< Wahebrania 12 >
1 Kwahiyo, kwa kuwa tumezungukwa na wingu kubwa la mashaidi, na tutupe kila kitu kinacho tulemea pamoja na dhambi ambayo inatuzingira kwa urahisi. Tupige mbio kwa saburi katika mashindano yaliyowekwa mbele yetu.
2 Tuyaelekeze macho yetu kwa Yesu, aliye mwanzilishi na mwenye kutimiliza imani yetu, ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake alistahmili msalaba, akiidharau aibu yake, na akakaa chini mkono wa kulia wa kiti cha enzi cha Mungu.
3 Maana mtafakarini yeye aliye stahimili maneno ya chuki kutoka kwa wenye dhambi, dhidi yake mwenyewe ili kwamba msije mkachoka au kuzimia mioyo yenu.
4 Hamjataabika au kuteseka mkishindana na dhambi kiasi cha kuishiwa damu.
5 Tena mmesahau kule kutiwa moyo ambako kunawaelekeza kama watoto wa kiume: “Mwanangu, usiyachukuwe kwa wepesi marudia ya Bwana, wala usikate tamaa unapo rekebishwa na yeye.”
6 Kwa kuwa Bwana humrudi yeyote ambaye anampenda, na humwadhibu kila mwana ambaye humpokea.
7 Stahimili majaribu kama kurudiwa. Mungu hushughulika nanyi kama anavyoshughulika na watoto, maana ni mtoto yupi ambaye baba yake hawezi kumrudi?
8 Lakini kama hakuna kurudiwa, ambako sisi sote tunashiriki, basi ninyi ni haramu na si watoto wake.
9 Zaidi ya yote, tulikuwa na baba zetu kidunia wa kuturudi, na tuliwaheshimu. Je haitupasi hata zaidi kumtii Baba wa kiroho na kuishi?
10 Kwa hakika baba zetu walituadhibu kwa miaka michache kama ilivyoonekana sawa kwao, lakini Mungu hutuadhibu kwa faida yetu ili tushiriki utakatifu wake.
11 Hakuna adhabu inayofurahisha kwa wakati huo. Huwa na maumivu. Hata hivyo, baadaye huzaa tunda la amani ya utauwa kwa wale waliofundishwa nayo.
12 Kwa hiyo inueni mikono yenu iliyolegea na kufanya magoti yenu yaliyo dhaifu kuwa yenye nguvu tena;
13 nyosheni mapito ya nyayo zenu, ili kwamba yeyote aliye mlemavu hataongozwa upotevuni lakini apate kuponywa.
14 Tafuteni amani na watu wote, na pia utakatifu ambao bila huo hakuna atakayemwona Bwana.
15 Muwe waangalifu ili kwamba asiwepo atakayetengwa mbali na neema ya Mungu, na kwamba lisije shina la uchungu litakalochipuka na kusababisha shida na kukengeusha wengi.
16 Angalieni kuwa hakuna zinaa au mtu asiye mtauwa kama vile Esau, ambaye kwa sababu ya mlo mmoja aliuza haki yake ya kuzaliwa.
17 Kwa kuwa mnajua kwamba baadaye, alipotamani kurithi baraka, alikataliwa, kwa sababu hakupata fursa ya kutubu pamoja na baba yake, hata ingawa alitafuta sana kwa machozi.
18 Kwa kuwa hamkuja katika mlima ambao unaweza kuguswa, Mlima unaowaka moto, giza, kukatisha tamaa na dhoruba.
19 Hamkuja kwa sauti za tarumbeta, au kwa maneno yatokanayo na sauti ambayo ilisababisha kila wasikiao wasiombe neno lolote kusemwa kwao.
20 Kwa kuwa hawakuweza kuvumilia kile kilichoamuliwa: “Ikiwa hata mnyama agusaye mlima, lazima apigwe kwa mawe.”
21 Ya kutisha zaidi aliyoyaona Musa alisema, “Nimeogopa sana kiasi cha kutetemeka”.
22 Badala yake, mmekuja mlima Sayuni na katika mji wa Mungu aliye hai, Yerualem ya mbinguni, na kwa malaika elfu kumi wanaosherehekea.
23 Mmekuja katika kusanyiko la wazaliwa wa kwanza wote waliosajiliwa mbinguni, kwa Mungu hakimu wa wote, na kwa roho za watakatifu ambao wamekamilishwa.
24 Mmekuja kwa Yesu mpatanishi wa agano jipya, na kwa damu iliyonyunyizwa ambayo hunena mema zaidi kuliko damu ya Habili.
25 Angalia kuwa usije ukamkataa mmoja ambaye anenaye. Kwa kuwa kama hawakuepuka walipomkataa mmoja aliye waonya duniani, kwa hakika hatutaepuka ikiwa tutageuka mbali kutoka kwa yule atuonyaye kutoka mbinguni.
26 Kwa wakati huo sauti yake ilitikisa dunia. Lakini sasa ameahidi na kunena, “Bado mara nyingine tena sitatikisa dunia pekee, bali mbingu pia.”
27 Maneno haya, “Mara moja tena,” inaonesha kutoweshwa kwa vitu vile vitetemeshwavyo, hivi ni, vitu vile ambavyo vimeumbwa, ili kwamba vile vitu visivyotetemeshwa vibakie.
28 Kwa hiyo, tupokee ufalme ambao hautetemeshwi, tufurahi katika hali ya kumwabudu Mungu kwa kukubali pamoja na kunyenyekea katika kicho,
29 kwa maana Mungu wetu ni moto ulao.