< Mwanzo 9 >
1 Kisha Mungu akambariki Nuhu na wanawe, na kuwaambia, “Zaeni, mkaongezeke, na muijaze nchi.
2 Hofu na utisho wenu vitakuwa juu ya kila mnyama aliye hai juu ya nchi, juu ya kila ndege wa angani, juu ya kila kitu kiendacho chini juu ya ardhi, na juu ya samaki wote wa baharini. Vimetolewa katika mikono yenu.
3 Kila kitu kiendacho kilicho hai kitakuwa chakula kwa ajili yenu. Kama nilivyo wapa mimea, sasa nawapa kila kitu.
4 Lakini msile nyama pamoja na uhai wake - yaani damu yake - ndani yake.
5 Lakini kwa ajili ya damu yenu, uhai uliomo katika damu yenu nitataka malipo. Kutoka katika mkono wa kila mnyama nitaitaka. Kutoka katika mkono wa kila mtu, yaani, kutoka katika mkono wa yule ambaye amemuua ndugu yake, nitataka fidia kwa ajili ya uhai wa mtu huyo.
6 Yeyote amwagaye damu ya mtu, kwa njia ya mtu damu yake itamwagwa, kwa sababu ilikuwa ni katika mfano wa Mungu kwamba Mungu alimuumba mtu.
7 Na hivyo nanyi zaeni na kuongezeka, sambaeni katika inchi yote na muongezeke juu yake.”
8 Kisha Mungu akazungumza na Nuhu na wanae pamoja naye, akisema,
9 “Kwa ajili yangu, sikiliza! Ninakwenda kulithibitisha agano langu pamoja nawe na uzao wenu baada yenu,
10 na kwa kila kiumbe hai kilicho pamoja nawe, pamoja na ndege, mnyama wa kufugwa, na kila kiumbe cha nchi pamoja nawe, kuanzia kwa wote waliotoka kwenye safina, mpaka kwa kila kiumbe hai juu ya nchi.
11 Kwa sababu hii ninalithibitisha agano langu pamoja nanyi, kwamba hapatatokea kuangamizwa kwa mwenye mwili kwa njia ya maji ya gharika. Tena hapatatokea gharika ya kuangamiza nchi.”
12 Mungu akasema, “na hii ndiyo ishara ya agano ambalo ninafanya kati yangu na ninyi pamoja na kila kiumbe hai kilicho pamoja nanyi, kwa vizazi vyote vya baadaye:
13 Nimeweka upinde wangu wa mvua katika wingu, na itakuwa ndiyo ishara ya agano kati yangu na nchi.
14 Hata itakuwa nitakapoleta wingu juu ya nchi na upinde wa mvua ukaonekana katika wingu,
15 ndipo nitakumbuka agano langu, ambalo ni kati yangu na ninyi na kila kiumbe hai cha wote mwenye mwili. Maji hayatafanyika tena gharika kuharibu wote wenye mwili.
16 Upinde wa mvua utakuwa katika mawingu na nitauona, ili kukumbuka agano la milele kati ya Mungu na kila kiumbe hai cha wote wenye mwili ambacho kiko juu ya nchi.”
17 Kisha Mungu akamwambia Nuhu, “Hii ni ishara ya agano ambalo nimelithibitisha kati yangu na wenye mwili wote ambao wako juu ya nchi.”
18 Wana wa Nuhu ambao walitoka katika safina walikuwa ni Shemu, Hamu, na Yafethi. Na Hamu akamzaa kanaani.
19 Watatu hawa walikuwa ndio wana wa Nuhu, na kutokea kwa hawa nchi yote ikajaa watu.
20 Nuhu akaanza kuwa mkulima, na akapanda mizabibu.
21 Akanywa sehemu ya divai na akalewa. Akawa amelala hemeani uchi.
22 Kisha Hamu, baba yake na Kanaani, akaona uchi wa baba yake na akawaambia ndugu zake wawili waliokuwa nje.
23 Kwa hiyo Shemu na Yafethi wakachukua kanzu wakaitanda juu ya mabega yao, na wakatembea kinyumenyume na wakaufunika uchi wa baba yao. Nyuso zao zikiwa zimegeuka nyuma upande mwingine, kwa hiyo hawakuona uchi wa baba yao.
24 Nuhu alipozinduka kutoka katika ulevi wake, alijua ni jambo gani mtoto wake mdogo amemfanyia.
25 Hivyo akasema, “Alaaniwe Kanaani. Na awe mtumishi kwa watumishi wa ndugu zake.”
26 Akasema pia, Yahwe, Mungu wa Shemu, abarikiwe, Kanaani na awe mtumwa wake.
27 Mungu na apanuwe mipaka ya Yafethi, na afanye makazi yake katika hema za Shemu. Kanaani na awe mtumwa wake.”
28 Baada ya gharika, Nuhu aliishi miaka miatatu na hamsini.
29 Siku zote za Nuhu zilikuwa ni miaka mia tisa na hamsini, na kisha alikufa.