< Mwanzo 50 >
1 Yusufu akahuzunika sana hata akauangukia uso wa baba yake, akamlilia, na kumbusu.
Basi Yosefu akamwangukia baba yake, akalilia juu yake na akambusu.
2 Yusufu akawaagiza watumishi wake matabibu kumtia dawa babaye. Hivyo matabibu wakampaka dawa Israeli.
Ndipo Yosefu akawaagiza matabibu waliokuwa wakimhudumia, wamtie baba yake Israeli dawa ili asioze. Hivyo matabibu wakamtia dawa asioze,
3 Wakatimiza siku arobain, kwani huo ndio uliokuwa muda kamili wa kutia dawa. Wamisri wakamlilia kwa siku sabini
wakatumia siku arobaini, kwa maana ndio muda uliotakiwa wa kutia dawa ili asioze. Nao Wamisri wakamwombolezea Yakobo kwa siku sabini.
4 Siku za maombolezo zilipotimia, Yusufu akaongea na watumishi wa baraza la kifalme wa Farao kusema, “Ikiwa nimepata kibali machoni penu, tafadharini ongeeni na Farao, kusema,
Siku za kumwombolezea zilipokwisha, Yosefu akawaambia washauri wa Farao, “Kama nimepata kibali machoni penu semeni na Farao kwa ajili yangu. Mwambieni,
5 'Baba yangu aliniapisha, kusema, “Tazama, ninakaribia kufa. Unizike katika kaburi nililolichimba kwa ajili yangu mwenyewe katika nchi ya Kanaani. Ndipo utakaponizika.” Basi sasa niruhusu niende nimzike baba yangu, na kisha nitarudi.”
‘Baba yangu aliniapisha na kuniambia, “Mimi niko karibu kufa; unizike katika kaburi lile nililochimba kwa ajili yangu mwenyewe katika nchi ya Kanaani.” Sasa nakuomba uniruhusu niende kumzika baba yangu, nami nitarudi.’”
6 Farao akajibu, “Nenda na umzika baba yako, kama alivyokuwapisha.”
Farao akasema, “Panda, uende kumzika baba yako, kama alivyokuapiza kufanya.”
7 Yusufu akaenda kumzika baba yake. Maofisa wa Farao wote wakaenda pamoja naye - washauri wa nyumba yake, maofisa waandamizi wote wa nchi ya Misri,
Hivyo Yosefu akapanda kwenda kumzika baba yake. Maafisa wote wa Farao wakaenda pamoja naye, watu mashuhuri wa baraza lake na watu mashuhuri wote wa Misri.
8 pamoja na nyumba yote ya Yusufu na ndugu zake, na nyumba yote ya baba yake. Lakini watoto wao, kondoo wao na makundi ya mbuzi wao yaliachwa katika nchi ya Gosheni.
Hawa ni mbali na watu wote wa nyumbani kwa Yosefu, na ndugu zake, na wale wote wa nyumbani mwa baba yake. Ni watoto wao, makundi yao ya kondoo, mbuzi na ngʼombe tu waliobakia katika nchi ya Gosheni.
9 Vibandawazi na wapanda farasi pia walikwenda pamoja naye. Lilikuwa kundi kubwa sana la watu.
Magari makubwa na wapanda farasi pia walipanda pamoja naye. Likawa kundi kubwa sana.
10 Hata walipokuja katika sakafu ya kupuria ya Atadi upande mwingine wa Yordani, wakaomboleza kwa majonzi ya huzuni kubwa. Yusufu akafanya maombolezo ya siku saba kwa ajili ya babaye pale.
Walipofika kwenye sakafu ya kupuria nafaka ya Atadi, karibu na Yordani, wakalia kwa sauti na kwa uchungu; Yosefu akapumzika huko kwa siku saba kumwombolezea baba yake.
11 Wenyeji wa nchi, Wakanaani, walipoona maombolezo katika sakafu ya Atadi, wakasema, “Hili ni tukio la kuhuzunisha sana kwa Wamisri.” Ndiyo maana eneo hilo likaitwa Abeli Mizraimu, lililoko mbele ya Yordani.
Wakanaani walioishi huko walipoona maombolezo yaliyofanyika katika sakafu ile ya kupuria ya Atadi, wakasema, “Wamisri wanafanya maombolezo makubwa.” Kwa hiyo mahali pale karibu na Yordani pakaitwa Abel-Mizraimu.
12 Hivyo wanawe wakamfanyia Yakobo kama alivyokuwa amewaagiza.
Hivyo wana wa Yakobo wakafanya kama baba yao alivyowaagiza:
13 Wana wake wakampeleka katika nchi ya Kanaani na wakamzika katika pango katika shamba la Makpela, karibu na Mamre. Ibrahimi alikuwa amelinunua pango pamoja na shamba kwa ajili ya eneo la kuzikia. Alikuwa amelinunua kutoka kwa Efroni Mhiti.
