< Wahebrania 11 >
1 Sasa imani ni hakika aliyo nayo mtu wakati atarajiapo kitu fulani kwa ujasiri. Ni hakika ya kitu ambacho bado hakijaonekana.
2 Kwa sababu hii mababu zetu walithibitika kwa imani yao.
3 Kwa imani tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa amri ya Mungu, ili kwamba kile kinachoonekana hakikutengenezwa kutokana na vitu ambavyo vilikuwa vinaonekana. (aiōn )
4 Ilikuwa kwa sababu ya imani kwamba Habili alimtolea Mungu sadaka ya kufaa kuliko alivyofanya Kaini. Ilikuwa ni kwa sababu hii kwamba alisifiwa kuwa mwenye haki. Mungu alimsifu kwa sababu ya zawadi alizoleta. Kwa sababu hiyo, Habili bado ananena, ingawa amekufa.
5 Ilikuwa kwa imani kwamba Enoko alichukuliwa juu na hakuona mauti. “Hakuonekana, kwa sababu Mungu alimchukua” kwa vile ilinenwa juu yake kuwa alimpendeza Mungu kabla ya kuchukuliwa juu.
6 Pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, kwa kuwa ajaye kwa Mungu lazima aamini kwamba Mungu anaishi na kwamba huwapatia zawadi wale wamtafutao.
7 Ilikuwa ni kwa imani kwamba Nuhu, akiwa ameonywa na Mungu kuhusiana na mambo ambayo hayakuwa yameonekana, kwa heshima ya ki Mungu alitengeneza safina kwa ajili ya kuiokoa familia yake. Kwa kufanya hivi, aliuhukumu ulimwengu na akawa mrithi wa haki ambayo huja kupitia imani.
8 Ilikuwa ni kwa imani kwamba Ibrahimu, alipoitwa alitii na kwenda mahali ambapo alipaswa kupokea kama urithi. Alitoka bila kujua mahali gani alikuwa anakwenda.
9 Ilikuwa ni kwa imani kwamba aliishi katika nchi ya ahadi kama mgeni. Aliishi katika mahema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi wenzake wa ahadi ile ile.
10 Hii ni kwa sababu alitarajia kuupata mji ambao mwenye kuubuni na mjenzi wake angelikuwa ni Mungu.
11 Ilikuwa ni kwa imani kwamba Ibrahimu, na Sara mwenyewe, walipokea nguvu ya kutunga mimba ingawa walikuwa wazee sana, kwa kuwa walimuona Mungu kuwa mwaminifu, ambaye aliwaahidia mtoto wa kiume.
12 Kwa hiyo pia kutoka kwa mtu huyu mmoja ambaye alikuwa amekaribia kufa wakazaliwa watoto wasiohesabika. Walikuwa wengi kama nyota za angani na wengi kama mbegu za mchanga katika ufukwe wa bahari.
13 Hawa wote walikufa katika imani pasipo kupokea ahadi. Isipokuwa, wakiwa wameziona na kuzikaribisha kwa mbali, walikiri kwamba walikuwa wageni na wapitaji juu ya nchi.
14 Kwa wale wasemao mambo kama haya wanaweka bayana kuwa wanatafuta nchi yao wenyewe.
15 Kwa kweli, kama wangekuwa wakiifikiria nchi ambayo kwayo walitoka, wangelikuwa na nafasi ya kurejea.
16 Lakini kama ilivyo, wanatamani nchi iliyo bora, ambayo, ni ya kimbingu. Kwa hiyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao, kwa kuwa ametayarisha mji kwa ajili yao.
17 Ilikuwa ni kwa imani kwamba Ibrahimu baada ya kujaribiwa, alimtoa Isaka. Ndiyo, yeye ambaye alipokea kwa furaha ahadi, alimtoa mwanawe wa pekee,
18 ambaye juu yake ilinenwa, “Kutoka kwa Isaka uzao wako utaitwa.”
