakuwa kama simba kwa Efraimu, kama simba mkubwa kwa Yuda. Nitawararua vipande vipande na kuondoka; nitawachukua mbali, na hakuna wa kuwaokoa.
15 Nitakwenda na kurudi mahali pangu, mpaka watambue hatia yao na kutafuta uso wangu, hata wakanitafute kwa bidii katika dhiki yao.
Kisha nitarudi mahali pangu mpaka watakapokubali kosa lao. Nao watautafuta uso wangu; katika taabu yao watanitafuta kwa bidii.”

< Hosea 5 >