Wakamchukua mpaka nchi ya Kanaani, wakamzika kwenye pango katika shamba la Makpela, karibu na Mamre, ambalo Abrahamu alilinunua kutoka kwa Efroni, Mhiti, pamoja na shamba liwe mahali pa kuzikia.
14 Baada ya kuwa amemzika babaye, Yusufu akarudi Misri, yeye, pamoja na ndugu zake, na wote waliokuwa wamemsindikiza ili kumzika babaye.
Baada ya Yosefu kumzika baba yake, akarudi Misri pamoja na ndugu zake na wale wote waliokuwa wamekwenda naye kumzika baba yake.
15 Nduguze Yusufu walipoona kwamba baba yao amekufa, wakasema, “Itakuwaje ikiwa Yusufu atatukasirikia na akataka kutulipa kikamilifu kwa ajili ya uovu tuliomtenda?”
Ndugu zake Yosefu walipoona kwamba baba yao amekufa, wakasema, “Itakuwaje kama Yosefu ataweka kinyongo dhidi yetu na kutulipa mabaya yote tuliyomtendea?”
16 Hivyo wakamwagiza Yusufu, kusema, “Baba yako alitoa maelekezo kabla hajafa, kusema,
Kwa hiyo wakampelekea Yosefu ujumbe, wakasema, “Kabla baba yako hajafa aliacha maagizo haya:
17 'Mwambieni hivi Yusufu, “Tafadhari samehe makosa ya ndugu zako na dhambi yao uovu waliokutenda.” Basi wasamehe watumishi wa Mungu wa baba yako.” Yusufu akalia walipomwambia.
‘Hili ndilo mtakalomwambia Yosefu: Ninakuomba uwasamehe ndugu zako dhambi na mabaya kwa vile walivyokutenda vibaya.’ Sasa tafadhali samehe dhambi za watumishi wa Mungu wa baba yako.” Ujumbe huu ulipomfikia, Yosefu akalia.
18 Ndugu zake pia wakaenda na kuinamisha nyuso zao mbele zake. Wakasema, “Tazama, sisi ni watumishi wako.”
Ndipo ndugu zake wakaja na kujitupa chini mbele yake. Wakasema, “Sisi ni watumwa wako.”
19 Lakini Yusufu akawajibu, “Msiogope, Je mimi ni badala ya Mungu?
Lakini Yosefu akawaambia, “Msiogope. Je, mimi ni badala ya Mungu?
20 Lakini kwenu, mlikusudia kunidhuru, lakini Mungu alikusudia mema, kuhifadhi maisha ya watu wengi, kama mwonavyo leo.
Mlikusudia kunidhuru, lakini Mungu alikusudia mema, ili litimie hili linalofanyika sasa, kuokoa maisha ya watu wengi.
21 Hivyo basi msiogope. Nitawahudumia ninyi na watoto wenu wadogo.” Kwa njia hii aliwatia moyo na kuongea na mioyo yao kwa upole.
Hivyo basi, msiogope. Mimi nitawatunza ninyi nyote pamoja na watoto wenu.” Akawahakikishia na kusema nao kwa wema.
22 Yusufu akakaa Misri, pamoja na familia ya baba yake. Akaishi miaka mia moja na kumi.
Yosefu akakaa katika nchi ya Misri, yeye pamoja na jamaa yote ya baba yake. Akaishi miaka 110,
23 Yusufu akawaona wana wa Efraimu hata kizazi cha tatu. Pia aliwaona wana wa Makiri mwana wa Manase, waliowekwa katika magoti ya Yusufu.
naye akaona kizazi cha tatu cha watoto wa Efraimu. Pia akaona watoto wa Makiri mwana wa Manase, wakawekwa magotini mwa Yosefu walipozaliwa.
24 Yusufu akawambia ndugu zake, “Ninakaribia kufa; lakini kwa hakika Mungu atawajilia na kuwaongoza kutoka katika nchi hii na kuwapeleka katika nch aliyoapa kumpa Ibrahimu, kwa Isaka na kwa Yakobo.”
Ndipo Yosefu akawaambia ndugu zake, “Mimi ninakaribia kufa. Lakini kwa hakika Mungu atawasaidia na kuwachukueni kutoka nchi hii na kuwapeleka katika nchi aliyomwahidi kwa kiapo Abrahamu, Isaki na Yakobo.”
25 Kisha Yusufu akawaapisha watu wa Israeli kwa kiapo. Akasema, “Bila shaka Mungu atawajilia. Wakati huo mtachukuwa mifupa yangu kutoka hapa.”
Naye Yosefu akawaapisha wana wa Israeli na kuwaambia, “Hakika Mungu atawasaidia, nanyi ni lazima mhakikishe mmepandisha mifupa yangu kutoka mahali hapa.”
26 Hivyo Yusufu akafa, mwenye miaka 110. Wakampaka dawa na akawekwa katika jeneza huko Misri.
Kwa hiyo Yosefu akafa akiwa na umri wa miaka 110. Baada ya kumtia dawa ili asioze, akawekwa kwenye jeneza huko Misri.