19 IbrahImU alijua kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kumfufua Isaka kutoka katika wafu, na kwa kuzungumza kwa lugha ya maumbo, alimpokea.
20 Ilikuwa ni kwa imani kwamba Isaka alimbariki Yakobo na Esau kuhusu mambo yajayo.
21 Ilikuwa ni kwa imani kwamba Yakobo alipokuwa katika hali ya kufa, alimbariki kila mmoja wa watoto wa Yusufu. Yakobo akaabudu, akiegemea juu ya fimbo yake.
22 Ilikuwa ni kwa imani kwamba Yusufu wakati wake wa mwisho ulipokaribia, alinena juu ya kutoka kwa wana wa Israel Misri na akawaagiza kuchukua pamoja nao mifupa yake.
23 Ilikuwa ni kwa imani kwamba Musa, alipozaliwa, alifichwa kwa miezi mitatu na wazazi wake kwa sababu walimuona kuwa ni mtoto mchanga aliyekuwa mzuri, na hawakutishwa na amri ya mfalme.
24 Ilikuwa ni kwa imani kwamba Musa, alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mtoto wa binti Farao.
25 Badala yake, alichagua kushiriki mateso pamoja na watu wa Mungu badala ya kufurahia anasa za dhambi kwa kitambo.
26 Alifikiri aibu ya kumfuata Kristo kuwa ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri kwa kuwa alikaza macho yake katika zawadi ya wakati wake ujao.
27 Ilikuwa ni kwa imani kwamba Musa alitoka Misri. Hakuhofia hasira ya Mfalme, kwa kuwa alivumilia kwa kutazama kwa asiyeonekana.
28 Ilikuwa ni kwa imani kwamba aliishika pasaka na kunyunyiza damu, ili kwamba mharibu wa mzaliwa wa kwanza asiweze kuwagusa wazaliwa wa kwanza wa kiume wa waisrael.
29 Ilikuwa ni kwa imani kwamba walipita katika bahari ya shamu kama katika nchi kavu. Wakati wamisri walipojaribu kupita, walimezwa.
30 Ilikuwa ni kwa imani kwamba ukuta wa Yeriko ulianguka chini, baada ya kuuzunguka kwa siku saba.
31 Ilikuwa ni kwa imani kwamba Rahabu yule kahaba hakuangamia pamoja na wale ambao hawakuwa watiifu, kwa sababu alikuwa amewapokea wapelelezi na kuwahifadhi salama.
32 Na niseme nini zaidi? Maana muda hautoshi kusimulia ya Gideoni, Barak, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samwel na za manabii,
33 ambao kupitia imani walizishinda falme, walitenda haki, na wakapokea ahadi. Walizuia vinywa vya simba,
34 walizima nguvu za moto, walikwepa ncha ya upanga, waliponywa kutoka katika magonjwa, walikuwa mashujaa vitani, na walisababisha majeshi wageni kukimbia.
35 Wanawake walipokea wafu wao kwa njia ya ufufuo. Wengine waliteswa, bila kukubali kuachwa huru ili kwamba waweze kupata uzoefu wa ufufuo ulio bora zaidi.
36 Wengine waliteswa kwa dhihaka na kwa vichapo, naam, hata kwa vifungo na kwa kutiwa gerezani.
37 Walipondwa mawe. Walikatwa vipande kwa misumeno. Waliuawa kwa upanga. Walikwenda kwa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi walikuwa wahitaji, wakiendelea katika maumivu na wakitendewa mabaya
38 (ambayo ulimwengu haukustahili kuwa nao), wakitangatanga nyikani, milimani, katika mapango na katika mashimo ya ardhini.
39 Ingawa watu wote hawa walikubaliwa na Mungu kwa sababu ya imani yao, hawakupokea alichoahidi.
40 Mungu alitangulia kutupatia kitu kilichobora, ili kwamba bila sisi wasingeweza kukamilishwa.